Thursday, February 27, 2020

NYUMBA YA MAAJABU




                 

Sophia alitoka hadi sebleni ambapo kila aliposogea ile sauti ya Tv nayo ndio ilisikika zaidi, alipofika karibu na kuchungulia alikuta ni kweli Tv iliwaka na ilikuwa ikionyesha vizuri kabisa.
*TUENDELEE...*

Kwa kweli Sophia alipatwa na woga sana safari hii, hali hiyo ilipekea aanze kupiga makelele na kufanya mumewe atoke chumbani mbio hadi pale sebleni.
Moja kwa moja Ibra alimuuliza mkewe kuwa amekubwa na kitu gani,
“Nini tatizo mke wangu?”
“Ona Tv inawaka”
Ibra aliiangalia ile Tv ambayo ilikuwa ikionyesha vizuri kabisa kisha akamuangalia mkewe na kusema,
“Si nilichomoa nyaya zote kwenye hii Tv mimi!”
“Ndio ushangae sasa inawaka”
Ibra akaisogelea ile Tv na kuangalia vizuri akakuta nyaya zote zimechomekwa vizuri kabisa, kisha akamuangalia tena mke wake na kumuuliza,
“Nani kachomeka tena hizi nyaya za Tv?”
“Hakuna aliyechomeka itakuwa zimejichomeka zenyewe”
Ibra akacheka kama kwa dharau hivi kisha akamwambia mkewe,
“Nyaya zinajichomekaje zenyewe Sophy mke wangu? Unajua wewe huwa unabaki hapa nyumbani hebu kumbuka nani kachomeka nyaya? Au Siwema jana alichomeka hizo nyaya?”
“Ibra hakuna aliyechomeka, mimi nina uhakika na ninachoongea. Kwakweli nimeanza kuamini maneno ya Yule bibi kuwa hii nyumba ni ya maajabu na siwezi tena kubaki humu ndani peke yangu”
“Kwamaana hiyo unataka mimi nifanyaje? Je tuwe tunaenda wote kazini au nikuletee msichana wa kazi?”
Sophia akawa kimya kwa muda bila ya kujibu lile swali la Ibra, kisha Ibra akaisogelea ile Tv na kuizima halafu akachomoa tena nyaya zote za T vile, halafu akaanza kuongea na mkewe tena
“Unajua zamani watu walipokuwa wakiniambia kuwa mamama wajawazito wana vituko sana nilikuwa siwaamini kabisa ila sasa najionea mwenyewe kwa macho yangu. Kwakweli vituko vyako Sophy vimezidi sasa”
“Jamani vituko gani ambavyo mimi navifanya Ibra?”
“Hebu kumbuka toka umeshika hiyo mimba ni vituko mwanzo mwisho, mara useme vyombo vimeoshwa kimiujiza sijui chakula kimepikwa kimaajabu mara nguo zimejifua zenyewe. Sasa ya saivi ndio kali hii ya kujiwasha kwa Tv duh! Tutafika kweli kwa mtindo huu mke wangu? Sophy hukuwa mtu wa kwenda kwa waganga ila kupindi hiki umekwenda hadi kwa mganga na kuniletea makubwa zaidi, kihela chetu kimekwenda na maji. Ulitaka umuue Jane, hivi unaweza kuua wewe? Hiyo roho umeitoa wapi mke wangu? Wewe sio Sophy niliyekuzoea jamani!”
“Ibra najua unanishangaa kwavile mambo mengi ni mimi ninayeyaona ila ungeona na wewe ungeelewa kwanini nakuwa hivi”
“Kwahiyo unataka turudi yale maisha ya zamani? Unataka yale maisha ya wewe kutembeza karanga na kurudi na mia tano ndani? Unayataka maisha yale ya kukosa hata hela ya kula ndani? Mumeo nimepambana na kufanya maisha yetu yabadilike ili angalau mke wangu uweze kuishi yale maisha ambayo wanawake wengine wanaishi ila matokeo yake ndio haya kukosa amani ndani! Nilikuwa najiuliza sana kwanini wanaume wengine huwarudisha wake zao nyumbani hadi watakapo jifungua ila sasa nimepata jibu kabisa, kwakweli wewe Sophia ni miongoni mwa wanawake wanaotakiwa kurudi nyumbani kwao hadi uatakapojifungua”
Sophia hakuongea chochote kwani kauli ya mumewe kuwa anastahili kurudi kwao hadi atakapojifungua ilimkera sana ukizingatia maisha ya kwao aliyajua mwanzo mwisho.

Ibra alirudi tena chumbani ambapo moja kwa moja akaenda kukoga huku akili yake ikimueleza kuwa lazima Sophia alikwenda sebleni na kuchomeka nyaya za Tv kisha akaiwasha na kujifanya kuwa imejiwasha ili kumfanya yeye awe anaamini maneno yake kuwa kuna maajabu katika nyumba hiyo.
Ibra alikuwa akioga huku akiwaza cha kufanya kwa huyu mkewe kwani alimuona kama anaanza kuchanganyikiwa na akili, alimaliza kukoga na kurudi chumbani alianza kuvaa huku akiongea peke yake,
“Kwakweli kama mimba zenyewe ndio hivi sijui kama nitaweza jamani, ndio kwanza mimba ya mtoto wa kwanza je akifika mpaka huyo wanne anayehitaji yeye dah sijui kama sitabaki kijiti mimi kwa mawazo jamani mmh! Mwanamke ananieleleza huyu sijapata kufikiria.”
Wakati akiwaza hayo, salimsikia Sophia akimuita tena kwa sauti ya juu kabisa na kumfanya atoke na kuelekea Sophia alipo ambapo alimkuta jikoni,
“Eeh kuna nini kipya huku jikoni?”
“Vyombo vya jana vimeoshwa vyote”
Safari hii Ibra hakushtuka wala nini bali alicheka tu na kumwambia mkewe,
“Kama vimeoshwa si ndio vizuri umepunguziwa kazi au unaonaje mke wangu!”
“Ibra unachukulia masikhara wewe, sasa hutaki hata kujiuliza kuwa vimeoshwa na nani ikiwa ndani tuko wawili tu mimi na wewe!”
“Ingekuwa tunakuta vyombo visafi vimechafuliwa hapo sasa ndio ningechukua hatua ila kukuta vyombo vichafu vimeoshwa sasa nichukue hatua gani wakati kazi zetu zinajifanya zenyewe tu. Hakuna hata sababu ya kushtuka kwa hilo mke wangu kuwa kawaida tu”
Sophia alimuangalia mumewe kwa hasira kiasi na kuhisi kuwa mumewe kuna vitu anafahamu kuhusu yanayotokea ila amemficha tu maana muda wote yeye ndio anaonekana kuridhishwa kabisa na kinachotokea.
Kisha akamuuliza anapoelekea maana alimuona akiwa amemaliza kujiandaa kabisa,
“Kwahiyo ndio unataka kwenda wapi?”
“Nataka kwenda kumleta fundi wa Tv”
“Kipindi kile ulisema hivyo hivyo ila mpaka leo kimya haonekani fundi wala nini”
“Fundi ningemletaje na yale majanga yako? Tatizo lako kila leo unazua jipya yani hatupumui humu ndani.”
“Kwahiyo mimi unaniacha na nani?”
“Nilikuuliza nikuletee msichana wa kazi au uende kwenu ukapumzike? Hakuna ulilonijibu sasa unafikiri mimi nasemaje tena!”
“Ila mimi si nilishakwambia sitaki msichana wa kazi nataka aje mdogo wangu”
“Sophy, mdogo wako Yule Tausi unamjua vizuri kabisa kwakweli siwezi kumleta hapa maana mambo yatakuwa ni yale yale tu. Lini Tausi ametulia nyumbani? Hebu usitake kuleta makubwa zaidi. Cha muhimu hapa ni mdada wa kazi tu.”
“Sawa siwezi kukupinga si umeamua bhana, sasa tutampatia wapi huyo mdada wa kazi?”
“Tutampata tu hata usijali, ngoja nianze kuulizia kwa wadau mbali mbali.”
“Ila kwa leo mimi sibaki hapa peke yangu”
“Kwahiyo unataka nikusubiri twende wote kwa fundi?”
“Ndio nisubiri”
“Mmh kweli kazi ninayo, haya kajiandae nakusubiri”
Ilibidi Ibra akae sebleni akimngoja mkewe amalize kujiandaa wende huko kwa fundi.

Sophia alipomaliza kujiandaa alitoka, kisha yeye na mumewe wakatoka nje ambapo Ibra aliona ni vyema wakamfate fundi kwa miguu tu kwani hapakuwa na umbali wowote,
“Ni vyema maana itakuwa pia ni zoezi tosha kwangu”
Wakaanza kutembea kwa mwendo wa kawaida tu ila mbele kidogo walimuona binti kajiinamia tena alionyesha wazi kuwa alikuwa akilia, kwakweli Sophia huruma ilimjaa kwa binti Yule na kumuomba mumewe kuwa wamsogelee na wamuulize kuwa alikuwa na tatizo gani ila kama kawaida ya Ibra na roho yake ngumu alikuwa akipinga,
“Sophy, kila mtu ana matatizo yake hapa duniani utayaulizia ya wangapi jamani?”
“Ibra jamani mbona huwa huna huruma! Unakuwa na roho mbaya hivyo kwanini?”
“Roho mbaya kushinda wewe uliyekuwa unataka kumuua Jane!”
“Jamani hayo mambo si yaliisha! Hebu tukamuulize Yule binti inaonekana ana matatizo”
Ibra aliamua kukubaliana na mkewe kisha wakamsogelea Yule binti ambaye ni kweli alikuwa akilia, Sophia akainama na kumuuliza kuwa ana matatizo gani
“Nina matatizo mengi sana dada yani hapa nilipo hata kula sijala njaa nayo inaniuma sana”
Sophia akaingiwa na imani na kumuomba mumewe kuwa warudi na binti huyo nyumbani kwao ili waweze kumpatia chakula na awaeleze yale yaliyomsibu ili kama wataweza kumsaidia zaidi basi wamsaidie. Ibra hakupinga swala hilo kisha wakamsaidia Yule binti kuinuka na kuanza kuelekea nae nyumbani kwao.
Walifika na kuingia nae ndani ambapo Sophia alienda kupasha kile chakula cha usiku na kumpatia ili ale, kisha na wao wakapakua cha kwao na kuanza kula kwani walikuwa wakienda kwa fundi wakati hata kula walikuwa hawajala.
Walikuwa kwa pamoja pale na kumaliza kisha wakatulia kabisa kusikiliza kuwa huyu binti alikuwa na matatizo gani, Sophia alianza kwa kumuuliza,
“Kwanza kabisa unaitwa nani na ni kitu gani kilichokupata mpaka ukawa umekaa pale unalia?”
“Mimi kwa majina naitwa Neema, kwakweli nina matatizo sana yani tangu alipokufa mama yangu nimekosa kabisa furaha ya maisha kwani nilikuwa nikiishi na bibi tu ila ndugu wote walikuwa hawanitaki nyumbani”
Akainama tena na kuanza kulia ambapo Sophia alimsogelea na kumbembeleza,
“Pole sana Neema jamani dah pole sana, eeh ikawaje?”
“Tatizo la sasa ni kuwa Yule mtetezi wangu yani bibi yangu nae amekufa na kuniacha na ukiwa halafu ndugu wakanifukuza. Nimejikuta nikitangatanga tu kisha nilipanda gari la mizigo lililoniacha mjini ila nimejikuta sina pa kuelekea na hata sijui cha kufanya”
“Khee jamani binadamu wabaya sana, pole sana. Ngoja na sisi tuangalie namna ya kukusaidia Neema”
“Nitashukuru sana jamani maana sina uelekeo mimi”
Ibra akaona ni vyema amuache Sophia na huyo Neema ili yeye ende huko kwa fundi, kwahiyo akawaaga pale na kutoka nje ambapo kabla hajaondoka Sophia alimfata nje na kumuuliza kuhusiana na wao kumsaidia binti huyo.
“Unaonaje tukiishi na huyu binti mume wangu?”
“Sophy, tutazungumza nikirudi ngoja saivi nishughulikie hili swala la fundi”
“Sawa basi badae”
Ibra akaondoka na kumfanya Sophia arudi ndani.

Sophia alienda kukaa karibu na Yule binti ili hata kujaribu kuongea nae kama ataweza kuishi hapo nyumbani kwao,
“Je tukikwambia ukae hapa na sisi unaonaje?”
“Nitafurahi sana dada, unaonekana una roho nzuri sana dada yangu”
“Usijali, jisikie huru kabisa yani jisikie upo nyumbani. Ila kazi za nyumbani unaweza kufanya?”
“Hakuna kazi ambayo mimi inanishinda, maisha niliyokulia yamefanya niwe naweza kazi zote dada yangu kwahiyo hata usiwe na hofu kuhusu mimi.”
Sophia alijikuta akiwa na huruma sana kwa huyu binti na pia akivutiwa nae sana na kuona lile swala lake na mumewe la kuhitaji mdada wa kazi limepata ufumbuzi kwa stahili hiyo.
Muda kidogo Ibra alirudi akiwa na kijana ambaye alimtambulisha kuwa ni fundi, Yule kijana moja kwa moja alienda kuiangalia ile Tv kisha akaanza kuwaorodheshea matatizo ya ile Tv na kuhitaji wampatie pesa ili aende akanunue vifaa kwaajili ya kurekebisha Tv hiyo.
“Inahitajika kama laki moja na nusu hapa ili tatizo lisijirudie tena, yani msingekuwa makini siku moja ingewalipukia hii”
“Ila mbona gharama sana mtu wangu?”
“Ndio hivyo, ni kutokana na kifaa ambacho kimeharibika huwa kinauzwa gharama sana tena hapo nimekupunguzia sababu wewe wangu bhana, yani hela ya ufundi hapo nitachukua elfu kumi tu maana laki na arobaini yote nitaenda kununulia hicho kifaa”
Ibra akafikiria kidogo, ila kwavile hapendi malalamiko ya kila siku kuhusu ile Tv aliamua kujitoa muhanga kwa kutoa hiyo pesa ili amkabidhi huyo fundi kwaajili ya kununua hicho kifaa. Ila kabla fundi hajapokea ile pesa, huyu Neema akamwambia Ibra,
“Kaka hata usitoe hiyo pesa maana hii Tv sio mbovu”
“Kwani wewe hii Tv unaijua?”
“Siifahamu ila moyo wangu unaniambia kuwa hii Tv sio mbovu”
Kisha akamuangalia Yule fundi na kumwambia,
“Kwanini unakuwa muongo hivyo? Au ukubwa wa hii nyumba ndio unafanya na wewe utake kuponea hapa! Hebu waambie ukweli kuwa hii Tv sio mbovu na wala hakuna kifaa chochote kilichoharibika, sema ukweli”
Huyu fundi alionekana akitetemeka na kujieleza kuwa ni kweli ile Tv haikuwa mbovu ila yeye alishikwa na tamaa ya pesa tu na ndiomana akasema vile, Ibra alimshangaa sana huyu fundi kwani alikuwa ni kati ya watu aliowaamini sana, kisha huyu fundi aliondoka bila kuaga.
Ibra alimuangalia Neema na kumshukuru kisha akamuuliza kuwa amejuaje kuwa ile Tv sio mbovu na amejuaje kuwa Yule fundi ni muongo,
“Bibi yangu alinifundisha kuwa mtu muongo akiongea macho yake huwa anapepesa pepesa, sasa nilipomuangalia huyo fundi nikamuona akipepesa macho na moja kwa moja nikagundua kuwa ni muongo.”
Sophia aliyekuwa amekaa kimya kwa kipindi chote nae aliamua kuchangia mada kwa kumshukuru sana Neema maana ilikuwa kama amewasaidia katika kupoteza pesa nyengine, ila bado alimwambia kuwa ile Tv ina tatizo la kujiwasha na kujizima ndiomana wakaita fundi awasaidie.
“Msijali, ilimradi mimi nipo hapa hilo tatizo halitajitokeza tena”
Sophia hakuongeza neno zaidi ya kwenda kumuonyesha Neema chumba ambacho atakuwa analala kwa kipindi chote atakachokuwa anaishi hapo.
Alimpeleka kwenye chumba ambacho kilikuwa na kitanda na godoro tu kisha Sophia akatoka na kumuacha huyo Neema kwenye chumba hicho, Sophia alienda chumbani kwake na kumchukulia Neema mashuka ili aweze kutandika vizuri pale kitandani na kufanya papendeze kulala.
Sophia akiwa na mashuka yake mkononi kwa lengo la kumpelekea Neema, aliingia kwenye kile chumba na kumkuta Neema akiwa amesimama tu ila kitanda kilikuwa kimetandikwa vizuri kabisa tena kwa mashuka mazuri.

Itaendelea…….....……!!!
.





from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/3c9lViJ

No comments:

Post a Comment