Thursday, February 27, 2020

NYUMBA YA MAAJABU



                   

 Walipofika nyumbani kwa Ibra, walishuka wote kwani Ibra alisimamisha gari yake nje kisha wakasogelea geti na kufungua kwa tahadhari, cha kushangaza sasa pale ambapo walimuacha nyoka jana walimkuta Jane amekaa tena akiwa hana habari yoyote.
*TUENDELEE...*

Kila mmoja alikuwa na mshangao juu ya lile, ambapo Ibra alimuita Jane kwa woga flani kuona kama ni mtu au ni lile joka limejigeuza kuwa ni mtu, Jane nae alipoitwa aliitika na kuinuka pale kisha akaanza kuwasogelea ambapo Sophia akamwambia Jane kwa ukali
“Tafadhali Jane usitusogelee ila tuambie umeingiaje humu ndani?”
“Kuingiaje kivipi? Mi nimekuja nikakuta geti liko wazi nikaingia”
“Nyoka yuko wapi?”
“Nyoka? Nyoka gani?”
“Unatuuliza sisi tena wakati palikuwa na nyoka hapo mlangoni”
“Sijaona nyoka kwakweli na nipo hapa kama saa moja iliyopita”
“Na ni nani aliyekwambia uje leo?”
“Sijaambiwa na mtu yeyote ila kuna vitu niliviota usiku ndiomana leo nikaja ili nikuulize”
Yule mganga nae aliwatazama Ibra na Sophia na kuwauliza kuwa Yule binti ni nani ambapo Sophia alimjibu kwa makini kabisa na kwa kujiamini,
“Huyo ndio Jane Yule mchawi maarufu”
Yule mganga akamtazama kwa makini Jane kisha akatikisa kichwa halafu akawageukia wakina Sophia na kuwaambia kuwa wamwambie Yule Jane aondoke kwani atawaharibia kazi ila Ibra akahamaki na kuuliza,
“Kazi gani sasa mganga wakati huyo nyoka hayupo tena”
“Nyoka hayupo tena? Unaweza kuangalia wewe kuwepo au kutokuwepo kwa nyoka?”
“Kama yupo yuko wapi sasa?”
Sophia akamuangalia mumewe kwa jazba na kumkazia macho kisha akamwambia,
“Ibra tafadhali acha kubishana na mtaalamu”
Kisha Sophia akamtazama Jane na kumwambia,
“Jane tunakuomba uondoke tafadhali”
Jane hakutaka kubishana nao na wala hakuongea lolote zaidi ya kutoka kwenye nyumba ile na kuondoka.

Sasa alibaki mganga na akina Sophia ambapo Siwema nae akatia chumvi kuhusu Jane,
“Mmh halafu kale katoto kanaonekana ni kachawi haswaa yani haiwezekani kawe kanajiamini kiasi kile jamani”
“Umeona dada eeeh kale katoto sio ka kawaida kabisa”
Mganga akaanza kuongea kuwa inaonekana nyoka kuna mahali kajificha kwahiyo alitakiwa afanye jitihada za kumuita kwanza nyoka huyo ili amteketeze ila katika kumuita huyo nyoka alihitaji wachinje kuku wa kienyeji watatu ili apate nguvu ya kufanya hivyo.
Kwakweli Ibra alijiona akizidi kupoteza pesa kwa uzembe wa mke wake ila hakuwa na namna yoyote ya kufanya kwa muda huo. Ikabidi atoe pesa za hao kuku kisha Yule msaidizi wa mganga akaenda kuwanunua kuku hao.
Na baada ya muda kidogo Yule msaidizi alirudi na hao kuku watatu, kisha Yule mganga akawachinja wale kuku na kuanza kama kuita ila aliita na ukapita muda mrefu sana bila ya hilo joka kujitokeza wala nini tena haikuonyesha kama kulikuwa na dalili yoyote ya kuwepo nyoka katika eneo lile, ndipo Yule mganga alipowauliza tena jina la binti aliyetoka pale.
“Yule binti niliyesema aondoke anaitwa nani?”
“Yule anaitwa Jane”
“Jamani ngoja niwaambie ninachokiona”
Wote wakatulia kumsikilizia Yule mganga anachotaka kusema, kisha Yule mganga akaanza kuwaambia
“Nimekazana hapa kumuita Yule joka lakini hajatokea, mizimu yangu imenionyesha kitu ambacho kilikuwa kimeendelea mahali hapa. Swala ni kwamba Yule binti anaelewa kila kitu tulichokuja kukifanya hapa halafu yeye hataki tukifanye. Sasa jambo alilolifanya Yule binti ni kuondoka na lile joka kwa madai kwamba atakwenda kulitumia kwenye shughuli zake. Ila nyie hata msihangaike nae, mimi nampa siku tatu tu za kuendelea kunusa harufu ya dunia hii. Kazi ya kummaliza sasa nitaifanya mimi mwenyewe baada ya kunisumbua hivi, nyie ngojeni baada ya siku tatu tu mtaitwa kwenye msiba wa huyo binti. Ngoja sisi tuondoke.”
Ibra akataka kuwapeleka ila waliomba kukodiwa usafiri wa kukodi ambapo ilimbidi Ibra afanye hivyo kisha Yule mganga na msaidizi wake wakaondoka.
Ibra akiwa pamoja na Sophia na Siwema wakafungua mlango wa ndani sasa na kuingia ndani ambapo walikaa sebleni huku wakimlaani Jane mwanzo mwisho, kwakweli Sophia alionekana wazi wazi akimchukia huyo Jane,
“Kwakweli naichukia ile siku ya kwanza kumfahamu yule mama Jane maana ndio kaniletea yote haya”
“Tena inaonyesha huyo mama ni mchawi kushinda mwanae maana haiwezekani mtoto awe mchawi halafu mama asiwe”
“Najuta kuwafahamu dada maana wamenieleleza balaa”
Ibra nae akachangia ya kwake sasa,
“Mimi najuta kumfahamu huyo mganga wenu maana bila yeye hizi pesa zote zilizonitoka leo zisingenitoka”
Ikabidi Siwema atetee kuhusu hiyo mada,
“Usiseme hivyo shemeji, uhai ni bora kuliko mali”
Wakaongea ongea kisha Ibra akamuitia na huyo Siwema usafiri wa kukodi ambapo nae aliondoka kwa stahili hiyo.

Ndani walibaki wawili sasa huku Ibra akiwa na swala lake lile lile la kulaumu kuhusu mganga,
“Yani inamaanisha mganga ndio amekukera kiasi hicho mume wangu!”
“Amenikera sana, kiukweli Sophia zamani ulikuwa ni mwanamke mwenye akili sana na ulikuwa na uchungu na pesa zetu. Nakumbuka hukutaka kabisa tufanye mambo ya kijinga kwani muda wote ulikuwa ukiwaza maendeleo, sasa siku hizi umekumbwa na nini mke wangu? Hebu fikiria isingekuwa wewe kwenda kwa mganga kwa mara ya kwanza na kupewa ile dawa ya kumuangamiza Jane je yote haya yangetokea? Na je huyu mganga alikuwa na ulazima gani wa kuchinja Yule ng’ombe, mbuzi na kondoo nyumbani kwake halafu huku akaja na damu tu! Kwanini asingekuja kwanza eneo la tukio na kuona hali halisi ilivyo kisha ndio awachinje? Kwakweli mmeniingiza hasara sana tena sana hadi sina hamu na huyo mganga tena”
“Nisamehe mume wangu ila mimi nilifanya yote haya kwa lengo la kuikomboa familia yetu.”
“Hapa hata ulikuwa hukomboi ila ulikuwa unatudidimiza tuwe maskini tena. Yani siamini kabisa kama leo nimepoteza milioni moja na nusu kwa ujinga tu dah!”
“Pole mume wangu”
“Ngoja tusaidiane kupika tule tupumzike”
Kisha wakaenda jikoni na kuanza kuandaa chakula ambapo Ibra alipofungua friji aliona kuna nyama na kuchukua nyama hiyo na kuanza kuikatakata kisha kuibandika wakati huo Sophia alikuwa akishughulika na mchele ili waweze kupika kwa haraka.
Haikuchukua muda mrefu sana wakawa tayari wamemaliza kuandaa chakula na kwenda kukaa mezani kisha wakakaa na kuanza kula huku wakikisifia kile chakula kuwa kitamu sana kwani kilikuwa na ladha nzuri mdomoni na kilivutia kula tu.
“Yani siku hizi humu ndani tunapika chakula kuwashinda hata wa hotelini maana chakula chetu ni kitamu balaa”
“Basi tusiwe tunakula hotelini siku hizi maana mapishi yetu ni hoteli tosha”
“Kwani huu wali umeweka viungo mke wangu?”
“Wala, ni maji, mafuta na chumvi tu”
“Mmh unavyonukia na kunoga balaa”
“Kwakweli hata mimi nashangaa chakula kilivyokitamu dah”
Walikula huku wakisifia muda wote kisha walipomaliza Sophia alitoa vyombo na kwenda na mumewe chumbani kujimwagia kisha moja kwa moja kupumzika kwani walikuwa wamechoka sana na mizunguko ya siku hiyo ukizingatia ni tangu jana na lile varangati la nyoka.

Wakiwa wamelala Sophia alijiwa na ndoto na kuwa kama vile analiona tukio lote ambalo lilitokea usiku wa jana yake wakati wamelala hotelini, alijiona akiwa anaitwa na jinsi ambavyo mume wake alimkataza asiitike. Kisha akamuona binti njiani akionyesha kushtushwa na lile jina la Sophia lililokuwa likiitwa na moja kwa moja akaonyesha kuitika huku akielekea mahali ambapo anaitwa ila mbele kidogo akakiona kile kitoto ambacho huwa wanakutana nacho njiani ila kilionyesha kuwa na sura kama ya kiutu uzima na ghafla alitoa vitu vya ajabu na kumwagia Yule dada ambaye alianguka chini.
Sophia alishtuka sana na kupiga kelele ambazo moja kwa moja zilimshtua mume wake pia na kumfanya aamke kutoka usingizini huku akiuliza kwa mshangao kuwa mkewe ameona kitu gani.
Sophia alikuwa akitetemeka sana kisha akaanza kumueleza mumewe kile ambacho alikuwa amekiona kwenye hiyo ndoto,
“Mmh hayo ni makubwa mke wangu kwakweli tunatakiwa kuwa makini maana hiyo hali ni mbaya, unajua nini kwakweli kale katoto huwa sina imani nacho kabisa yani, kale katoto nahisi ni jini”
Sophia akashtuka sana na kumuangalia mumewe, kisha akamuuliza kwa mshangao,
“Jini tena mume wangu jamani dah! Mbona unaniletea habari za kutisha?”
“Sio habari za kutisha ila ndio ukweli huo mke wangu maana haiwezekani tuwe tunakutana nae njiani tena katika mazingira ya kutatanisha kiasi kile. Ila usijali mke wangu maana swala hili lazima nitalitafutia ufumbuzi tu.”
Kwakweli ile habari ya jinni ilimkosesha raha Sophia ingawa hata pale mumewe alipomtaka warejee kulala alijilaza tu bila ya kujiwa na usingizi tena kwani alijikuta akiwa na mawazo sana huku akikumbuka stori za zamani kuwa majini yanakuwa marefu sana yani huoni mwisho wao halafu chini yanakuwa na kwato za ng’ombe ila akawa anajiuliza kuwa mbona kale katoto ni kafupi sana je ni jamii gani ya jini, alikosa jibu kabisa huku usingizi wake nao ukiwa umekata kabisa.
Masaa yakapita akiwa macho tu kwa muda mrefu kitu kilichomfanya aboreke pale kitandani hivyo akaona vyema hata awahi kuamka zaidi ya siku zote. Ilipofika saa kumi na moja alfajiri aliona ni vyema ende kukaa sebleni tu kuona kama ataweza kusinzia labda na kuweza kulipiza usingizi wake wa usiku.
Akainuka pale kitandani na kwenda mpaka mlangoni ambapo alifungua mlango ila akasikia kama sauti ya Tv ikiongea sebleni kwakweli aliogopa sana ukizingatia mara ya mwisho mumewe alichomoa nyaya zote za kwenye Tv hiyo. Sophia akarudi chumbani kwa kasi ya woga kwani hakutaka kushuhudia kile kitu, moja kwa moja akenda kumuamsha Ibra aliyeonekana kuwa na usingizi mzito sana.
“Ibra Ibra tafadhali amka”
“Kwani vipi Sophia kuna nini jamani? Mi si nilisema leo siendi kazini, niache nipumzike”
“Najua kama huendi Ibra ila kuna kitu nataka ushuhudie”
“Kitu gani jamani?”
Ikabidi Ibra aamke na kumuangalia mkewe kisha kumuuliza tena kuwa ni kitu gani ambapo Sophia akamuomba Ibra moja kwa moja kwa muda huo aelekee sebleni ili akaone yeye mwenyewe, Ibra akainuka na kuelekea sebleni ila hakuona chochote ambapo Sophia nae alimfata nyuma. Kisha Ibra akamuuliza Sophia kuwa kulikuwa na kitu gani,
“Mbona hamna chochote kipya hapa sebleni! Ni kinini hicho ambacho ulikiona?”
“Tv ilikuwa inaongea yani kamavile ilikuwa imewashwa”
“Uliiona kabisa ikionyesha?”
“Hapana ila nilisikia sauti ndio nikakimbilia ndani kukuamsha”
“Mmmh maruweruwe hayo mke wangu ukizingatia na ndoto ambayo ulikuwa umeota usiku. Hapa hakuna lolote la kutisha mke wangu hata usiwe na woga wa aina yoyote ile, uwe na amani tu”
“Lakini nilisikia kabisa”
“Ilimradi hujaona ujue basi ni maruweruwe tu mke wangu. Umefanya na nini usingizi wangu wote ukatike jamani saa kumi na moja hii bado giza totoro nje”
“Nisamehe mume wangu lakini kwakweli sikuwa na jinsi zaidi ya kukuamsha tu.”
“Usijali, mi nakuelewa sana Sophy wangu”
Kisha Ibra akamuomba Sophia kuwa warudi tena chumbani kulala tu hadi saa moja maana siku hiyo hakuwa na mpango wowote wa kutoka asubuhi asubuhi.

Wakarudi chumbani ambapo Ibra alipojilaza tu usingizi ulimchukua tena na kufanya Sophia awe macho peke yake huku akiwa na mawazo mbalimbali.
Alikuwa akijiuliza kama kweli alisikia sauti ya tv au yalikuwa ni mawazo yake tu na maruweruwe kama mumewe alivyosema ila ilikuwa ni kweli kabisa kuwa alisikia mlio wa Tv kabisa, kwa mbali yale maneno ya Yule bibi aliyekutana nae kwa Siwema na kumwambia kuwa nyumba yake ni ya maajabu yakaanza kumuingia akilini na kuona kama kuna kaukweli flani ambako alikuwa akipingana nako ila alijiuliza kuwa je hayo maajabu yanaletwa na Jane au kuna mtu mwingine anayewafanyia mambo hayo ili kuwatisha kwenye nyumba yao?
Alipokuwa akiwaza hayo, kwa mbali akasikia tena sauti ya Tv na kufanya akurupuke pale kitandani ila kwa muda huu akajipa moyo wa ujasiri ambapo aliamua kwenda sebleni na kushuhudia kabisa kama ni Tv kweli au ndio maruweruwe yake kama mumewe alivyosema.
Sophia alitoka hadi sebleni ambapo kila aliposogea ile sauti ya Tv nayo ndio ilisikika zaidi, alipofika karibu na kuchungulia alikuta ni kweli Tv iliwaka na ilikuwa ikionyesha vizuri kabisa.

Itaendelea.....................!!!







from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/3a1XOk2

No comments:

Post a Comment