Tuesday, February 4, 2020
KITUMBUA CHA KIHINDI SEHEMU YA TATU (3)
“Niseme nisiseme” alizungumza mganga yule kwa sauti nzito
“Sema mganga” alijibu mama Mbingu.
“Mainaya ametupiwa Jini ” alisema mganga huku akichungulia kioo chake.
“Mungu wangu!” alihamaki mama Mbingu.
“Jini?” Magosho akahoji kwa mshangao.
“Ndio tena Jini maiti” mganga alizidi kufafanua.
Magosho, Ashura pamoja na mama Mbingu wakawa wanatazamana wasijue cha kuzungumza. Mganga akavunja ukimya ule.
“Zaidi ya hayo Kuna vitu amelishwa ambavyo sio vizuri” mganga alizidi kuleta changamoto hasa kwa watoto wa mgonjwa.
ENDELEA…3
“Kwahiyo itakuwaje mtaalamu?” Magosho akahoji.
“Tutaanza na kumtapisha hivyo vitu, halafu baadaye tutamtoa huyo jini maiti” alisema mganga kisha akachukua kikapu kilichokuwa na unga mweupe wa mahindi akakiweka pale karibu na mgonjwa. Akamgeukia Magosho na kumwambia achote kiasi fulani cha unga ule na kuuweka kwenye ungo ambao ulikuwa hauna kitu ndani yake. Magosho akafanya kama alivyokuwa ameagizwa na mganga yule. Na baada ya hapo mganga akamwambia Magosho achangue unga ule kuangalia kama kulikuwa na kitu ndani yake. Baada ya Magosho kufanya vile akabaini kuwa kwenye ungo ule hapakuwepo na kitu chochote zaidi ya ule unga aliouweka.
Mganga Kutuzo akachukua dawa kutoka kwenye kibuyu chake kikubwa na kuichanganya na ule unga, akachukua ungo mwingine na kumwambia Magosho afunike ule ungo uliokuwa na unga. Baada ya kitendo kile akachukua mapembe mawili ya mmnyama na kuyaweka juu ya ule ungo. Ukapita muda wa dakika kama tano ambazo mganga alizitumia kuzungumza maneno ya kiganga.
Magosho akaambiwa afunue ungo ule ili kutazama ndani yake kulikuwa na nini. Hakuna kilichoonekena zaidi ya ule unga. Mganga akamwambia Magosho achakue unga uliokuwemo kwenye ungo.
Loo! Magosho alishituka sana baada ya kugusa vitu fulani kwenye unga ule. Lilikuwa ni jambo la kushangaza sana. Vidole viwili vya mkono wa binadamu vilikuwa vimefungwa pamoja na sindano saba za kushonea nguo kwa mkono. Pia kulikuwa na nywele nyeupe ndefu, viwembe saba, kitovu cha mtoto mchanga, pamoja na hirizi ndogo iliyokuwa imefungwa kwa kitambaa cheusi. Vitu hivyo vyote vilikuwa vimefungwa pamoja. Vilikuwa vikitoa harufu mbaya sana.
“Vitu hivi ndivyo vilivyokuwa vinamletea maumivu makali ya mgongo na kuiuno” alisema mganga huku akivifungua vitu vile ambavyo yeye aliviita uchawi. Aliwahakikishia kuwa baada ya tiba ile mama yao asinge lalamika tena kuugua maradhi kama yale.
Mganga akaeleza kuwa sababu ya wachawi kumroga mama yule ni wivu kwasababu mama Ashura alikuwa ni mtu wa kujishughulisha na biashara za kukaanga mihogo na vitumbua, hivyo wakaona anapata sana ndiyomaana wakaamua kumkomesha. Akamalizia kwa kusema kuwa uchawi ule ulitokana na kushirikiana wanaume wawili na mwanamke mmoja.
“Nitawapa dawa ambazo mgonjwa wenu atazitumia, lakini ni lazima tumtoe jini aliyekuwa naye. Ni hatari sana.” Alisema mganga Kutuzo.
“Tawile mganga” mama Mbingu akajibu.
“Sasa ili kumtoa jini huyu kunatakiwa maji ya bahari lita tatu, shuka nyeupe mbili, kaniki tatu, na kitambaa chekundu mita tatu, mchele kilo saba, kisu ambacho hakijawahi kutumika, na mbuzi wawili yaani mweusi na mweupe.” Alimaliza mganga na kumuangalia Magosho ambaye alikuwa akiandika yale maada wakati anayataja.
Kiukweli gharama ya vitu vile ilimchosha Magosho na kupoteza matumaini ya kuvipata. Hata hivyo hakukata tamaa na kumaliza kuandika vitu vyote. Wakakubaliana na mganga kwamba wangerejea mara tu ya kupatikana vitu vile vilivyokuwa vikitakiwa.
*****
Kuugua kwa mama Ashura kulimuumiza sana Magosho kwasababu ni yeye aliyekuwa akitegemewa kwa kiasi kikubwa pale nyumbani. Hakuwa na namna nyingine zaidi ya kupambana kiume. Kwakuwa hali ya mama Ashura haikuwa nzuri ilibidi Ashura ajihusishe na shughuli za kibiashara. Yeye ndiye aliyekuwa akichoma vitumbua na kukaanga mihogo kwa ajili ya biashara. Hata hivyo biashara iliyumba kidogo kwasababu alitakiwa kumhudumia mama yake wakati huo huo..
Magosho alikuwa akitoka na kwenda mjini kuhangaika kufanya vibarua na kupata visenti japo vichache lakini vilisaidia kuendesha maisha ya pale nyumbani kwao. Dawa alizokuwa akizitumia mama Ashura zilionekana kumsaidia kwa kiasi fulani.
Siku zilivyo sogea hali ya mama Ashura ilibadilika tena na kuwa mbaya zaidi. Hadi kufikia kipindi kile watoto wake hawakuwa wamepata fedha za kutosha kuweza kumtibia. Hapakuwepo na namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuuza vitu vya ndani pamoja na nguo zao ili kuweza kupata pesa. Baada ya kuona wamepata pesa za kununulia vifaa vya matibabu wakampeleka mama yao kwa mganga Kutuzo.
Mganga alimtibia mama Ashura kwa takribani siku saba mfurulizo lakini hali ya mama yule haikutengemaa na badala yake ikazidi kuwa mbaya. Aliwapatia dawa za kunywa , kufukiza , na nyingine za kukoga. Hata hivyo hazikumsaidia na badala yake hali ya mgonjwa ikazidi kuwa mbaya.
“Kaka..” Ashura aliita huku akimnywesha uji mama yake.
“Naam” aliitikia Magosho
“Mimi naona tumpeleke mama hospitali”
“Unalosema ni lamsingi Ashura, lakini….”
“Lakini nini?”
“Hapana, nimekuelewa mdogo wangu” Magosho alijifanya hakuwa na kikwazo kumbe alitaka kusema hawakuwa na pesa. Akainamisha kichwa kwa sekunde kadhaa, alipoinuka akamwambia mdogo wake awe makini na mgonjwa yeye kuna mahali alikuwa anakwenda.
Baada ya dakika kama arobaini na tano hivi Magosho alirejea akiwa na kibajaji. Walimpakia mama yao na safari ya kuelekea hospitali ya Muhimbili ikaanza.
Kutokana na foleni walichukua takribani masaa mawili kufika hospitali. Hali ya mgonjwa bado haikuwa ya kuridhisha. Ashura alikuwa akitokwa na machozi muda wote. Magosho alijitahidi sana kujizuia kutoa machozi mbele ya dada yake ili asimkatishe tamaa. Mara kwa mara alikuwa akigeukia pembeni na kujifuta machozi.
Walipofika walimteremsha mgonjwa na kumpeleka mapokezi. Kulikuwa na idadi kubwa sana ya wagonjwa siku ile. Wagonjwa waliandikishwa lakini hawakuweza kutibiwa kutokana na mgomo wa madaktari hao uliokuwa ukiendelea nchini.
Kutokana na hali ile iliyokuwa imetawala pale hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mama Ashura hakupata nafasi ya kutibiwa. Alikuwa ni miongoni mwa wananchi walioathirika kutokana na mgomo ule. Akiwa amepakatwa na Magosho huku akipumua kwa taabu akafumbua mdomo wake na kuzungumza.
“Magosho Baba….” Aliita mama Ashura
“Naam mama” Magosho aliitikia.
“Najua mnanipenda sana. Hata mimi nawapenda pia wanangu” alisema mama Ashura kwa taabu.
“Nikweli mama tunakupenda sana, na bado tunakuhitaji”
“Hamna sababu ya kuhangaika tena. Nirudisheni tu nyumbani”
“Hapana mama, ni lazima tuhakikishe unapona” alisema Magosho na kumeza funda la mate
“Naomba mpendane kama mimi ninavyowapenda wanangu” alisema mama Ashura kwa sauti ya chini iliyo toka kwa taabu.
“Sisi tunapendana mama na tunakupenda pia”
“Wewe Magosho ni mkubwa, mlee mdogo wako na usimtupe”
“Usiseme hivyo, mama”
“Ashura, mpende kaka yako na umheshimu sana, yeye ndiye baba yako ndiye mama yako aliyebaki” Mama Ashura alitoa maneno ambayo yalizidi kumtoa Ashura machozi. Hakuweza kuzungumza kitu zaidi ya kuumia ndani ya moyo wake. Akamshika mama yake mkono na kuuweka kifuani mwake.
“Kwanini unazungumza vitu vya ajabu mama?” Ashura alihoji huku machozi yakidondokea kwenye kiganja cha mkono wa mama yake.
“Mimi ngoja nipumzike wanangu” alisema mama Ashura na kufumba macho yake taratiibu. Viungo vyake vikapoteza joto la mwili na kukaribisha mzizimo. Shingo ikalegea zaidi na kichwa chake kuegemea tumboni kwa Magosho.
Kitendo kile kiliwashitua sana watoto wake hasa kutokana na maneno aliyokuwa akizungumza. Hawakuamini na wala hawakuwa tayari kukubaliana na ukweli wa hali halisi. Mama yao mpendwa alikuwa amekwisha iaga dunia akiwa mikononi mwao.
* * *
Maisha ya Magosho na mdogo wake yalizidi kuwa magumu kila kulipo kucha. Wote wawili walikuwa wakiishi kwenye chumba kimoja kwasababu nyumba yao walikuwa wameiuza ili wapate pesa za kumtibia mama yao. Pesa zote za mradi wa vitumbua na mihogo nazo walizitumia kule kwa mganga Kutuzo kumuagua mama yao jini maiti.
Mtu aliyekuwa akitegemewa na familia ile ya watu wawili alikuwa ni Magosho. Ilimbidi kufanya juu chini kuhakikisha mdogo wake anakula, anavaa, na kulala. Hakuwa tayari kumuona dada yake huyo mpendwa akilala na njaa kitu ambacho pengine kingesababisha kumkumbuka mama yao mara kwa mara.
TUENDELEE
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2RWNqns
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment