Tuesday, February 25, 2020

NYUMBA YA MAAJABU





Ibra alikuwa akimshangaa tu mkewe ambapo kabla hata hajasema chochote, Sophia alianguka chini na kuzimia.
*TUENDELEE...*

Ikabidi Ibra ambebe mke wake na kwenda kumpakia kwenye gari kisha kumpeleka moja kwa moja hospitali huku akihisi kuwa pengine mkewe ana malaria imempanda kichwani ndio mana anaongea mambo yasiyoeleweka.
Walifika hospitali na moja kwa moja kupokelewa na wahudumu wa hospitali ile ambapo muda kidogo tu Sophia alionekana kuzinduka na kuwa sawa kiasi ambapo Ibra aliingia na mkewe kwa daktari na kuelezea kwa kifupi matatizo ya mke wake ambapo daktari aliwatajia vipimo vya kupima.
Walimaliza kufanya vipimo na wakaa mapokezi wakisubiri majibu na kuitwa na daktari. Muda wote Ibra alikuwa akimtazama mkewe kwani alimuona kama mtu mwenye matatizo sana kwa kipindi hicho, Sophia alimuuliza mumewe,
“Mbona unaniangalia sana bila ya kusema chochote?”
“Kwa kweli sina usemi mke wangu ingawa kuna mambo mengi sana najiuliza kuhusu wewe”
“Kama mambo gani?”
“Nadhani tutaongea zaidi tukirudi nyumbani, ngoja kwanza daktari atupe majibu ya vipimo ulivyofanyiwa”
Muda kidogo daktari aliwaita na walipoingia ofisini tu daktari alianza kwa kumpongeza Ibra,
“Hongera sana bwana Ibra, mkeo ni mjamzito”
Ibra akatabasamu kiasi kisha akamuuliza daktari,
“Kwahiyo tatizo lake ni mimba tu au kuna lingine?”
“Hakuna lingine lolote, ni mimba tu. Tena itakuwa vyema kama mkiwahi kuja kuanza na kliniki ili kujua maendeleo ya mtoto aliyeko tumboni”
“Sawa daktari, kwa hivyo hakuna tiba yoyote anayoweza kupatiwa?”
“Mr. Ibra, mimba si ugonjwa wa kutibiwa huwa ni hali tu inatokea kwa mwanamke kutokana na kile kitu tofauti kinachojitengeneza kwenye mwili wake. Cha muhimu kujua kuwa mkeo ana mimba na unatakiwa kuwa nae karibu sana ili uweze kumsaidia baadhi ya mambo. Mkianza kliniki mtajifunza mengi zaidi kwa hivyo mzingatie hilo.”
“Sawa basi tumekuelewa daktari, tutafanyia kazi ushauri wako”
Kisha daktari akampatia Sophia dawa za vitamin ambazo zingemsaidia kiasi kwa hali aliyokuwa nayo kwa kipindi hicho halafu wakaanza safari ya kurudi nyumbani kwao.
Walipokuwa njiani kurudi wanapoishi, wakamuona mtoto mdogo barabarani kwa makadirio anaweza akawa kwenye miaka mitatu, alionekana kusimamisha gari yao kama kwamba anaomba msaada ila Ibra alipita bila kusimama ambapo mbele Sophia alimshika mkono na kuonyesha kutokufurahishwa na kitendo cha Ibra cha kumpita mtoto Yule aliyeonekana kutaka msaada.
“Hivi Ibra inamaana Yule mtoto hukumuona?”
“Aaah Sophy, mtoto mdogo kama yule anawezaje kusimama barabarani na kusimamisha gari jamani!! Mambo mengine tutumie akili ya ziada tu mke wangu”
“Sijapenda Ibra yani sijapenda kabisa kabisa”
“Kwahiyo unatakaje?”
“Turudi ili tujue ana tatizo gani”
“Hivi unajua kama hata majambazi wanawatumiaga watoto wadogo mke wangu! Tusije tukajitafutia matatizo bure jamani”
“Hata kama turudi tu kwa kweli, hivi wewe huna hata huruma jamani! Mtoto mdogo vile unaanza kumuwekea imani za majambazi mmh! Turudi tafadhali.”
Ibra hakutaka kumkwaza mke wake tena ukizingatia kwa ile hali yake ya ujauzito aliyoambiwa na daktari, hivyo basi akarudisha gari nyuma kwa lengo la kumfata Yule mtoto.
Walifika pale ambapo Yule mtoto aliwasimamaisha na walimkuta pale pale ambapo Ibra alisimamisha gari kisha Sophia akashuka na kumchukua Yule mtoto kisha akapanda nae kwenye gari na kujaribu kumuuliza anapoelekea ambapo Yule mtoto aliwaonyesha kwa kidole tu anapoelekea kisha Ibra akaondoa gari na kuanza kwenda alipoonyesha Yule mtoto.
Walifika mahali kisha Yule mtoto akasema,
“Simama hapa hapa”
Ibra alisimamisha gari ila kwa hofu kiasi kwani hakutegemea kama Yule mtoto anaweza kuongea ukizingatia mwanzo aliwaonyesha kwa mkono tu.
Kisha Sophia akafungua mlango kwa vile alikuwa amempakata mtoto huyo na kumshusha akizani labda kuna maelekezo mengine Yule mtoto atayatoa, ila Yule mtoto alivyoshuka tu aliwatazama na kuwaambia,
“Asanteni kwa kunikaribisha rasmi kwenye maisha yenu”
Akapunga mkono kisha akaondoka kwa kukimbia ambapo kwa sekunde chache tu alipotea kwenye macho yao.
Ibra na Sophia wakatazamana kisha Ibra akamuuliza mkewe,
“Hivi umemuelewa huyu mtoto?”
“Mmmh hata sijamuelewa”
Ibra nae akaguna kisha akaondoa gari mahali pale na kuendelea na safari yao ya kurudi nyumbani.
Walipofika nyumbani ilionyesha wazi kuwa Ibra alichoshwa kabisa na Yule mtoto ambaye walikutana nae njiani kwani ilikuwa ngumu sana kwake kuelewa msaada ambao Yule mtoto aliuhitaji kutoka kwao, kisha akamuuliza tena mke wake
“Hivi Yule mtoto ulimuelewa?”
“Hapana hata sikumuelewa”
“Safari ijayo usiwe na roho ya huruma kiasi kile itatuponza, huruma muda mwingine sio nzuri”
“Lakini tumepungukiwa na nini mume wangu kumsaidia Yule mtoto jamani? Hata Mungu atatuongezea thawabu”
“Thawabu zipo ila si kwa staili ile ya Yule mtoto, natumaini hakuwa na nia mbaya juu yetu”
“Mtoto Yule bhana hawezi kuwa na nia mbaya kwa kweli”
“Sawa”
Kisha Ibra akabadilisha mada na kumpongeza mke wake kwa mimba aliyobeba,
“Hongera sana mke wangu, sasa furaha yetu itaenda kukamilika”
Sophia akatabasamu kisha akamsogelea mumewe na kumkumbatia kwani aliona mawazo yake yakianza kutimia juu ya wao kuwa na watoto wa kutosha mle ndani.
“Hongera na wewe pia mume wangu maana hii ni furaha yetu sote”
“Yani sipati picha kumshika mwanangu akizaliwa maana nitafurahi sana kumuona kwa kweli, itakuwa furaha kubwa sana ya maisha yangu”
“Mimi je! Nitafurahi sana sana maana sasa nitakuwa nimepata mtu wa karibu, siku ya kwanza kumshika na kumnyonyesha nitafurahi sana”
Walionekana kutabasamu na kufurahia ambapo muda huu ibra alionekana kumuuliza mkewe kuwa atapendelea kula chakula gani maana alitaka kujitolea siku hiyo kupika kwaajili ya mke wake, Sophia akatabasamu na kumjibu mumewe kuwa atakula chakula chochote tu.
“Leo nitakupikia mwenyewe Sophy, tafadhali wewe pumzika tu hapo nipike fasta fasta tule”
Sophia akatabasamu na kukaa kwenye kochi huku akihisi kuwa mumewe anafanya mbwembwe tu kwani alijua muda wowote atamshtua kuwa akapike mwenyewe, Ibra alikwenda jikoni na kumuacha Sophia pale sebleni ambapo kwa muda mfupi kabisa Sophia alipitiwa na usingizi pale pale kwenye kochi.
Wakati Sophia amelala pale kwenye kochi akajiwa na ndoto ambapo kwenye ndoto hiyo akamuona Yule mtoto waliyemkuta kule njiani, alionekana akitabasamu huku akimuangalia Sophia na kumwambia,
“Nitakuwa nakusaidia kazi zote ngumu na hata zile nyepesi zikiwa nyingi nitafanya mimi, napenda ukarimu wako ila huyo mtoto ajaye atakuwa ni ndugu yangu mimi sababu yeye nitampenda zaidi”
Sophia alijikuta akimuuliza huyu mtoto,
“Kivipi?”
Huyu mtoto alionekana akicheka tu bila kuongeza neno la ziada na kumfanya Sophia ashtuke sana kwenye ile ndoto na kujikuta kama akipiga kelele hivi ambapo Ibra alimfata mbio na kumuuliza kuwa kuna tatizo gani.
“Vipi Sophy mke wangu ni nini tatizo?”
“Mmh nimeota ndoto hata siielewi”
“Ndoto gani hiyo?”
“Nimemuota Yule mtoto tuliyemkuta njiani”
“Sophy mke wangu nakuomba uachane na habari za Yule mtoto kwani naona wazi zitakuchanganya tu, yani fanya hivi kwenye akili yako kuwa hatujawahi kukutana na Yule mtoto maana bila ya hivyo sidhani kama itakuwa rahisi kumsahau. Bora ujiwekee kuwa hatujawahi kukutana nae kabisa, Yule mtoto hafai kumuweka akilini kwani hakuwa mtoto wa kawaida kabisa”
“Kwanini unasema hakuwa mtoto wa kawaida?”
“Wewe fikiria hata alipoingia tu kwenye gari alionyesha kuziendesha akili zetu na kujikuta tukifanya anavyotaka yeye kama vile kumpeleka pale alipopataka tena kwa maelekezo ya kidole tu, kwakweli Yule mtoto si wa kawaida hatutakiwi kumuweka akilini mke wangu.”
“Sawa nimekuelewa mume wangu”
“Twende basi tukale”
“Mmh hata nina hamu ya kula basi!!”
“Njoo tule hivyo hivyo kidogo kidogo”
Ikabidi Sophia asogee na mumewe mezani na kuanza kula, kwa kweli alimpa hongera mumewe kwa chakula kile maana kilikuwa kitamu sana,
“Asante ingawa nimekipika kawaida tu yani hata mimi mwenyewe nashangaa kuwa kitamu hivi”
Sophia akatabasamu kwani mumewe alimshangaza sana kusema kuwa hata yeye anashangaa utamu wa chakula wakati kakipika mwenyewe.
Walipomaliza kula, Sophia alitoa vile vyombo na kuvipeleka jikoni kisha akaviosha ambapo muda huo Ibra alikuwa sebleni.
Sophia alipomaliza kuosha vile vyombo, ikamjia kumbukumbu ya zile nguo chafu ambazo aliziloweka pia ikamjia kumbukumbu ya vile alivyozikuta kwenye kamba kuwa zilishafuliwa na kuanikwa, ni hapo hapo akakumbuka kuwa hiyo ndio sababu iliyomfanya azimie hapo kabla.
Kwahiyo alipotoka jikoni tu, moja kwa moja akaelekea uwani ambako huwa anafua nguo zake, alipofika uwani safari hii hakuona nguo yoyote chafu wala za kwenye kamba hakuziona. Akapata wazo la kwenda chumbani kuangalia, ambapo alifika chumbani na kufungua kabati alikuta zile nguo zote zilishakunjwa na kupangwa kabatini, kwakweli Sophia akaguna na kujiuliza kidogo.
“Inamaana Ibra ndio kafanya haya mambo? Ndio lazima tu atakuwa yeye tu maana hakuna mwingine wa kufanya haya.”
Kisha Sophia akatoka chumbani na kurudi sebleni na kwenda kukaa karibu na Ibra kisha akamwambia,
“Asante mume wangu kwa kunisaidia udobi”
“Udobi? Udobi gani tena?”
“Si zile nguo chafu umezifua zote na kuzianua kisha umezipanga kabatini”
“Mmh mbona kama sikuelewi!”
“Hunielewi kivipi wakati zile nguo umeshaanuwa na kupanga kabatini”
Ilionyesha Ibra alikuwa haelewi kitu kwakweli, ikabidi Sophia amshike mkono na kumpeleka mpaka uwani pa kufulia ambapo hapakuwa na nguo yeyote kwenye kamba, kisha akampeleka chumbani na kufungua kabati ambapo alimuonyesha nguo zikiwa zimepangwa vizuri kabatini, Ibra akamtazama Sophia na kumuuliza
“Nani kafanya yote haya?”
“Unaniuliza mimi tena! Si wewe hapo”
“Sijafanya hiki kitu mimi”
Wakajikuta wakitazamana kwa muda kidogo, huku wakiwa na hofu kwa mbali.

Mwisho wa sehemu ya 4

Itaendelea ……………..!!!






from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2TePXJd

No comments:

Post a Comment