Tuesday, February 25, 2020
NYUMBA YA MAAJABU 8
Alipoingia jikoni alishangaa sana kuona vyombo vyote vimeoshwa na vimeshapangwa kabatini kwakweli alijikuta akipiga kelele na kumfanya Ibra amfate kwa haraka sana,
“Vipi Sophia nini tena mke wangu?”
“Misukule”
“Misukule! Misukule imefanyaje?”
Ibra alikuwa akimshangaa mkewe na kuangaza macho yake huku na kule kuangalia kama kuna chochote.
*TUENDELEE...*
Ila Ibra hakuona chochote mle jikoni na kumuuliza tena mke wake,
“Sophy, misukule kivipi?”
“Misukule imekosha vyombo na kuvipanga”
“Misukule imekosha vyombo na kuvipanga? Wee Sophy akili yako iko sawa kweli? Unajua misukule wewe?”
Ibra alikuwa akimshangaa mke wake na kumuona kama ni mtu aliyekuwa akichanganyikiwa maana mambo aliyokuwa akiongea hayakuwa na mantiki yoyote ile.
Aliamua kumuinua mkewe pale chini na kuelekea nae chumbani kwani alikuwa kama kapigwa na bumbuwazi.
Walipokuwa chumbani sasa, Ibra aliamua kumuacha kwa muda kitandani kisha yeye kwenda kuelekea kukoga kama alivyokuwa amepanga.
Kwakweli Sophia hakujielewa kabisa na kuhisi hadithi za Jane za kuhusu misukule zikianza kumuingia akilini vilivyo na kuona ni kweli ile nyumba yao ina misukule maana kila akiangalia yale matukio kengele ya hatari ndivyo ilivyozidi kulia katika ubongo wake.
Wakati akiwaza hayo akasikia kama mlango wa sebleni ukifunguliwa na kufungwa kama kwamba kuna mtu kaingia au katoka ila akajiuliza kuwa itawezekanaje ikiwa alishafunga mlango huo wakati wanaingia ndani, kwakweli woga ulimshika mpaka pale Ibra alipotoka bafuni kuoga na kumkuta mkewe akiwa amejikunyata.
Ibra alimfata mkewe na kukaa naye karibu kisha akamkumbatia na kumuuliza kwa ukaribu zaidi,
“Kwani nini tatizo mke wangu? Unajua Napata shida sana kukuelewa!”
“Ibra hata mimi sielewi kwakweli yani sielewi kabisa kabisa”
“Unajua kwangu inakuwa ngumu sana kwa sababu sijawahi kuishi na mwanamke mjamzito maana inawezekana haya ni mambo ya kawaida kwa wajawazito ila mimi sielewi kwakweli. Inabidi unifafanulie mke wangu kuwa ni mambo gani yanakusibu au ni vitu gani unaviona ili nijue tunaanzia wapi kupata ufumbuzi”
“Tatizo Ibra nikisema huniamini, hebu sikia tulitoka hapa tumeenda kumsindikiza Jane ila kulikuwa na vyombo vichafu jikoni, tumerudi ili nikavioshe nakuta vyote vimeoshwa wakati humu ndani tupo mimi na wewe tu. Nimekaa hapa nasikia mlango wa sebleni ukilia sasa hayo mambo yanamaana gani mume wangu?”
“Mmh kama hayo mambo ni ya kweli basi kuna makubwa”
“Mi nahisi kuna misukule humu ndani”
“Hebu Sophia tusiongelee hizo habari maana usiku huo unakuja tutashindwa kulala”
Kisha Ibra akamuomba mkewe ajiandae ili angalau watoke waende mahali wapate kubadilisha hali ya hewa.
Sophia alipomaliza kujiandaa, yeye na mumewe wakatoka mle ndani na kufunga milango vizuri kabisa kisha wakapanda kwenye gari yao na moja kwa moja Ibra akaelekea na mkewe hotelini ili kutimiza lengo lake la kubadilisha hali ya hewa ila kichwani alikuwa na maswali mengi sana ambayo hayakuwa na majibu kwa wakati ule.
Kikubwa alichowaza ilikuwa ni kama Sophia anaongea ukweli kuhusu yale matukio basi lazima kuna kitu kinaendelea kwenye ile nyumba yao, pia akawaza kuwa kama ni kweli basi huenda majirani zao ni wachawi.
Ibra alikuwa kimya tu huku akinywa juisi taratibu ambapo Sophia akamuomba kuwa kesho yake ampitishe kwa Siwema ili akamsalimie,
“Basi kesho asubuhi unavyoondoka naomba mi ukaniache kwa Da’ Siwema nikamsalimie maana nimemkumbuka sana.”
“Mmh kwa nikujuavyo wewe utataka kumwambia mambo yanayotokea nyumbani, tafadhali usimwambie kabla hatujayafanyia ufumbuzi”
“Wala hata sina nia hiyo ya kumwambia, mi nataka nikamsalimie tu”
Ibra alikubaliana na mke wake ingawa alielewa wazi lengo la mkewe ni nini ukizingatia huwa hawezi kukaa na kitu moyoni, wakazungumza zungumza pale kisha wakarudi nyumbani.
Wakati wanarudi kama kawaida wakamuona Yule mtoto akisimamisha gari yao kama ile siku ya kwanza ila kwakweli leo Ibra hakutaka huu ujinga kabisa na akapita kama vile hajaona chochote na kufika mbele akasema kuwa hawatokwenda tena kula kwenye ile hoteli kwani aliona kamavile inamahusiano ya moja kwa moja na Yule mtoto ambaye wanamkuta njiani.
Walifika nyumbani na moja kwa moja wakenda kulala kwani Ibra hakutaka kupoteza muda wa kujiwekea mawazo ya tofauti.
Kulipokucha kama walivyopanga, Ibra alijiandaa huku Sophia nae akijiandaa kisha wakatoka kwa pamoja na kufunga milango kama kawaida.
Ibra alimpeleka Sophia mpaka kwa Siwema na kumuacha hapo, ambapo Sophia alimgongea Siwema ila alikaa kwa muda bila ya kufunguliwa na kumfanya aamue kukaa nje ya nyumba hiyo akimsubiri huyo Siwema.
Baada ya masaa kama mawili, Siwema alitoka ndani tena alionekana akiwa amechoka choka hivi na alipomuona Sophia alimshangaa sana na kumuuliza
“Khee Sophia mbona asubuhi asubuhi! Umefika hapa saa ngapi?”
“Nimefika muda tu dada, nimegonga weee ila hujanifungulia ndio nikaamua kukaa hapa nje.”
“Pole sana kwakweli hata sikusikia kugonga kwako jamani, karibu Sophy. Kwanza najishangaa leo kuchelewa kuamka kiasi hiki jamani”
Siwema akamkaribisha Sophia ndani kisha wakakaa pamoja huku Siwema akitamani kujua kilichompeleka Sophia mahali pale kwani haikuwa kitu cha kawaida kwa Sophia kwenda pale tangu alipohama.
“Vipi kwema lakini?”
“Kwema tu dada”
“Kwahiyo naweza kwenda kukoga kisha tukaendelea na maongezi ya hapa na pele?”
“Ndio dada wala hata usijali kitu”
Siwema aliinuka na kwenda kukoga ili kuondoa uchovu wake kisha akaandaa chai na kuanza kunywa, ila Sophia alipokunywa kidogo tu alikimbia nje na kutapika hivyobasi kumfanya Siwema awe na mashaka juu ya afya ya Sophia.
“Vipi mdogo wangu au twende hospitali?”
“Hapana dada, nadhani nimetapika kutokana na mimba niliyonayo”
“Wow, una mimba Sophy!”
“Ndio dada”
“Kwakweli hiyo ni khabari njema, hongera sana mdogo wangu. Cha msingi kwasasa ni kuzingatia chakula bora ili kuufanya mwili wako upate afya na nguvu. Kula matunda kwa wingi na mboga za majani”
“Asante dada”
“Vipi umeshaanza kliniki?”
“Bado sijaanza ila nitakwenda kuanza”
“Ni vyema ukaanza kliniki mapema mdogo wangu kwani inasaidia kujua ukuaji wa mtoto na pia kuangalia mwenendo mzima wa afya yako”
“Hakuna tatizo dada huko kliniki nitakwenda tu ila yaliyonileta hapa leo sio hayo ni mengine kabisa”
“Mmh yepi hayo tena Sophy?”
Sophia akaanza kumueleza Siwema kuhusu mambo ambayo ameyaona hivi karibuni katika nyumba yake, pia akamuelezea kuhusu Jane jinsi walivyozoeana na jinsi ambavyo Jane amekuwa akimsimulia kuhusu habari za misukule. Pia akamsimulia kuhusu kile chakula ambacho Sophia alihisi kuwa kimepikwa na Jane kwa dakika mbili, na kumueleza alivyofahamiana na mama Jane hadi yeye kuwa karibu na huyo Jane.
Siwema akapumua kidogo na kumuangalia Sophia kisha akamuuliza,
“Hivi mpaka hapo hujaelewa mchezo mzima unaondelea mdogo wangu?”
“Kivipi dada?”
“Hebu kwanza niambie huyo Jane anajishughulisha na nini?”
“Jane kamaliza kidato cha nne kwahiyo huwa yupo nyumbani tu akisubiri matokeo”
“Mmmh mdogo wangu hapo akili kichwani mwako, huyo binti kwanza hashindwi kukupiku kwa mumeo ukizingatia kila mumeo anapokula chakula chake anakisifia kuwa kitamu sana, kwanza umenieleza hapa kuwa huyo binti wala hawana matumaini nae kuwa atafaulu au la kwahiyo mama yake hashindwi kumlengesha kwa Ibra ili angalau hata awe mke wa pili ampunguzie majukumu”
“Jamani dada mbona hayo mapya sasa, inamaana na haya maajabu ya ndani kwangu yanasababishwa na yeye?”
“Ndio, hisia zangu zinanituma kuwa huyo binti atakuwa mchawi yani ingawa simjui ila naona kabisa kuwa ni mchawi, na yote anayafanya ili kukutisha na nyumba yako. Anataka uiogope nyumba yako na ikiwezekana uondoke ili ajilengeshe kwa Ibra. Yaani usipokuwa makini utashangaa anaolewa na yeye, si vizuri kuokoteza majirani mdogo wangu mwisho wa siku unapata ya kuyapata kama hivi”
“Mmh au ndiomana ananitishia na stori zake za misukule?”
“Ndio, anataka uoanishe matukio na stori zake ili upatwe na uoga halafu mwisho wa siku uone nyumba mbaya na uikimbie nyumba yako aingie yeye. Hivi unafikiri ni nani asiyetamani kuishi kwenye jumba la kifahari kama lile? Nani asiyependa maisha ya raha unayopewa wewe na mumeo? Hakuna Sophy, kila mwanamke anatamani kuishi vizuri kwa furaha na amani unatakiwa uwe makini sana”
“Nashukuru dada ila nitafanyaje kumuepuka?”
“Kwanza kabisa mzuie kuja nyumbani kwako, halafu pili kuna mtaalamu nitakupeka atatupa dawa ili tumzuie kabisa kabisa kukanyaga na mauchawi yake.”
“Kwahuyo mtaalamu tutakwenda lini sasa?”
“Nadhani itakuwa vyema tukenda kesho, wataalamu hawaibukiwi hovyo hovyo. Inatakiwa kudamka asubuhi na mapema na kuelekea huko.”
Wakaendelea na stori mbali mbali huku Siwema akimfundisha Sophia namna ya kutunza mimba aliyokuwa nayo na jinsi ya kumtunza Ibra hata katika hicho kipindi cha ujauzito wake.
Jane kama ambavyo aliongea na akina Sophia jana yake na jinsi ambavyo walimuomba kuwa na siku hiyo ende nyumbani kwao ili akampe kampani Sophia, alipoamka tu alienda kujiandaa kisha kumuaga mama yake kuwa anakwenda nyumbani kwa Sophia,
“Mmmh kushakunogea tayari!”
Jane akatabasamu kisha akamuaga mama yake na kuelekea huko kwa Sophia.
Alipofika, alikuta geti liko wazi kabisa na kushangaa kuwa imekuwaje wamesahau hata kurudishia geti lile akajiuliza na kuingia kisha akalirudishia huku akiongea
“Usikute dada Sophy bado hajatoka nje maana si kawaida hili geti kuwa bwamu kiasi hiki”
Alipofika mlango wa ndani aligonga ila hakufunguliwa na kujaribisha kufungua ambapo nao ulifunguka na kumfanya Jane aingie ndani na kukaa pale sebleni huku akiita.
“Dada, dada, dada Sophy”
Ila hakujibiwa, moja kwa moja akahisi kuwa huenda Sophia amekwenda Sokoni ila kwanini hakufunga milango? Akajipa jibu kuwa huenda aligundua kuwa atafika ndiomana hakufunga milango.
Alikaa kaa pale na kuamua kuwasha video huku akimsubiri Sophia arudi ila wakati akiangalia alijikuta akipitiwa na usingizi na kulala pale pale kwenye kochi.
Ibra alipomaliza shughuli zake aliamua kumfata Sophia kule nyumbani kwa Siwema ili aweze kurudi nae nyumbani, alimkuta mkewe akiendelea na maongezi mbalimbali na Siwema ambapo naye alijumuika kidogo kisha kuaga.
“Ila kabla ya yote shemeji napenda kukupongeza kwa ujauzito alionao mdogo wangu”
Ibra alitabasamu kidogo na kushukuru huku akitoka nje na Sophia, ila Sophia akamuuliza tena Siwema,
“Vipi hiyo kesho nije au wewe utakuja nyumbani?”
“Itakuwa vyema kama ukija Sophy”
Kisha Sophia na Ibra wakapanda kwenye gari na safari ya kurudi kwao ikaanza.
Wakiwa kwenye gari Ibra alimuuliza mkewe,
“Kwahiyo siku hizi habari itakuwa ni hii ya kuletana kwa Siwema au?”
“Mmmh jamani Ibra si leo na kesho tu, au kama utashindwa basi nitakuja mwenyewe”
“Haya basi usinune maana na wewe siku hizi kitu kidogo tu unanuna, ila tabia yako sijaipenda”
“Ipi tena?”
“Yani mimba changa hivyo umeshaanza kuitangaza mmh!”
“Jamani Ibra kwani kuna ubaya gani kumwambia Da’ siwema jamani wakati ni kama ndugu yangu!”
“Sawa umefanya vyema ila kiukweli mimba haitangazwi, acha itajitangaza yenyewe”
Sophia akanyamaza kwani aliona kamavile ni malumbano kidogo na mume wake.
Wakiwa wanaendelea na safari yao, ibra akapita karibia na njia ya ile hoteli ambapo mbele kidogo walikaona kale katoto ila leo kalionekana kamelala chini na kumfanya Sophia ashtuke sana kisha Ibra akamwambia,
“Achana na habari za hako katoto, hakana jema na maisha yetu wala usishtuke. Safari ijayo sitapita tena njia hii”
Wakaendelea na safari yao hadi walipofika kwenye nyumba yao.
Sophia alishuka na kufungua geti kisha Ibra akaingiza gari ndani halafu wakafunga geti na kufungua mlango wa kuingia ndani, kwakweli Sophia alishtuka sana kumuona Jane akiwa amelala kwenye kochi na kuita Ibra kwa nguvu aliyekuwa akipaki gari lake vizuri.
Ibra aliingia ndani huku nae akishangaa kwani halikuwa jambo la kawaida, Sophia alishikwa na hasira sana na kumsogelea Jane pale kwenye kochi na kumkurupua kwa kumpiga ambapo jane nae alishtuka kama chizi na kuanza kupiga kelele za mwizi tena kwa nguvu kabisa.
_Mwisho wa sehemu ya 8_
Itaendelea…………………!!!
✍ By, Atuganile Mwakalile.
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/3a2oGQT
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment