Thursday, February 27, 2020
NYUMBA YA MAAJABU 19
Akatoka hadi sebleni ambapo aliangaza macho yake huku na kule ili kumuona Neema ila hakumuona na kumfanya ashangae kwani kawaida ya Neema ni kukaa pale sebleni akiangalia Tv, Ibra alipotazama Tv aliikuta ikiwaka na kuona kuwa ile ni sababu tosha ya kumtimua Neema kuwa anaachaje Tv inawaka wakati yeye hayupo pale sebleni.
Ibra akasogea sasa karibu, alipotazama kwenye kochi alishtuka sana baada ya kuona kuna nyoka amekaa juu ya kochi akiwa amejiviringisha na kichwa amekiinua juu.
*TUENDELEE...*
Kwa kweli Ibra aliishiwa na ujasiri ghafla na kujikuta akipiga kelele kwani hakujua afanye kitu gani kwa muda huo, kelele za Ibra zilimshtua Sophy na kumfanya atoke mbio ili ajue kuwa mumewe amepatwa na nini ila nae alipofika pale sebleni alipatwa na woga wa hali ya juu baada ya kumuona Yule nyoka kwenye kochi na kujikuta akimkumbatia mumewe kwa nguvu huku akiita jina la Neema kama kwamba wanamuhitaji Neema aweze kuwasaidia.
Muda kidogo Neema alitokea na moja kwa moja akamuamuru Yule nyoka atoke nje, kisha akenda kufungua mlango ambapo Yule nyoka alijitoa pale kwenye kochi na kutoka nje kisha Neema akafunga mlango na kuwatazama Ibra na Sophia ambao walikuwa kimya kabisa kwani walikuwa wakitetemeka kwa woga.
Kisha Neema akawaambia kwa kujiamini
“Njooni mkae tuzungumze”
Sophia akadakia,
“Hapana Neema, labda utueleze kwanza Yule nyoka katokea wapi?”
Neema akacheka na kuwaambia,
“Yule sio nyoka ni mtu”
Wote wawili wakashangaa kuwa ni mtu kivipi, kisha Neema akaendelea kuwaeleza,
“Yule ni Jane”
Sophia na Ibra wakashtuka sana kwani hawakutegemea kabisa kuwa Yule nyoka anaweza kuwa Jane, kwahiyo wakauliza
“Ni Jane kivipi?”
“Yote kayataka huyu kaka Ibra, aliyekutuma leo uende kwakina Jane ni nani? Na huyu nyoka alikuja kwa lengo la kuwadhuruu, mshukuru sana uwepo wangu.”
Ibra akashangaa kiasi kuwa huyu Neema amejuaje kuwa yeye alienda kwakina Jane na iweje Jane ajigeuze nyoka wakati alishasema kuwa huyu Neema si mtu mzuri, akajikuta akikosa swali wala jibu. Ni Sophia pekee aliyeweza kuuliza zaidi,
“Inamaana hatorudi tena?”
“Hawezi kurudi kwasababu mimi nipo”
Kisha Ibra akamshika mkewe na kurudi nae chumbani huku akiwa na mawazo lukuki.
Wakiwa chumbani Sophia aliamua kumuuliza Ibra,
“Mume wangu huko kwakina Jane ulikwenda muda gani? Ni nani aliyekushauri uende huko jamani! Mbona unapenda kutafuta matatizo Ibra? Hivi uambiwe na nani kuwa Jane sio mtu mzuri ndio uamini jamani mmh!”
Ibra alikuwa kimya kwanza kwani bado kuna mambo mengi sana yalikuwa yakizunguka akili yake haswa kuhusu huyu Neema na Jane je ni nani wa ukweli kati yao? Ila kwa upande mwingine alimuamini zaidi Jane kuliko Neema, kisha akapanda kitandani na kulala bila ya kuongea ya zaidi na mkewe, hivyo akamfanya Sophia nae apande kitandani na kulala pia.
Wakiwa wamelala, Ibra akajiwa na ndoto ambapo kwenye ndoto ile alikuwa akiona vitu ambavyo vipo kwenye nyumba yao, kwanza kabisa alijiona yupo ndani na kutoka sebleni ambapo akamuona Neema mmoja akiwa jikoni na Neema mwingine akiwa sebleni na gafla Yule Neema wa sebleni akageuka na kuwa nyoka kisha Neema wa jikoni akatoka na kumfukuza Yule nyoka halafu akamuangalia Ibra na kutabasamu kisha akamwambia,
“Mimi ndio Neema, kunikwepa huwezi…….”
Ibra akashtuka kutoka usingizini huku akihema ila akaisikia sauti ya Neema ikiendelea kuongea,
“Na kunifukuza pia huwezi, nimejipa jina hili kwa makusudi kwani huwezi ukaniepuka kamwe”
Kisha akasikia kicheko cha Neema ambapo Ibra akajawa na hofu sana huku akimuamsha mkewe ili nae aweze kusikia ila Sophia alipoamaka hakusikia chochote kwani hata ile sauti ya kicheko haikuendelea tena, Sophia akamuuliza mume wake
“Tatizo ni nini mume wangu jamani?”
“Sophia mke wangu haya ni majanga”
“Majanga! Majanga kivipi?”
“Nimeota ndoto mbaya sana ila yenye uhalisia ndani yake”
“Uhalisia kivipi na ni ndoto gani?”
“Sophia mke wangu, sijielewi sijielewi kabisa. Hebu angalia saa hapajakucha kweli?”
Sophia akaangalia muda na kumwambia mumewe,
“Ni saa nane kamili mume wangu”
“Dah muda hata hauendi pakuche jamani, mimi hata sijui kama nitaweza kulala tena, nitakaa macho tu”
“Hapana usikae macho tulale, hizo ni ndoto tu. Hivi unakumbuka kipindi kile mimi nilipokuwa nikiota ota ulikuwa unaniambiaje Ibra? Basi jua kwamba hizo ni ndoto tu hata zisikupe mawazo tulale mume wangu”
“Tatizo huelewi kuhusu hizi ndoto mke wangu”
“Hata wewe ulikuwa huelewi pia kuhusu ndoto nilizokuwa naota mimi ila napenda kukwambia tena mume wangu kuwa hizo ni ndoto tu zisikutishe”
Sophia alijitahidi kumshawishi mumewe ili waendelee kulala ambapo Ibra nae alijitahidi aweze kulala ila usingizi ulimpiga chenga kwa muda huo.
Kulipokucha kama kawaida, Ibra aliamka na kwenda bafuni kuoga ila kila alipokuwa akioga na kufumba macho aliona sura ya Neema na kumfanya apate hofu kama aliyoipata majuzi yake hivyo akatoka bafuni kwa haraka sana na kumuamsha mkewe ili angalau avae huku akizungumza na mke wake.
Sophia aliamka na kumtazama mume wake ambaye alionekana hata kuoga hakuoga vizuri siku hiyo,
“Ila oga yako siku hizi mume wangu majanga tupu, unatoka na povu jamani”
“Sophia naamini kuna muda utanielewa tu mke wangu”
“Kunieleza hutaki sasa sijui nitakuelewaje”
“Nitakueleza tu hata usijali”
Sophia akamuangalia mume wake kwa makini sana ila hakuweza kumwambia zaidi kwani alijua ni wazi hapendi kuulizwa sana kitu ambacho alisema atamueleza. Kisha Ibra akamwambia Sophia kuwa amsindikize nje kwani ndio alikuwa akienda kwenye shughuli zake ambapo Sophia alifanya hivyo na walipofika sebleni tu ikawa kama jana kuwa Neema alishaandaa chai ili Ibra anywe na akamuomba afanye hivyo kabla ya kuondoka,
“Hapana Neema nimeshachelewa”
“Unajua hata usiku hujala kaka!”
“Naelewa ila hata usijali”
Kisha Ibra akatoka nje na kufuatiwa na mkewe ambaye alitoka nae hadi nje kabisa akimwambia asubiri alitoe gari kwanza, na alipolitoa gari tu alimwambia mkewe apande ili azungumze nae kidogo ambapo Sophia alifanya hivyo,
“Sophy mke wangu, mimi naenda kwenye shughuli zangu ila tu nakuomba kuwa makini sana na huyu Neema, kuwa nae makini kwenye kila kitu kuanzia chakula anachokupikia yani kila kitu. Nakupenda mke wangu, kuna mengi tu nahitaji kuyafatilia kwa undani kuhusu huyu mtu humu ndani”
Kisha akamuaga mke wake na kumbusu kwenye paji la uso, ambapo Sophia akashuka kwenye ile gari halafu yeye akaondoka zake.
Sophia alirudi ndani na kumkuta Neema akiwa kimya pale sebleni ambapo jambo la kwanza kabisa Neema akamuuliza Sophia alichokuwa akizungumza na Ibra,
“Mmh Neema ni mambo ya kawaida tu ya kifamilia”
“Ila hata mimi ni mmoja ya wanafamilia yenu kwahiyo natakiwa kujua vyote vinavyoendelea humu ndani, natakiwa kufahamu kila kitu”
“Hakuna tatizo ila utafahamu taratibu”
“Napenda kuwekwa wazi na kila kinachoendelea hapa ndani, haijalishi amekwambia kuhusu nini ila unapaswa kunieleza”
Kwavile Neema alionekana kumng’ang’ania Sophia amueleze ikamfanya Sophia aamue kuwa kumweleza ukweli vile ambavyo amezungumza na mumewe kwenye gari, Sophia alipomaliza tu kumueleza alishangaa Neema akicheka na kusema,
“Nimefurahi sana kuona Sophia unasema ukweli, basi nakuahidi kuendelea kushirikiana na wewe bega kwa bega na wala usiwe na hofu juu yangu kama unavyoambiwa na mumeo. Tafadhali yapuuzie maneno yake, kinachomsumbua zaidi ni kuwa anafika kwakina Jane na wanamuharibu kisaikolojia”
Sophia akatabasamu tu ingawa kiukweli hakupenda kumwambia Neema kile alichozungumza na mumewe ila ndio hivyo alikuwa ameshamwambia.
Ibra akiwa katika shughuli zake, kuna rafiki yake alipita na kujikuta akizungumza nae mawili matatu kwani hawakuonana kwa kipindi kirefu sana. Pia rafiki yake alimdokeza kuhusu biashara mpya ambayo inaingiza sana faida na kumfanya Ibra atamani kuhusu biashara hiyo kwani alipenda sana kujaribu vitu kwa ajili ya kujiongezea kipato tena ukizingatia kuna mambo mengi yaliingia katikati na kufanya pesa yake iyumbe kwahiyo alifurahi sana kuonana na huyo rafiki yake na kuelezewa kuhusu hiyo biashara.
Rafiki huyu wa Ibra alitamani sana kupafahamu nyumbani kwa rafiki yake kwanza kwani toka amehamia huko hakuwahi kufika,
“Utapafahamu tu Lazaro hata usijali”
“Tena ikiwezekana iwe leo ndugu yangu si unajua duniani hapa mambo mengi sana!”
“Yeah naelewa, basi tutapita mara moja upafahamu kisha twende huko kwenye biashara unayosema.”
“Sawa hakuna tatizo na kwa hakika hii biashara utaipenda sana ndugu yangu”
Wakakubaliana na kuondoka mahali hapo wakielekea nyumbani kwa Ibra kwanza kisha waende kwenye hiyo biashara ambayo Ibra aangalie inavyokwenda na kama ataweza kuifanya na kuendelea kujiongezea kipato.
Walipofika nyumbani kwa Ibra kwa kweli Lazaro alishangaa sana ile nyumba ya rafiki yake kuwa kapata wapi pesa ya kuweza kumiliki nyumba yote ile,
“Mjini mipango Lazaro”
“Kweli mjini mipango yani kwa stahili hii mmh! Nimeshangaa kwakweli maana sio kawaida kabisa. Nakumbuka nilikuwa na uwezo kukuzidi ila nyumba yangu mimi ni ya kawaida tu ila mwenzangu upo kwenye mjengo wa maana. Hongera sana kaka”
“Nashukuru ndugu yangu, karibu sana”
Walishuka kwenye gari na kisha Ibra akafungua mlango wa ndani na kumkaribisha Lazaro ndani ambapo walimkuta Sophia na Neema wakiwa sebleni wamekaa kama kawaida, Ibra akawasalimia ila Lazaro alimsalimia Sophia tu ambapo Ibra akamshtua kuwa huyu mwingine hajamuona ila Lazaro akahamaki tu,
“Yupi huyo?”
“Inamaana humuoni hapo?”
Ibra alimuonyesha alipo Neema ila Lazaro bado hakuonyesha kama amemuona mtu yeyote eneo hilo na alikuwa akimshangaa tu Ibra huku akimwambia,
“Hebu acha masikhara Ibra unataka nimsalimie nani tena wakati nimemuona shemeji tu”
Sophia akamaliza mjadala kwa kuwakarabisha wakae, ila bado Ibra hakuridhishwa na hali ile na kufanya ajaribu kumuuliza kitu Neema aone kama kweli Lazaro hajamuona huyu Neema.
“Neema hujamuona huyu mgeni na wewe?”
Neema akamtazama tu Ibra bila ya kumjibu chochote huku maongezi mengine yakiendelea pale sebleni ambapo Lazaro aliwalalamikia kuwa nyumba yao inaonekana kuwa ni nzito sana,
“Hii nyumba ni nzuri ila ni nzito sana”
“Nzito kivipi?”
“Mnatakiwa mtafute watu wa maombi ili muifanyie maombi nyumba yenu ikae sawa”
Sophia akaguna na kuuliza,
“Mmh maombi tena?”
“Ndio maombi ni muhimu sana maana naona nyumba yenu ni nzito jamani”
Ibra akamtazama mkewe kisha akamtazama Neema ambaye alionekana yupo makini sana kutazama Tv, kisha Ibra akamuuliza Neema
“Unasikia kinachoongelewa huku?”
Neema alikuwa kimya tu na alimuangalia kisha akaendelea kuangalia Tv, Ibra akachukia sana na kumfanya ainuke na kwenda kuzima Tv moja kwa moja kwenye soketi ya kuingiza umeme kisha akarudi tena kukaa.
Ila Lazaro nae aliaga na kumuomba aende nyumbani kwake, Ibra akamuuliza kuhusu wao kwenda kule kwenye biashara.
“Sitaweza kwenda tena maana hapa nilipo kichwa kimeanza kunigonga naomba niondoke tu”
Lazaro akainuka na kufanya Ibra nae ainuke ili amsindikize, walipotoka nje Lazaro alionekana kuwa na kizunguzungu kikali sana ambapo ilibidi Ibra ampakie kwenye gari yake na kuitoa nje kabisa huku akitaka kumpeleka hospitali ila Lazaro aligoma na kuhitaji kurudishwa tu nyumbani kwake ambapo ikabidi Ibra afanye hivyo.
Sophia alibaki ndani na Neema huku akijiuliza kimoyomoyo kuwa kwanini Neema alikuwa hamjibu chochote Ibra halafu bado alionekana kimya kabisa ingawa Tv ilikuwa imezimwa na Ibra kwa hasira.
Sophia aliamua kumuongelesha yeye sasa ili aone kama atajibiwa kitu chochote,
“Neema mbona kimya sana mdogo wangu?”
Neema alikuwa kimya tu hakujibu chochote kile na kumfanya Sophia azidi kumshangaa kwani haikuwa kawaida kabisa kwa Neema kufanya hivyo. Sophia akainuka pale alipokaa na kusogea alipo Neema ili kumshtua kwa kumshika kabisa, ila aliposogea ili amguse ghafla akashangaa kuwa pale hapakuwa na mtu yoyote yani Neema hakuonekana ghafla.
Kwakweli Sophia alipigwa na butwaa kwani muda wote alikuwa akimuona Neema mahali hapo halafu tena ghafla Neema ametoweka, alijikuta akitetemeka tu na kuwa kama mtu asiyejielewa.
Itaendelea………………….!!!
✍ By, Atuganile Mwakalile.
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/399l6Ew
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment