Thursday, February 27, 2020
NYUMBA YA MAAJABU 12
Ikabidi washuke wote na kuingia kwa tahadhari ili kama ni nyoka basi wajue cha kufanya kabla ya kuingiza gari ndani, ila walipoingia tu getini waliona nyoka mkubwa akiwa amejiviringisha pembezoni mwa mlango wao wa kuingia ndani kanakwamba anawasubiria kuwa waingie nae.
*TUENDELEE...*
Kwakweli hapakuwa na mwenye ujasiri kati yao wa kuweza kuendelea mbele, Ibra alimuangalia mkewe na kumuuliza,
“Tutafanyaje sasa?”
“Wewe ni mwanaume unatakiwa ujue cha kufanya”
“Yani uanaume kwa joka lote lile, mbona hunitakii mema mke wangu!”
“Sasa tutafanyaje?”
“Nadhani tuondoke tukatafute hoteli ya kulala kwa leo, lile joka tushughulike nalo kesho maana giza nalo hilo limeshaingia, hakuna namna hapa. Tutampata nani muda huu wa kutusaidia kulimaliza joka kubwa vile?”
Ikabidi wakubaliane kufanya hivyo maana haikuwa kitu rahisi kwa wao kupambana na lile joka, na kwa jinsi giza lilivyoingia haikuwa rahisi kusema utatafuta watu ili waweze kulimaliza joka lile.
Wakarudi nje na kupanda kwenye gari yao kisha kuondoka na kuelekea hoteli nyingine ya karibu ili kuangalia ustaarabu wa kupata chumba na kulala, kwa bahati nzuri walipata chumba kwenye hoteli ambayo walikwenda kwa muda huo.
Ila mpaka wanaingia ndani kila mmoja alikuwa na mawazo yake kuhusu lile joka waliloliacha nje ya nyumba yao, Sophia alimuuliza mumewe,
“Hivi joka kubwa kama lile linaweza kutokea wapi mjini hapa?”
“Kwakweli hata mimi sielewi Sophy maana sio hali ya kawaida kabisa ile, tena mjini hapa jamani kukutana na nyoka kama Yule mmmh!”
“Mi nahisi ametumwa Yule mume wangu”
“Inawezekana kabisa unayoyasema maaana si kitu rahisi kwa mjini hapa kukutana na nyoka mkubwa kiasi kile”
“Sasa unahisi tufanyeje?”
“Kwakweli hata sijui, nahisi kuchanganyikiwa tu”
“Mmmh mi nahisi kesho twende kwa da Siwema atupeleke kwa yule mganga ili aweze kutusaidia kwa hili, yani Yule nyoka ni wa kutumwa kabisa kabisa si jambo la kawaida mume wangu”
“Unafikiri nitabisha? Hata siwezi kubisha mke wangu, yani sibishi chochote kwakweli katika maisha yangu sijawahi kuona nyoka mkubwa kama Yule zaidi ya kuona kwenye sinema tu. Kwakweli haya ni makubwa, na kama ni uchawi basi ni uchawi wa wazi wazi kabisa yani”
Sophia aliridhika na kauli ya mumewe ya kukubali kwenda kwa mganga ili pia aweze kuwaeleza zaidi kuhusu Jane kwani alipenda mumewe nae aelewe kwa kina ubaya wa Jane anayemtetea kila siku.
Ibra aliona ni vyema wakapumzisha mawazo hivyobasi akamuomba mkewe walale tu ili kesho yake waamkie huko kwa Siwema, Ibra alimsogelea mkewe pale kitandani na kumkumbatia ili wapate kulala kwa pamoja. Na haikuchukua muda wote wawili wakajikuta wakipitiwa na usingizi.
Sophia alianza kupatwa na ndoto ambapo katika ndoto hiyo aliona lile tukio ambalo liliwapata wakati wakitoka hotelini kula ambapo aliona tukio zima la Yule mtoto alivyopanda kwenye gari yao na jinsi Ibra alivyomshusha kwa ghadhabu, ila kwenye hii ndoto alimuona huyu mtoto akiwaambia kuwa,
“Nitawakomesha”
Sophia alijikuta akishtuka kutoka usingizini huku jasho jingi likimtoka ambapo Ibra nae alishtuka huku akimshangaa mkewe na kumuuliza kuwa imekuwaje tena,
“Ndoto mume wangu”
“Ndoto! Ndoto gani?”
Ghafla wakasikia mtu akiita jina la Sophia kwa nguvu kutoka nje ya hoteli hiyo ambapo Sophia alitaka kuitika ila Ibra alimziba mdomo na kumkataza.
“Usipende kuitika unapoitwa usiku, je unajua anayekuita ni nani na ana lengo gani na wewe?”
Sophia akahema kwa nguvu sana na kumuuliza mumewe,
“Hivi kwanza kuna mtu anayenifahamu huku?”
“Ndio ushangae sasa, hakuna anayekufahamu je utakuwa unamuitikia nani? Hata kama ukiwa mahali kwa watu wanaokufahamu tafadhali mke wangu usipende kuitika usiku, yani wewe chukulia kwamba anayeitwa sio Sophia wewe, chukulia kwamba kuna Sophia wengi sana ulimwenguni huenda kuna mmoja ndiye anayeitwa lakini sio wewe. Usiitike kabisa mke wangu”
Ile sauti ya kumuita Sophia nayo ilikazana na kumfanya Sophia kuingiwa na woga ila mumewe alijaribu kuongea nae na kujitahidi kumtoa ile hali ya uoga ili awe katika hali ya kawaida kabisa na ahisi kuwa anayeitwa sio yeye.
Sauti ile iliita na kuita ila mwishowe ikafifia kabisa na kuwa kimya ila bado Sophia hakulala na kumfanya Ibra nae asiweze kulala kwani alikuwa akimpa maneno ya kumfanya mkewe asijisikie vibaya hata kidogo.
Kwavile hawakuwa na usingizi, ikabidi Ibra amuulize Sophia kuhusu kile alichokiota ambapo Sophia alimueleza lile tukio aliloliota na jinsi mwishoni alivyoambiwa na Yule mtoto, kidogo Ibra akapata wazo jipya na kumwambia Sophia,
“Unaona sasa, unakumbuka ule mchana ilikuwa sauti kama ile tuliyosikia ikikuita na tuliposimamisha gari ndio akapanda yule mtoto wa maajabu halafu saizi unaota tena na sauti inaanza kukuita tena, je huwezi kuona kuwa matukio yanawiana hayo!”
“Mmh halafu kweli mume wangu, bora umenikataza kuitika”
“Ndio hivyo, nadhani alitaka uitike ili awe na uhakika na chumba tulicholala. Ondoa mashaka mke wangu, tulale kwa amani sasa maana hawajui tumelala chumba kipi”
“Kwahiyo kama ni watu wabaya basi wamechemka”
“Tena wamechemka haswaaa”
Ibra akamkumbatia mkewe kisha wakaanza kuutafuta usingizi na hatimaye wakalala tena.
Kulipokucha, waliamka mapema sana na kwenda kukoga ili kujiandaa kutoka pale hotelini, ambapo walitumia muda mfupi tu kujiandaa kwani hawakuwa na mengi ya kufanya.
Wakati wanatoka pale hotelini walishangaa kuna mahali watu wengi sana wamejaa na kufanya washuke kwenye gari yao na kwenda kushuhudia kuwa ni kitu gani kimetokea, waliposogea walishangaa kumuona binti mmoja pale chini akiwa ameuwawa kikatili sana ila muda mfupi tu walifika maaskari ambao ilionyesha walipewa taarifa kuhusu Yule mtu aliyeuwawa ambapo walimfunika na kumpakiza kwenye gari yao na kuondoka na baadhi ya watu kwa maelezo zaidi.
Ibra alikuwa akishangaa sana na kufanya nae aulize kwa kina kama sehemu hiyo huwa kuna matukio yoyote ya ajabu,
“Eti kaka, kwani hapa huwa kuna matukio ya hivi?”
“Kwakweli kaka haijawahi kutokea yani ndio mara ya kwanza na kila mmoja anashangaa maana hatujawahi kupatwa na matukio ya hivi halafu ubaya zaidi ni kuwa haijulikani ameuliwa na kitu gani”
“Mmh ndugu zake wamepatikana?”
“Kwakweli ilikuwa ngumu kumtambua ila kuna binti mwingine alipita hapa na ameweza kumtambua, hivyo amekimbia kwao kuwaita ndugu zake nadhani wakifika hapa itabidi waelekee moja kwa moja polisi au hospitali maana polisi wamewahi kufika”
Muda kidogo walifika watu kama wamechanganyikiwa kabisa huku wakitaka kuonyeshwa huyo marehemu ambapo watu waliwapa maelekezo juu ya polisi waliofika na kuchukua ule mwili wa marehemu, kati ya wale watu alisikika mama mmoja akilia sana huku akiongea,
“Mungu wangu jamani, naomba unisaidie asiwe binti yangu kweli jamani, yani Sophia wangu mimi hapana haiwezekani kabisa”
Wengine walimuita dereva wa bajaji aliyewapakiza wale na kuelekea nao kwenye kituo cha polisi ili waweze kuwahi kumuona huyo marehemu kabla hajapelekwa monchwari.
Sophia alimuangalia mumewe na kumuomba kuwa waondoke eneo lile kwani tayari alihisi kuchanganyikiwa baada ya kusikia kuwa Yule binti aliyeuwawa aliitwa Sophia pia, Ibra alimsikiliza mkewe na kisha wakaelekea kwenye gari ambapo moja kwa moja safari yao ilikuwa ni kwenda kwa Siwema na hakuna aliyeongea kwa muda huo.
Walipofika nyumbani kwa Siwema walimkuta akijiandaa kwaajili ya majukumu yake mengine, hata na yeye alishangaa ujio wao ila kwa haraka haraka akahisi kuwa huenda Yule binti ameshakufa kwahiyo ndio wamekuja kumpa habari, kwahiyo aliacha alichokuwa anafanya na kwa shauku kubwa alitulia kuwasikiliza kilichowapeleka mahali pale.
Sophia hakutaka kupoteza muda na moja kwa moja akaanza kumueleza yaliyotokea nyumbani kwao mpaka kuwafanya wao kuamua kuja kwake ili awapeleke huko kwa huyo mganga.
“Kheee mbona makubwa jamani! Je na hii asubuhi huyo joka mmemuacha hapo mlangoni?”
“Hata nyumbani hatujaenda tena, usiku tumelala hotelini kwakweli hali ni mbaya, twende tu kwa huyo babu akatusaidie jamani”
“Basi ngoja nijiandae fasta fasta twende jamani maana haya mambo ni makubwa sana”
Siwema akaingia ndani, muda kidogo akapita tena Yule bibi ambaye alimwambia Sophia kuwa nyumba yake ni ya maajabu ila huyu bibi hakuwasalimia wala nini zaidi ya kumsemesha Sophia kwa kumwambia,
“Una bahati sana, ushukuru mumeo ana upeo mkubwa”
Sophia akamshangaa huyu bibi na kumuuliza kwa jazba,
“Kivipi”
“Usiku ule ungeitika wakati unaitwa basi sidhani kama muda huu ungekuwa hapa, ingawa umemuingiza pabaya mtu ambaye hakustahili kabisa”
“Sikuelewi ujue”
“Ni ngumu kunielewa kwasababu huwa naongea ukweli mtupu, mnatakiwa muwe karibu sana na Mungu lasivyo ile nyumba itawashinda”
“Nyumba na kuitwa usiku vina uhusiano gani?”
Kabla huyu bibi hajajibu, Siwema alikuwa kashatoka ndani na hapo hapo akaanza kumfokea Yule bibi kwa kumfukuza.
“Hivi wewe bibi una mpango gani na familia yangu? Si nilishakwambia usipite hapa nyumbani kwangu tafadhali ondoka mchawi mkubwa wewe tena ukome kukatisha hapa”
Yule bibi aliondoka bila ya kuongea chochote za ziada ingawa alionekana kuondoka akiwa amenyong’onyea, ikabidi Ibra nae amuulize Siwema kwa ukaribu kuwa Yule bibi ni vipi
“Yani Yule bibi ni mchawi hakuna mfano nawaambia halafu huwa anajifanya kila kitu anakijua, Sophia nilikwambia lakini usipende kumsikiliza huyu bibi hata nashangaa unavyomsikiliza jamani. Haya twendeni tusije tukachelewa foleni huko kwa babu”
Ikabidi Ibra afungue gari na wakapanda wakielekea kwa mganga wa kienyeji sasa.
Walipofika kwa mganga kama kawaida walikuta foleni kubwa tu maana mahali hapo palikuwa hapakosi watu hata mara moja.
Ila waliamua kuvumilia kwenye foleni hadi pale ilipofika zamu yao na kuingia ambapo mganga alikuwa amekaa na matunguli yake ila alikuwa kimya kabisa mpaka pale wao walipoanza kumueleza ambapo Siwema alianza kwa kumuomba msamaha kwanza,
“Babu tusamehe, nadhani tumekosea masharti na yametupata makubwa. Nje ya nyumba kuna nyoka mkubwa amefanya tushindwe kuingia ndani”
Huyu babu alianza kuongea kwa jazba,
“Mnajua nyie ni wajinga sana, tena wajinga haswaa yani mlishindwa kujiuliza kuwa kwanini ile dawa iliganda? Na nani aliwatuma muende kuitupa nje?”
Sophia nae akaanza kujitetea,
“Tusamehe babu, kwakweli hatukujua cha kufanya. Tusamehe tafadhali, tunaomba msaada wako”
“Ile dawa ni kali sana, mara nyingi mimi huitoa kwa lengo la kummaliza mchawi kwamaana ile dawa mtu akiinywa hawezi kuepuka kifo hata afanye kitu gani. Ile dawa ilitakiwa inywewe na muhusika ambapo angeinywa tu angeona habari yake kwanza wadudu wa tumboni wote wangekuwa wakubwa maradufu na hao ndio wangemuua kisha kuanza kumtoka hovyo hovyo yani kila sehemu ya uwazi kwenye mwili wake ingetoa wadudu ambao wangekuwa wakubwa sana na hakuna ambaye angeweza kukaa karibu na mwili wa marehemu huyo kisha wangekwenda kumzika mapema sana. Sasa nyie mmeitupa pale nje kwenu tena ikiwa imekauka vile, ubaya wa ile dawa ikikauka tu harufu yake huwavutia viumbe jamii ya nyoka. Pale kwenu palikuwa na nyoka mdogo ambaye amekunywa ile dawa na mwisho wa siku ndio kawa vile. Hata mkirudi tena kumuona mtakuta amekuwa mkubwa zaidi ya mwanzo na huwa ni vigumu sana kuwaua nyoka waliokula ile dawa kwani ukiwasogelea tu hukimbilia kukudhuru kwanza”
Ibra alihisi kuchoka kabisa kwa maelezo haya, kisha akamuuliza Yule mganga,
“Sasa tutafanyaje babu?”
“Hapo dawa ni moja tu, tunatakiwa tutoe kafara ya ng’ombe mzima”
“Ng’ombe mzima?”
“Ndio ng’ombe mzima tutamchinja kisha damu yake tutaiweka dawa ambapo huyo nyoka ataifata hiyo damu kisha atajifia mwenyewe halafu tutachinja kondoo na mbuzi kwa lengo la kumfanya huyo nyoka atoweke kabisa”
Ibra alijikuta akiwa na mawazo lukuki maana hakujiandaa kwa hayo maswaibu ya kununua ng’ombe mzima wa kafara kisha kondoo na mbuzi. Yule mganga akawasisitizia kabisa,
“Hiyo kazi inatakiwa ifanyike leo, yani leo maana kadri huyo nyoka atakavyozidi kukaa ndio itakavyokuwa ngumu kumtoa”
“Basi babu ngoja tulete pesa kwaajili ya kununua huyo ng’ombe, mbuzi na kondoo”
Kisha wakatoka nje ambapo Ibra alikuwa na mawazo tu muda wote, alichukua simu yake na kuwapigia rafiki zake akiwaomba wamkopeshe pesa maana aliona akiitoa kwenye biashara yake atafanya iyumbe mapema sana.
Kwa bahati nzuri aliowapigia na kuwakopa walimtumia pesa bila hata kukawia na kufanya ashukuru sana ili akakamilishe hilo zoezi na waweze kurudi kwao.
Ila Ibra alijikuta akimlaumu sana mkewe na kumuona kuwa ni mwanamke mpumbavu maana yote hayo kayasababisha yeye kwa kutaka kummaliza Jane na mwisho wa siku wamejikuta wakiingia kwenye gharama zisizo na maana.
Walikwenda kumtaarifu mganga kuhusu upatikanaji wa fedha kisha vile vitu vikenda kutafutwa ili kujiandaa kwa hiyo shughuli ya kumtoa Yule nyoka nyumbani kwa Ibra.
Walipofanikiwa kupata vitu vyote, kwanza kabisa Yule ng’ombe alichinjwa pale pale nyumbani kwa mganga ambapo mganga aliweka damu ya Yule ng’ombe kwenye chupa na kuiweka na dawa.
“Yani hapa nataka tukifika tu kitu cha kwanza iwe ni kuimwaga hii damu maana haitakuwa vyema kwenda kumchinja ng’ombe mbele ya Yule nyoka.”
Kisha mbuzi na kondoo nao wakachinjwa ambapo damu yao iliwekwa kwenye chupa moja na kuchanganywa.
“Sasa akisha kunywa hii ya ng’ombe, atakufa kisha tutammwagia hii ya kondoo na mbuzi ili atoweke.”
Kisha wakenda kupanda kwenye gari, Ibra, mganga, msaidizi wa mganga, Siwema na Sophia. Safari ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa Ibra.
Walipofika nyumbani kwa Ibra, walishuka wote kwani Ibra alisimamisha gari yake nje kisha wakasogelea geti na kufungua kwa tahadhari, cha kushangaza sasa pale ambapo walimuacha nyoka jana walimkuta Jane amekaa tena akiwa hana habari yoyote.
Itaendelea…………….!!!
.
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2voNNib
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment