Thursday, February 27, 2020
NYUMBA YA MAAJABU
Sophia akiwa na mashuka yake mkononi kwa lengo la kumpelekea Neema, aliingia kwenye kile chumba na kumkuta Neema akiwa amesimama tu ila kitanda kilikuwa kimetandikwa vizuri kabisa tena kwa mashuka mazuri.
*TUENDELEE...*
Kwa kweli Sophia alishangaa sana na kumtazama Neema kwa mshangao zaidi ila huyu Neema hakuonekana na hofu yoyote ile na kufanya Sophia amuulize,
“Neema, kitanda kimetandikwa na nani? Na je mashuka yametoka wapi hayo?”
Neema hakujibu ila naye alimuuliza swali Sophia,
“Kwani umeyapenda dada haya mashuka?”
Sophia alizidi kushangazwa kwani hakutegemea na yeye kuulizwa swali badala ya kujibiwa swali lake kwahiyo ilikuwa kamavile ni kitu kinachomchanganya zaidi, kisha kabla hajaongeza neno lolote akamshangaa tu Yule Neema akimpokea yale mashuka na kisha kumshukuru sana kwa kumletea,
“Asante dada kwa haya mashuka kwani nayo ni mazuri sana dada yangu”
Bado Sophia hakuweza kuongeza neno lolote zaidi ya kutoka mle chumbani na moja kwa moja akaelekea chumbani kwake kwani hata sebleni alipitiliza, Ibra alikuwa ametulia tu pale sebleni akimuangalia mkewe akipitiliza chumbani na kuhisi kuwa huenda kuna vitu ambavyo mkewe alivisahau huko chumbani kwani kwa matarajio yake alihisi kuwa mkewe alipomaliza kupeleka yale mashuka angerudi pale sebleni waweze kuzungumza.
Muda kidogo ni Neema aliyetoka na kwenda kukaa sebleni ambapo alimtazama tu Ibra bila ya kuongea chochote kile, Ibra nae hakuchukua muda mrefu akainuka pale sebleni na kuelekea chumbani.
Alipofika chumbani alimkuta mkewe akiwa amelala kabisa kamavile ni muda mrefu aliingia kulala, moja kwa moja Ibra alihisi kuwa ni uchovu wa mimba ndio umemfanya mkewe awe katika ile hali kwani haikuwa kawaida yake hapo zamani, ila Ibra nae alipanda kitandani na kujilaza karibu na mkewe ambapo kwa muda mchache tu naye usingizi ulimpitia.
Walipokuja kushtuka muda tayari ulikuwa umeshaanda tena aliyeanza kushtuka alikuwa ni Ibra na kumuamsha mkewe,
“Sophy, Sophy tumelala sana mke wangu amka”
Sophia nae aliamka na kuanza kujinyoosha kwa uchovu huku akijihisi kuchoka sana, kwa pamoja wakainuka na kutoka chumbani ambapo walimkuta Neema akiwa pale sebleni tena alionekana kuyazoea sana mazingira yale kupita maelekezo kwani alikuwa sawa na binti ambaye amekuwa pale kwa siku zote. Ambapo walipofika tu sebleni aliwakaribisha mezani kuwa chakula tayari, hakuna aliyehoji kati yao kuwa ni nani aliyemwambia Neema kupika au kumuelekeza cha kupika bali walielekea mezani wote na kuanza kula huku huyu Neema akiwa anaendelea na shughuli nyengine.
Alianza Sophia kukisifia kile chakula kuwa ni kitamu sana huku akiyasifu mapishi ya Neema kuwa ni binti aliyefundwa vyema, Ibra nae alimsapoti mkewe kwa kummwagia sifa za kutosha huyu Neema. Hadi wanamaliza kula ilikuwa ni kumsifia Neema tu pale mezani.
Walipomaliza tu Neema alikuja na kutoa vile vyombo na kuvipeleka jikoni moja kwa moja kisha Sophia na Ibra wakarudi sebleni na kukaa ambapo neema alikuwa ameiwasha ile Tv ambayo walikuwa wakiogopa kuiwasha kwa siku zote mle ndani.
Hakuna aliyemuuliza chochote Neema kwani wote walitulia na walionekana kuridhishwa na uwepo wake mle ndani, ingawa mara nyingi sana walimuona huyu Neema akiwaangalia sana ila hawakuweza kuhoji kitu chochote kile zaidi ya kutabasamu tu.
Usiku ulipoingia zaidi, Sophia na Ibra walielekea chumbani kwao huku Neema nae akielekea chumbani kwake.
Walipokuwa chumbani, Ibra aliamua kumuuliza mkewe kilichompelekea mchana kwenda kulala bila ya kumtaarifu.
“Ilikuwaje kwani maana nilikukuta umelala hoi kabisa au ndio mambo ya mimba tena?”
“Naelewa basi! Hata sielewi, nilikuja chumbsni sijui hata kufanya nini nikashangaa usingizi ulipotokea loh yani nimelala usingizi mzito kupita maelezo ya kawaida.”
“Duh pole mke wangu, najua ni mimba hiyo inayokusumbua ila mambo yatakuwa sawa baada ya miezi kadhaa tu.”
“Na hapa tumbo halijakua vizuri je likikua sijui itakuwaje”
“Utazoea tu mke wangu ila ni vyema kama ukianza kliniki si unajua wanasema ni bora kuanza mapema!”
“Naelewa mume wangu nitaanza tu hata usijali”
“Ila unasema hivyo kila siku halafu wala huonyeshi uhitaji wa kuanza kabisa hata sijui kwanini?”
“Ngoja tumbo litokee tokee kwanza”
“Mmh jamani Sophy, mbona watu wanaanza mapema unataka tumbo litokeeje?”
“Khee Ibra hao wanaoanza mapema umewaona wapi? Ushawahi kukaa na mwanamke mjamzito wewe?”
“Basi yaishe mke wangu ila ni vyema kuanza kliniki”
“Sawa nitaanza hata usijali”
Sophia akajinyoosha pale kitandani na kulala, muda huo huo ikawa kama amelala kwa muda mrefu kwani alikuwa na usingizi mzito sana na kufanya Ibra amtazame tu kisha na yeye akalala.
Ibra alipolala tu akajiwa na ndoto, ile ndoto ilimuonyesha kuwa Yule nyoka mkubwa waliyemuona mlangoni kwao hakuwa nyoka kweli bali alikuwa ni huyu Neema waliyekuwa nae ndani kwani alivyokuwa akimuona kwenye ndoto alimuona akibadilika badilika mara akiwa mtu na mara akiwa joka. Kisha akamuona Jane akiingia pale ndani kwao na ghafla Yule nyoka akayeyuka halafu akaonekana chini ya mti mahali ambapo ndio pale pale walipoenda kumkuta Neema akiwa amejiinamia.
Kwakweli Ibra alishtuka sana kwani hakutegemea kama anaweza kupata ndoto ya namna ile ukizingatia huyo Neema ndio wanaishi nae ndani kwa kipindi hicho, jasho lilikuwa likimtoka sana Ibra na kumfanya ashindwe kuendelea kulala kabisa kwani alikaa tu kitandani kwa muda huo, kisha akakumbuka jinsi mkewe nae anavyopata ndoto ambazo huwa zinamfanya akose usingizi kabisa kwakweli na leo ilikuwa zamu yake yeye.
Kulipokucha Ibra aliamka na kujiandaa kwaajili ya kwenda kwenye shughuli zake, kisha akamuamsha na mkewe kwa kumuaga kuwa anatoka kwa muda huo, hivyo Sophia aliinuka ili aweze kufunga mlango pale mumewe anavyotoka ila walipofika sebleni walimkuta Neema akiwa tayari ameshaamka, alikuwa amekaa tu akiangalia Tv ikabidi wamsalimie huku Sophia akimuuliza kuwa mbona mapema sana.
“Ndio kawaida yangu kuamka mapema huwa silali kupitiliza”
“Sawa ndio vizuri ila duh unawahi sana”
“Hata usijali kitu dada yangu”
Ibra akawaaga pale na kuondoka, ndani alibaki Neema na Sophia ambapo Sophia alirudi chumbani na kuendelea kulala.
Ibra akiwa njiani kwakweli alijikuta akikosa imani kabisa kumuacha mkewe na Neema ukizingatia mkewe ni mjamzito halafu Neema ni mgeni kwenye ile nyumba yao, akajiwa na wazo kuwa ni bora akamwambie Jane nae aende pale kwake ili awe nao pamoja kuliko mkewe kubaki mwenyewe na Yule Neema ambayo hawamfahamu vizuri.
Ibra aligeuza gari na moja kwa moja akaelekea kwakina Jane ambapo kama kawaida alimkuta mama yake Jane akiwa ndiye pekee aliyeamka huku akifanya shughuli za nyumbani kwake, hivyo akamsalimia na kuomba aitiwe Jane, ila leo mama Jane nae alifunguka
“Ila nyie mpaka mumtoe mwanangu ngeo ndio mtaona raha maana sio kwa kumuita ita huko halafu akifika kwenu mnamfanyia vituko. Au unafikiri habari zenu sikuzipata? Kwanza mwanangu Jane bado kalala labda uje badae.”
Ibra hakutaka kupingana na huyu mama ukizingatia ni kweli mambo ambayo walimtendea Jane hakuna mzazi yeyote anayeweza kuridhishwa au kufurahishwa nayo, hivyo Ibra akawa mpole tu na kumuaga huyu mama kuwa atarudi tena badae.
Ibra akaondoka pale kwakina Jane na kuelekea kwenye shughuli zake ila mawazo yake yalikuwa ni juu ya mkewe kwani alijikuta ghafla akikosa amani kabisa dhidi ya uwepo wa Yule Neema pale nyumbani kwao ukizingatia na ile ndoto aliyoota ndio kabisa yani.
Sophia sasa aliamka vizuri na kwenda sebleni tena ambapo alimkuta Yule Neema akiangalia tu Tv ila kazi za mle ndani zote zilikuwa zimefanyika, Sophia alikaa nae huku akizungumza nae kwa furaha sana.
“Kwakweli Neema nimekupenda bure maana wewe ni mchapakazi sana na hata sikukutegemea kabisa kama utakuwa hivi”
“Usijali dada mbona utazidi kufurahia uwepo wangu, yani utafurahia sana na kujilaumu kuwa kwanini umechelewa kugundua uwepo wangu”
“Ni kweli kabisa maana wewe hata sio mtu wa kupigishana kelele ukizingatia unafanya kazi zako kwa wakati.”
Neema akatabasamu tu, kisha akamwambia Sophia kuwa hata chai alishamuandalia mezani ambapo Sophia alienda moja kwa moja kunywa chai ile ambapo alikuta ni chai ya maziwa, chapati na mayai. Sophia alikunywa bila hata ya kuhoji kuwa vile vitu vimenunuliwa muda gani hadi kupikwa kwani alihisi huenda mumewe alinunua bila hata ya kusema.
Alipomaliza kunywa chai alirudi chumbani kukoga ili kupata nguvu mpya ambapo alikoga na kwenda kukaa kitandani huku akijikuta akifikiria mambo mawili matatu.
“Inamaana Neema zile chapati kazipika au kazinunua? Kama kazipika unga ametoa wapi? Na kama amezinunua basi pesa alipewa na nani? Hivi Ibra anaweza kutoa pesa bila ya kunishirikisha kweli? Vipi kuhusu yale mayai mmh! Itakuwa ni ibra tu ila hata hivyo chakula kilikuwa kitamu sana.”
Sophia akatulia na kuanza kuvaa kisha akatoka tena na kwenda sebleni ambapo Yule Neema alikuwa pale pale sebleni akiwa ametulia akiangalia Tv tu, ambapo Sophia alimuuliza
“Huchoki Neema kuangalia Tv?”
Neema akatabasamu tu na kudai kuwa anapenda sana kuangalia Tv kuliko kitu chochote na kama akichoka basi ataizima, Sophia hakutaka kuongea zaidi kwani alihisi anaweza kumfanya Neema achukie bure ukizingatia hoja yake ilikuwa ni kumwambia kuwa tv inahitaji kupumzika kwani sio vizuri kuwa inaonyesha muda wote.
Walikaa pale sebleni kwa muda kidogo na hata mchana iliwakutia pale pale, muda kidogo Neema akamwambia Sophia kuwa chakula cha mchana kilikuwa tayari mezani, Sophia alimuangalia na kumuuliza kuwa amekipika muda gani kwani kwa kumbukumbu zake walikuwa wote hapo sebleni kwa muda wote pamoja.
Neema akatabasamu na kumwambia Sophia,
“Tulikuwa wote ndio ila wewe muda mwingi ulikuwa unasinzia, mimi nimekwenda kupika nimekula hata hujajua. Pole dada, ila ni hali yako hiyo ndio imekufanya hivyo”
“Kheee kwani unajua kama mimi nina mimba! Nani kakwambia?”
“Si ngumu kumgundua mwanamke mjamzito tena ikiwa mtu unauzoefu nao ndio kabisa yani, mi hata mtu mwenye mimba ya siku moja namjua sembuse hiyo mimba yako ya miezi mitatu jamani”
Sophia akashtuka kuona kuwa Neema amejua hadi muda wa mimba yake kuwa ina miezi mitatu,
“Khee umejuaje kama mimba yangu ina miezi mitatu?”
“Mimi hata mimba ya siku moja nagundua kutokana na kukaa sana karibu na bibi yangu, tena mimba yako wewe hiyo miezi mitatu ipo wiki ya mwisho maana wiki ijayo itaanza mwezi wa nne. Yani usijali chochote, mimi nilishaisoma hali yako dada nenda kale upate nguvu maana mimba inataka uwe unakula hata kwa kujilazimisha ila uwe unakula ili kumfanya mwanao akue vizuri”
Sophia hakuongea zaidi ila aliinuka na kwenda mezani kula ambapo alikula vizuri sana tofauti na siku nyengine ambavyo huwa anakula kwa kujivuta vuta, alikuwa akifurahia tu utamu wa kile chakula kwa muda ule.
Alipomaliza kula alirudi pale sebleni na kukaa tena na Neema ambaye alionekana makini sana katika kuitazama ile Tv kamavile kuna vitu vya maana anavyovitazama kwani alionekana kuwa makini mno.
Sophia akamuuliza tena Neema kuwa anapendea nini kutazama Tv muda wote na kumuuliza kuwa kama hachoki kutazama vile.
“Si nilishakujibu dada kuwa napenda kuangalia Tv kuliko kitu chochote kile kwahiyo wewe usijali, au hupendi niwe naangalia?”
“Hapana, wee angalia tu Neema”
Sophia aliamua kujivunga tu kwa muda huo ingawa kiukweli hakupenda kwavile aliona Tv inakosa muda wa kupumzika.
Ibra aliwahi kutoka kazini siku hiyo kwani alihitaji kuzungumza na Jane na pia kumuomba awe anaenda nyumbani kwake pindi yeye akiwa kazini, kwahiyo moja kwa moja safari yake ilikuwa ni kuelekea kwakina Jane. Alipofika kwa bahati nzuri alimkuta Jane akiwa mwenyewe nje ya nyumba yao na kumuomba kwa ajili ya mazungumzo,
“Jane samahani nimekuita kwa pembeni kwavile naogopa mama yako asije akaniona bure. Tafadhali twende wote nyumbani kwangu nataka kuongea nawe kidogo tu”
Jane akaingia kwenye gari ya Ibra bila hata kuhoji maswali ya ziada, kisha Ibra akaendesha gari ambapo alipokaribia na nyumbani kwake alilisimamisha na kuzungumza kidogo na Jane.
“Kwanza unaendeleaje maana mama yako asubuhi alifoka sana hata sijui alijuaje”
“Dunia haina siri, siku ile nimepiga kelele kuna watu walimueleza mama na vile nilivyorudi naumwa mama aliniuliza sana mwisho wa siku sikuweza kuendelea kumficha na nikaamua kumwambia ukweli”
“Sawa hakuna tatizo Jane hata hivyo tulifanya makosa sana, ila kuna kitu kimoja nilikuwa naomba unisaidie”
“Kitu gani hicho?”
“Pale nyumbani tumepata msichana wa kazi ila mimi nimejikuta kutokumuamini kwakweli, sasa nilikuwa naomba pindi nikiwa kazini uwe unaenda pale nyumbani mara kwa mara kumuangalia mke wangu na ikiwezekana hata uwe unashinda pale pale”
Jane akajifikiria kidogo ila hakukataa na kumfanya Ibra afurahi kisha akamuomba kwa muda huo aingie nae ndani ili angalau amfahamu huyo mdada wa kazi waliyempata.
Ibra alisogeza gari yake mpaka getini kabisa kisha akashuka pamoja na Jane kuelekea ndani, na walipofika Ibra alifungua mlango wa ndani na kuingia ambapo Sophia na Neema walikuwa pale pale sebleni.
Ila Jane alipomuona Neema alishtuka sana na kufanya wote wamshangae kilichomshtua kiasi kile.
Itaendelea……………….!!!
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2T4Eayf
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment