Tuesday, February 25, 2020
NYUMBA YA MAAJABU 5
5⃣
Ilionyesha Ibra alikuwa haelewi kitu kwakweli, ikabidi Sophia amshike mkono na kumpeleka mpaka uwani pa kufulia ambapo hapakuwa na nguo yeyote kwenye kamba, kisha akampeleka chumbani na kufungua kabati ambapo ilionyesha nguo zikiwa zimepangwa vizuri kabatini, Ibra akamtazama Sophia na kumuuliza
“Nani kafanya yote haya?”
“Unaniuliza mimi tena! Si wewe hapo”
“Sijafanya hiki kitu mimi”
Wakajikuta wakitazamana kwa muda kidogo, huku wakiwa na hofu kwa mbali.
*TUENDELEE...*
Kila mmoja alihisi kuwa mwenzake kuna kitu anamficha hivyo wakajikuta wakiwa kimya kwa muda.
Ibra akaona ni vyema kupotezea hayo mambo ili asije akalumbana na mke wake bure, kwahiyo alichokifanya ni kumshika mkono na kurudi nae sebleni kisha kuanza kuongea nae mambo mbalimbali kuhusiana na mipango yake.
“Sophy mke wangu, inatakiwa katika akili zetu sasa tuanze kupanga mipango kuhusu mtoto wetu ajaye, kwanza kabisa nakushukuru sana mke wangu kwa hiyo zawadi uliyoibeba tumboni mwako kwa ajili yangu”
Sophia akatabasamu kwani maneno ya mume wake yalimpa faraja sana, kisha nae akamwambia mumewe,
“Hata mimi nina furaha sana kwani ile ndoto yetu ya kuwa na watoto wane naiona ikitimia kabisa.”
“Kwahiyo umepanga mdogo wake huyu aje baada ya muda gani?”
“Yani huyu akifikisha miaka miwili tu namletea mdogo wake”
“Lakini nasikia kwenye uzazi wa mpango huwa wanasema angalau watoto wapishane miaka mitano mitano ili kila mmoja apate yale malezi ya kutosha ya kitoto”
Sophia akacheka kidogo na kumwambia mumewe,
“Achana na hayo mambo ya wataalamu na hao wa uzazi wa mpango mume wangu, katika maisha kila mtu huwa anajipangia mambo yake mwenyewe, kwetu tumezaliwa tisa tena mama alituachanisha kidogo sana, mwingine kampita mwenzie miaka miwili, mwingine mmoja, mmoja na nusu lakini sote tumekuwa vizuri tu hatuna kasoro wala dosari yoyote kama unavyotuona.”
“Kasoro ipo Sophy”
“Kasoro gani?”
“Kwanza kabisa kwenu mmezaliwa wengi kushinda uwezo wa wazazi wenu, pili mlipishana karibu sana. Angalia mlivyo ni nani aliyebahatika kusoma kwenu hata aweze kuitwa msomi labda”
Sophia akanuna kiasi kisha akamuuliza Ibra,
“Kwahiyo kusoma ndio kasoro? Mbona nyie mpo wachache kwenu na hata hamjasoma kivile!”
“Ni kweli kwetu tupo wachache na hatujasoma hivyo ni kutokana na uwezo wa wazazi wetu ila uchache tuliokuwa nao umefanya tuweze kupambana na ugumu wa maisha. Kwakweli kwa upande wangu kaka zangu wote wamejikwamua kimaisha, kumbuka tupo watano nyumbani kwetu. Kaka zangu watatu walishajikwamua kimaisha, dada nae alijitahidi kujikwamua na sasa kaolewa huku akiendeleza gurudumu la maisha yani nilibaki mimi tu nyuma ambapo nami nimekomboka kwa sasa tena nimewapita wote kimaisha. Haya kwa upande wa kwenu yani mwenye afadhali ni wewe tu, angalia akili za dada zako zilivyo na Yule mdogo wako wa mwisho ni nini anafanya. Kaka zako je, bangi bangi na wao hapo kuna maendeleo gani ya kuwa wengi ambao hamueleweki? Kwa walivyo wazazi wenu wangewazaa wachache na uhakika wasingeshindwa kuwasomesha”
Sophia akanuna zaidi na kumuuliza tena Ibra tena kwa kupaniki,
“Tungekuwa wachache mimi ningekuwepo? Nakuuliza wewe ningekuwepo? Maana mimi kuzaliwa kwetu ni mtoto wa nane ndio akazaliwa Yule mdogo wangu, mara nyingine ujifikirie kabla ya kuongea mambo ya kijinga jinga.”
Kisha akainuka kwa hasira na kuelekea chumbani.
Ikabidi Ibra ainuke na kumfata mkewe chumbani ili aweze kumbembeleza ambapo akamkuta akilia,
“Jamani mke wangu usichukulie hasira yale yalikuwa ni maongezi tu wala sikuwa na nia mbaya”
“Hukuwa na nia mbaya wapi wakati unaisema familia yangu!”
“Nisamehe mke wangu tafadhali, nakupenda sana Sophy”
“Yani mi kusema watoto wapishane miaka miwili miwili umeona ndio ishu, kuna watu wanahangaika na wake zao huko sababu hawataki kuzaa zaa watazeeka ila mimi niliyejitolea kwako unaniona mjinga poa bwana.”
“Tafadhali mke wangu nisamehe, nakuomba nisamehe sana”
Ibra akapiga na magoti kumuonyesha mkewe kuwa anajutia kitu alichoongea, kitendo cha Ibra kupiga magoti kikampa Sophia faraja na kujikuta akitabasamu na kufanya afurahi na mume wake.
Kwavile ilikuwa ni jioni, Ibra akamuomba mkewe watoke kidogo wazunguke zunguke maeneo ya karibu kama kufanya zoezi la kutembea tu ambapo Sophy alikubali kisha akabadili nguo na kuwafanya watoke sasa.
Walipokuwa nje ya nyumba yao, Ibra aliona kuna upande ambao hajawahi kutembelea toka walipohamia kwenye nyumba ile na kumuomba mkewe waelekee upande ule kidogo, kisha wakatoka pale na kuanza kuelekea ule upande.
“Ila tusiende mbali sana nitachoka mwenzio”
“Usijali Sophy, tunatembea kwa stepu hakuna haja ya kwenda mbali sana.”
Wakiwa njiani wakaonana na Jane ambapo Sophia alisimama kwa tabasamu na kusalimiana na huyo Jane,
“Shikamooni”
“Marahaba, mbona hukuja tena nyumbani wakati uliniahidi kuwa utakuwa unakuja”
Jane akatabasamu kidogo kisha akasema,
“Kesho nitakuja dada hata usijali”
Waliongea kidogo pale na kuagana nae.
Alipoondoka, Sophia akamuuliza mumewe kama anamkumbuka Yule Jane,
“Mmh hata simkumbuki”
“Ndio Yule binti wa Yule mama jirani yetu ambaye mwanzoni kabisa nilikutana nae pale getini kwetu, na siku amekuja na binti yake hata wewe uliporudi uliwakuta”
“Aaah nishawakumbuka, si unajua tena kichwa hiki kina mambo mengi”
“Loh naona kweli mambo mengi maana hata hili ulikuwa hukumbuki kweli mambo yanakutinga”
Kisha wakaendelea na matembezi yao ya hapa na pale, kuna mahali palikuwa na kimlima kidogo ambapo Ibra akashauri warudi tu kwani alihisi kupanda kile kimlima kutamfanya mkewe achoke sana,
“Turudi nyumbani Sophy”
“Aah jamani, tusogee sogee kidogo yani mi ndio ushanitamanisha na kutembea, twende tukaishie pale kwenye kimlima”
“Ila si unaona giza nalo limeanza kuingia”
“Ndio naona ila tuishie hapo kwenye kimlima”
Ibra hakumpinga kwavile aliyekuwa akimuonea huruma ni yeye mwenyewe, kwahiyo wakaendelea mbele kidogo na kuanza kupandisha kile kilima.
Walipofika juu kidogo kulikuwa tena na mteremko kushuka chini ila kuna kitu kilimshtua Sophy kwa kule chini na kumfanya amkumbatie mumewe kwa nguvu,
“Nini tena Sophy?”
“Ona kule chini”
Ibra alipoangalia akamuona tena Yule mtoto wa mchana akiwatazama kamavile anaomba msaada, Ibra akamshika mkewe mkono na kurudi nae nyuma kisha kugeuza na kuanza kurudi nyumbani huku akiongea,
“Yani mimi nikikataa kitu ujue lazima kuna tatizo ona sasa bora hata tungerudi pale pale nilipokataa”
Sophia hakujibu chochote zaidi ya kukokotana na kurudi nyumbani.
Walifika nyumbani, ila Sophia alidai kuchoka sana na kuelekea chumbani kulala ambapo ibra nae alielekea chumabani na kulala pembeni ya Sophia kwa kumkumbatia ili aweze kuwa na amani.
Wakati usingizi umemkolea kabisa Sophia akajiwa na ndoto, akamuona tena Yule mtoto akiwa pale pale chini kidogo ya kile kilima ambapo kwenye ndoto hii Sophia alijiona akimfata Yule mtoto alipo na kumuuliza kuwa tatizo ni nini, kisha Yule mtoto akamwambia,
“Sina ubaya na wewe Sophia, una moyo wa kujali halafu una upendo sana ila tatizo ni huyu mume wako hana huruma kabisa. Je ungependa nimfanye nini?”
Sophia akawa kama anamshangaa huyu mtoto na kumuuliza,
“Umfanye nini kivipi na kwanini?”
“Mumeo ana roho mbaya sana Sophia, sipendi watu wasio na huruma wakati mimi huwa nakusaidia mambo mengi sana. Niambie basi nimfanye nini?”
“Hapana usimfanye chochote mume wangu”
“Usiwe na huruma hivyo Sophia kwa mtu asiye na huruma, yani mimi hata ukiniambia nimuue sasa hivi huyu mumeo namuua”
Sophia akashtuka kutoka kwenye ile ndoto na kupiga kelele huku jasho jingi likimtoka na kufanya Ibra nae ashtuke na kumuuliza mkewe kuwa tatizo ni nini,
“Vipi Sophy?”
Sophia alikuwa akihema juu juu na kumjibu mumewe,
“Nimeota ndoto mbaya sana”
“Mmmh pole mke wangu, hiyo ndoto inahusu nini?”
“Nimemuota tena Yule mtoto eti alitaka kukuua wewe”
Ibra akatabasamu kwavile hakuwa mtu wa hofu kwa mambo kama hayo haswa ya kuhusu ndoto, kisha akamwambia Sophia,
“Mke wangu, usiwe na wasiwasi juu yangu halafu ndoto za namna hiyo zisikutishe sana. Mimi ni mwanaume jasiri siwezi kuteketea kirahisi hivyo. Pia naomba Yule mtoto umtoe mawazoni mwako mke wangu tafadhali”
Kisha Ibra akainuka na mkewe na kwenda kukoga ili angalau kupata nguvu mpya na kuondoa uchovu uliopita hata iwasaidie kuanza upya usingizi.
Walimaliza kuoga na kurudi tena kulala.
Kulipokucha, Ibra aliamka na kujiandaa kwenda kwenye mahangaiko yake kisha akamuaga mke wake na kumwambia kuwa endapo kutatokea tatizo lolote basi asisite kumpigia simu.
“Usijali nitakujulisha mume wangu”
Kisha Ibra akambusu mkewe kwenye paji la uso na kumuaga.
Sophia hakuweza kuendelea kulala kwani muda ule ule aliamka na kwenda sebleni akiwa amejikalia tu kisha muda kidogo akafanya kazi zake za hapa na pale kisha kupumzika tena.
Akiwa pale sebleni alisikia hodi na kwenda kufungua ambapo aliyeingia alikuwa ni Jane hivyo kumfanya Sophia afurahi sana kwa kupata kampani ya muda ule.
“Bora Jane umekuja maana nilikuwa mpweke sana”
“Ndiomana nikaamua kutimiza ahadi yangu”
Sophia alimkaribisha vizuri sana Jane na kukaa pamoja sebleni huku wakizungumza mambo mbalimbali, ambapo Sophia alimuuliza Jane,
“Hivi huwa unafanya nini ukiwa nyumbani mwenyewe, ukiachana na kazi za nyumbani”
“Kwakweli dada mi napenda sana kusoma stori haswa stori za kutisha”
“Kheee wa ajabu wewe sasa stori za kutisha unazipendea nini?”
“Yani mi huwa napenda tu halafu huwa naona kama kweli vile”
“Basi mimi katika vitu ambavyo sipendi ni kusoma stori haswaa za kutisha sababu huwa naona ni uongo mtupu. Waandishi wanaandika vitu vya kidhahania yani havina ukweli wowote.”
“Mmh ila vingine vina ukweli dada, mfano mamabo ya misukule”
Sophia akacheka sana,
“Yani Jane na usomi wako wote bado unaamini kuhusu misukule! Hakuna kitu kama hicho duniani, tatizo lako hizo stori zimekukaa kichwani, ushawahi kuona msukule wewe? Zaidi ya kuona kwenye sinema na kusoma kwenye stori, hakuna kitu kama hicho”
“Lakini dada mara nyingi wanaoandika stori huwa ni mambo ambayo yapo kwenye jamii ndiomana yameandikwa”
“Aaah ni propaganda tu hizo ili wapate wasomaji wengi hakuna ukweli wowote”
“Ila kuna mambo ni mazuri na yanatufundisha kwakweli, mimi toka nianze kusoma hizi stori nimejifunza mambo mengi sana. Kwanza siwezi kulala bila kumuomba Mungu maana usiku wetu umezingirwa na mambo mengi, na pia nikiamka lazima nimshukuru Mungu na kuomba aniongoze siku hiyo ingawa mara nyingine nasahau kuomba nikiamka kwakweli”
Hapo hapo akajicheka tena na kusema,
“Aah hata leo yenyewe nimeshau kusali, kwakweli Mungu anisamehe tu”
Sophia nae akacheka na kumwambia,
“Hebu acha masikhara yako Jane, yani mi mtu haniambii kitu kuhusu mastori ya uongo yani siwezi kupoteza muda wangu nifatilie.”
Kisha wakabadili mada na kuanza kuongelea mambo mengine.
Mchana ulipofika Sophia alijisikia uchovu sana na kumuomba Jane akamsaidie kupika,
“Mdogo wangu Jane naomba msaada tafadhali”
“Sema chochote dada nitafanya”
“Jikoni kuna ndizi nilizimenya na nyama ipo kwenye friji, unaweza kwenda kupika ili tule”
“Aah usijali dada, jikoni ndio wapi?”
Sophia akamuonyesha Jane mlango wa jikoni ambapo Jane aliinuka na kuelekea jikoni.
Alipoingia alikwenda moja kwa moja na kufungua friji ambapo hakuona nyama yoyote ila alipoangalia kwenye jiko aliona sufuria imefunikwa vizuri kabisa akaamua kusogea na kufunua, kwanza akasikia harufu nzuri sana ya chakula na alipoangalia aliona ni ndizi zikiwa zimepikwa vizuri kabisa tena zikiwa na nyama na bado zilikuwa za moto. Kwakweli Jane alishangaa kiasi na kujiuliza,
“Hivi kaniambia nije nipike au nimsaidie kupakua jamani! Mbona chakula alishapika tayari! Nadhani kaniambia nije nipakue.”
Kisha akachukua bakuli kubwa na kupakua halafu akapeleka mezani na kuweka sahani halafu akamfata Sophia na kumwambia tayari.
Sophia akamuangalia kwa makini na kumuuliza,
“Tayari nini?”
“Tayari chakula kipo mezani”
“Mmh usinitanie Jane, haiwezekani zile ndizi ziwe zimeiva! Hebu acha utani”
Akaelekea na Jane mezani ila bado Sophia hakuamini na kumuangalia vizuri Jane kisha akamuuliza,
“Je wewe ni binadamu wa kawaida?”
Jane akamshangaa Sophia kwa swali lile.
_Mwisho wa sehemu ya 5._
Itaendelea……………..!!!
✍
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/39Z98NI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment