Tuesday, February 25, 2020

NYUMBA YA MAAJABU 03



Ila aliporudi chumbani ili afute alikuta yale matapishi yalishafutwa na pale palishakaushwa kabisa, kwakweli Sophia alichoka ghafla, akamuangalia Ibra pale kitandani ila Ibra alionyesha kutokuwa na habari yoyote kwani alikuwa amejilaza vile vile.
*TUENDELEE...*

Sophia hakuelewa kwakweli yani hakuelewa kabisa, akenda tena pale kitandani alipokuwa amejilaza Ibra na kumshtua, ambapo Ibra aliongea kwa kulalamika,
“Sophia jamani mbona hivyo mke wangu? Kwa nini unanifanyia hivi lakini si nimekwambia kuwa najisikia vibaya! Sasa kwanini hutaki mwenzio nipumzike jamani unanifanyia mambo ya ajabu, kwanini kunishtua shtua kila muda?”
“Samahani Ibra lakini nani kazoa matapishi yangu?”
“Matapishi?”
“Ndio, kwani hukunisikia wakati natapika?”
“Sijakusikia bhana, unanisumbua tu Sophy hebu acha nipumzike”
Ibra akageuka tena na kulala, kwakweli Sophia hakuelewa chochote alijikuta akijishika tama tu kwa mawazo kwani aliona kama vile Ibra anamchanganyia mada huku na yeye akizidi kujiuliza kuwa kama sio Ibra anayefanya hayo je yatakuwa yanafanywa na nani?
Hapo ndio ilikuwa ngumu kabisa kwa yeye kuelewa.
Akajikuta akikaa pale kitandani huku akitafakari kwa muda mrefu sana bila ya kupata majibu hadi akapata wazo la kumpigia simu tena Siwema ili amuulize ila aliona kama vile ni kumsumbua tu huyo Siwema, kwahiyo akatulia kimya kwa muda mrefu kidogo kisha akainuka pale na kuelekea jikoni kwa lengo la kuandaa vizuri mlo wa usiku.
Akiwa jikoni alijiuliza sana kitu kilichopelekea yeye kutapika ni nini,
“Hivi ni kwanini nimetapika ikiwa siumwi wala nini? Ni kitu gani kimepelekea mimi kutapika?”
Alijiuliza bila ya kupata jibu la aina yoyote ile kwahiyo akaamua kuandaa chakula tu.
Alipomaliza kuandaa chakula alitoka jikoni na kuelekea sebleni ambapo alimkuta mumewe amekaa na kwakweli alionekana kuwa sawa kabisa kwasasa tofauti na mwanzo,
“Khee Ibra kumbe umeamka tayari!”
“Ndio nimeshaamka”
“Eeh unajisikiaje na hali!”
“Nipo salama kabisa mke wangu”
“Basi ngoja nikakuandalie maji ya kukoga”
“Hata usijali mke wangu nimeshakoga labda ulete chakula tule”
Basi Sophia hakutaka kuhoji zaidi kwahiyo akenda kuleta chakula kisha yeye na mumewe wakaanza kula chakula hicho huku wakizungumza mambo mawili matatu,
“Kwahiyo Ibra sasa hivi unajiona umepona kabisa!”
“Ndio nimepona kwani nilikuwa naumwa sana eehh!”
“Yani hadi mimi ulinitia mashaka mume wangu mpaka hofu ilinitawala kabisa”
“Hata usiwe na mashaka mke wangu maana mimi ni mzima kabisa kabisa”
“Basi vizuri mume wangu kama ndio hivyo”
“Ila nakushukuru sana Sophy kwa mapenzi yako unayonionyesha na jinsi unavyonijali”
Sophia akatabasamu huku wakiendelea kula kile chakula, walipomaliza kama kawaida Sophia alitoa vyombo na kutaka kwenda kuvikosha ila Ibra alimuita na kumfanya Sophia asikoshe vyombo vile.
“Sophy mke wangu napenda nikae na wewe tupumzike pamoja”
“Naelewa mume wangu ila huwa sipendi kulala na vyombo vichafu ndani ndiomana huwa napenda kuvikosha pindi tunapomaliza kula”
“Ngoja nikuulize swali, kwani kesho unaenda wapi?”
“Nipo tu siendi popote”
“Sasa tatizo liko wapi hapo? Utaosha hata kesho, mi napenda tukae tuzungumze na tupumzike pamoja”
Ikabidi Sophia atumie nafasi hii kumuuliza Ibra kuhusu matapishi yake,
“Hivi Ibra hukunisikia wakati natapika?”
“Kwani unaumwa?”
“Hapana ila nilitapika”
“Mmmh sijakusikia kwakweli”
“Mmmh kwahiyo nani alizoa matapishi yangu?”
“Mmmmmh Sophy acha habari hizo bhana tumetoka kula, hebu tubadilishe mada”
Sophia hakuwa na jinsi zaidi tu ya kufata matakwa ya Ibra na kisha wakaamua kwenda kulala, Ibra alipopitiwa na usingizi Sophia akakumbuka vile vyombo akaona ni vyema akavioshe ili asipate tena maswali ya kujiuliza kuwa vyombo vimeoshwa na nani, kwahiyo akatoka mle chumbani na kwenda jikoni kwa lengo la kukosha vyombo.
Alivikuta vyombo vipo pale pale jikoni na kisha akaanza kuvikosha, muda kidogo alikuja Ibra kutoka chumbani huku akitikisa kichwa baada ya kumkuta Sophia akiosha vyombo,
“Ona sasa mke wangu halafu unakazana kuuliza nani kaosha vyombo wakati unaamkaga mwenyewe usiku wa manane kuvikosha jamani unakuwa kama mwanga, majukumu gani hayo ya usiku wa manane?”
“Unajua nini Ibra sikupenda nipate tena shida ya kudadisi juu ya mtu aliyeosha vyombo ndiomana nimeamua kuvikosha mwenyewe”
“Kwakweli umenishangaza Sophy yani nashtuka kitandani sikuoni kumbe upo jikoni unakosha vyombo, jamani mke wangu kwanini unakuwa hivyo jamani? Nadhani mtu yeyote atakayesikia hili lazima ashangae, kwani kuna umuhimu gani wa kukosha vyombo usiku kama vile hapatakucha?”
Ibra alionekana kutokupendezwa kabisa na hii tabia aliyoiona leo kwa Sophy kwani yeye alipenda anapogeuka kitandani basi amkute mkewe akiwa pembeni,
“Basi nisamehe mume wangu, nakuahidi hii hali haitajirudia tena kama nikishindwa kukosha muda ambao tumemaliza kula basi nitakuwa nasubiria hadi kesho yake. Nisamehe tafadhali”
Basi akavimalizia na kuviacha pale juu huku akipanga kuviweka kabatini kesho yake kwani hakutaka kumkwaza mume wake zaidi.
Wakaongozana pamoja kuelekea chumbani ambapo Ibra alionekana kutokuwa na usingizi sana kwani yote ilitokana na vile alivyolala jioni ya siku hiyo, kwahiyo walivyofika tu kitandani Ibra akaanzisha maongezi tena.
“Hivi ulisema kuwa leo umetapika eeh”
“Ndio nimetapika”
“Basi kama hiyo hali itaendelea itabidi twende hospitali”
“Kama ikijirudia tutakwenda mume wangu, asante kwa kunijali”
“Unajua Sophy mi nakupenda sana na kwakweli sipendi kuona ukisumbuka wala kuhangaika mke wangu ndiomana unaniona mara nyingine nafoka”
Kisha akamsogelea karibu na kumkumbatia ili waweze kulala, na kweli usingizi ukawapitia hadi palipokucha ambapo kama kawaida Ibra aliamka na kujiandaa kisha kumuaga mkewe na kwenda zake kazini.
Sophia nae kama kawaida yake alipoamka alienda moja kwa moja jikoni ambapo alikuta vile vyombo alivyoviosha usiku vikiwa tayari vimepangwa kabatini,
“Yani huyu Ibra ananikataza mimi ili afanye yeye ila ni sawa tu maana yupo kwenye harakati za kunionyesha upendo”
Alipofikilia hayo akaenda kuandaa chai na kunywa halafu akaenda kuloweka nguo ili afue, baada ya kuziloweka alirudi sebleni ili akae angalau kidogo halafu ndio akafue ila alivyokaa pale sebleni akapatwa na usingizi wa ghafla uliomfanya alale hadi kujisahau kuwa alipanga kwenda kufua nguo zake.
Ibra alirudi nyumbani na kugonga sana ila kwa bahati nzuri tu alikumbuka kuwa anafunguo za ziada kwenye gari lake kisha akaenda kuchukua funguo zile na kufungua milango ambapo alimkuta Sophia akiwa amelala tena hajitambui kabisa, ikabidi Ibra ndio amshtue Sophia kutoka kwenye ule usingizi aliokuwa amelala ambapo Sophia alionekana kushtuka sana.
“Kheee Sophia ndio kulala gani huko hadi umejisahau yani nimegonga na kugonga ila wapi”
Ila Sophia alionekana kuchoka sana hata akajikuta anashindwa kumjibu mumewe kwa wakati, hadi alipotulia kidogo kama kurudisha akili yake vile ndio akaweza kumjibu mume wake,
“Yani hata sijielewi ila nimechoka balaa”
“Mmh hata kupika umepika kweli wewe?”
“Kwakweli sijapika wala sijafanya chochote kile yani hata sijielewi”
“Pole sana mke wangu basi twende tukajimwagie upate nguvu kisha twende tukale hotelini maana hamna namna tena”
Sophia akakubali na kuzidi kuuona upendo wa Ibra juu yake kuwa Ibra anampenda na kumuhurumia sana kwani ile iliweza kuonyesha ni kwa kiasi gani alipendwa na Ibra.
Walipomaliza kujiandaa wakatoka na kuelekea hotelini kama ambavyo Ibra alisema ili kuweza kula, waliagiza chakula na kuanza kula ila ghafla Sophia akapatwa na kichefuchefu na kujikuta akikimbilia nje kutapika, Ibra alivyoona vile akamuomba muhudumu awafungie kile chakula kisha akenda kumuangalia mke wake,
“Kwani unajisikiaje Sophy”
“Najisikia vizuri tu”
“Vizuri wakati umetapika jamani! Itabidi kesho twende hospitali tukaangalie afya yako”
Sophia akakubali kisha akaja Yule muhudumu na kuwapa chakula chao ambapo Ibra alilipia na kuondoka na mke wake.
Walipofika nyumbani waliweka kile chakula na kuanza kula tena ila Sophia alionekana kula kwa kujivuta vuta sana,
“Lazima unaumwa Sophy ingawa wewe mwenyewe unajiona kuwa mzima”
“Ni kweli kabisa najiona kuwa mzima mimi”
“Hata kama unajiona ni mzima lazima kesho twende hospitali maana hii hali ni mbaya mke wangu”
“Sawa nimekuelewa kwa hilo”
Walipomaliza kula, Ibra alibeba vile vyombo na kuvipeleka jikoni kisha akamtaka mke wake kuwa waende kulala,
“Ila sina usingizi Ibra”
“Hata kama, ila mi nakuomba twende tu chumbani”
Kisha wakaelekea chumbani na moja kwa moja wakaenda kitandani ambapo ibra alikuwa akimuangalia sana mke wake kwani aliona wazi kuwa lazima atakuwa anaumwa tu ila anajikaza.
Kulipokucha, asubuhi na mapema Ibra akamuamsha mke wake ili aweze kujiandaa na waweze kwenda hospitali ambapo Sophia alifanya hivyo ila alipomaliza kujiandaa akamwambia mume wake,
“Lakini unajua Ibra mi siumwi kabisa na wala hata sijisikii vibaya”
“Unaweza ukajiona kuwa huumwi kumbe ugonjwa upo ndani kwa ndani, usifikiri ni kitu rahisi kutapika vile Sophia usiwe mbishi kwani mi nakuona kabisa kuwa unaumwa”
“Na hospitali tutakwenda kujielezaje sasa?”
“Tutajieleza kama hali halisi ilivyo”
“Ila bado mimi sidhani kama naumwa kwani nahisi ni uchovu wa jana tu”
“Uchovu wa jana umefanya kazi gani?”
Sophia akafikiria kidogo na kukumbuka kuwa aliloweka nguo,
“Mmmh jana nililoweka nguo ila sikuzifua mmh si zitanuka jamani maana nilisahau kabisa”
“Basi usijali tutafua pamoja tukirudi”
Sophia akatabasamu kisha akatoka na mume wake kwa lengo la kwenda huko hospitali, ila alipofika mlangoni akakumbuka kitu kwenye zile nguo alizokuwa ameloweka jana yake ikabidi amwambie mumewe amsubiri akachukue.
Alipofika uwani ambako aliloweka zile nguo alikuta zote zikiwa kwenye kamba tena zilionekana kukauka kabisa, kwakweli Sophia akashangaa sana na kumwita Ibra kwa nguvu ili kumuonyesha kile anachokiona.
Ibra nae alifika kwa haraka sana kama alivyoitwa na Sophia, kisha Sophia akamuonyesha nguo kwenye kamba ambapo Ibra aliuliza kwa mshangao
“Kwani vipi Sophy?”
“Nguo kafua nani?”
“Nguo kafua nani kivipi?”
“Kwani wewe huoni nguo kwenye kamba?”
“Naziona ndio kwani tatizo nini?”
“Nani kazifua sasa wakati mimi niliziloweka tu!”
Ibra alikuwa akimshangaa tu mkewe ambapo kabla hata hajasema chochote, Sophia alianguka chini na kuzimia.

Mwisho wa sehemu ya 3

ITAENDELEA...............!!!






from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2T2LzhD

No comments:

Post a Comment