Thursday, February 27, 2020

NYUMBA YA MAAJABU 16


               

Ibra alisogeza gari yake mpaka getini kabisa kisha akashuka pamoja na Jane kuelekea ndani, na walipofika Ibra alifungua mlango wa ndani na kuingia ambapo Sophia na Neema walikuwa pale pale sebleni.
Ila Jane alipomuona Neema alishtuka sana na kufanya wote wamshangae kilichomshtua kiasi kile.
*TUENDELEE...*

Jane alianza kurudi kinyumenyume na kuwafanya washangae zaidi huku Ibra akimuuliza kuwa tatizo ni nini au ni kitu gani kakiona, ila Jane hakusema chochote na alionekana akizidi kurudi kinyumenyume na alipofanikiwa kufika nje alionekana akiondoka kwa kukimbia kabisa eneo lile.
Walibaki wakimshangaa na kutazamana tu, kisha Sophia akamuuliza mume wake
“Umetoka nae wapi Yule na kwanini aogope vile na kukimbia?”
Ibra alikosa jibu ila Neema alionekana akicheka na kisha kuwajibu yeye,
“Hivi unafikiri angeweza kuingia Yule na kukaa pamoja na mimi!”
“Kwanini asiweze?”
“Yule mtoto ni mchawi halafu alikuwa amekuja na vitu vyake vya kichawi, sasa kuniona mimi ameogopa sana sababu mimi ni mtu safi na siwezi kuingiliwa na wachawi. Ndiomana ameshindwa hata kunitazama mara mbili hapa”
Sophia akamuangalia mumewe na kumwambia,
“Umesikia sasa, Yule Jane ni mchawi ila nikisema mimi unaona kamavile namuonea haya sasa leo umesikia kwa macho yako tena licha ya kusikia umeweza kujionea mwenyewe jinsi alivyojawa na hofu hadi kukimbia. Kwa kweli Neema amekuja kuikoa familia yetu mume wangu”
Ibra hakuongea chochote kwani hata yeye hakutegemea kabisa lile swala la Jane kumkimbia Neema ambaye wao wanaishi nae ndani, alijikuta akiwa na maswali pamoja na mawazo mengi sana katika kichwa chake. Ila Sophia alijitahidi kwa muda huo kumuweka mumewe sawa ambapo akamwambia akae ili atulize akili, ila Ibra kabla hajakaa akakumbuka kuwa gari yake alikuwa ameiacha nje ya geti kabisa na hivyo kumwambia mkewe asubiri akaiingize kwanza.
Ila alipotoka ndani tu alikuta ile gari ikiwa imeshaingizwa ndani ya geti huku geti likiwa limefungwa vizuri kabisa, kwakweli akili ya Ibra ilikuwa kamavile inavurugika kwa muda huo kwani alijikuta akiwa haelewi elewi kabisa, kitendo hicho kilimfanya asimame sana pale nje bila ya kuingia ndani ikabidi Sophia amfate nje maana aliona akikawia.
“Si ushaingiza gari, mbona umesimama tu?”
“Hii gari sijaiingiza mimi”
“Sasa nani ameiingiza jamani mume wangu?”
“Hata mimi nashangaa sielewi kabisa”
“Mmh twende ndani bhana itakuwa umejisahau tu”
“Hapana siwezi kujisahau kiasi hiki Sophy dah! Akili yangu haipo sawa kabisa”
Kisha akaingia ndani na moja kwa moja akaelekea chumbani ambapo Sophia aliamua kwenda kumfata huko chumbani.

Ibra alionekana kujiinamia tu kitandani kwani ilionyesha wazi kuwa alikuwa na mawazo mengi sana, ikabidi Sophia aendelee kumpa moyo mumewe na kuwa karibu naye ili angalau aweze kumsaidia katika kumpunguza mawazo aliyokuwa nayo.
“Ni vitu gani unawaza kiasi hicho mume wangu?”
“Wewe acha tu Sophy, kwakweli akili yangu haipo sawa kabisa”
“Pole sana, basi itabidi ukoge ili angalau uchangamshe akili. Tafadhali Ibra mume wangu naomba ufanye hivyo”
Ibra alimuelewa mkewe na kuamua kufanya hivyo ambapo moja kwa moja alikwenda bafuni kukoga. Ila alipokuwa mle bafuni kila akifumba macho inamjia picha ya Yule joka pamoja na picha ya Neema kwakweli akajikuta akipatwa na woga kupita maelezo ya kawaida. Kitendo hicho kilimfanya atoke bafuni kwa haraka bila hata ya kukoga vizuri.
“Khee mume wangu umetoka hadi na povu sikioni”
“Wee acha tu Sophia, kuna muda nitakueleza na utanielewa vizuri tu”
“Nieleze sasa hivi mume wangu ili tushauriane cha kufanya”
“Hata kama nikikueleza sasa hivi sijui kama utanielewa mke wangu, nitakueleza tu pindi akili yangu itakapotulia”
“Basi twende ukale mume wangu”
“Hiko chakula nani kapika?”
“Amepika Neema”
“Mmh kama Neema hapana, sijisikii kula kwakweli”
“Kheee makubwa, sasa maana ya mdada wa kazi ndani ni nini jamani mume wangu?”
“Mdada wa kazi ni mtu wa kutusaidia kazi za humu ndani ila sio mpaka chakula cha mumeo apike mdada wa kazi”
Sophia alimshangaa sana mumewe kwani hakutegemea kama angeongea maneno kama hayo, aliona kuwa Ibra ni mwanamme asiye na huruma kwani anajua fika hali ya Sophia kuwa ni mjamzito ila bado alihitaji kupikiwa chakula naye, kwakweli Sophia alikuwa amechukia kwa kiasi kisha akainuka na kumwambia,
“Ngoja nikakuandalie chakula mwenyewe basi ili ufurahi”
“Unakwenda kuniandalia chakula gani?”
“Wali”
“Sitaki wali, nataka ugali”
Kisha Sophia akatoka mle chumbani na kumuacha Ibra akiwa mwenyewe amejiinamia tu kwa mawazo.

Sophia alikwenda moja kwa moja jikoni huku akiwaza kuhusu Ibra kutokuwa na huruma na hali yake, kisha akaona ni vyema amsongee tu huo ugali kwa haraka kisha amuandalie na mboga ya haraka aweze kula.
Akabandika sufuria ya kusongea ugali, kisha akaenda kufungua friji ili aangalie kama kuna mboga ya aina yoyote. Alipofungua ile friji alishangaa kwa muda kwa kila mboga aliyoifikiria kichwani mwake ilikuwemo mle akajiuliza kuwa ni Ibra alinunua mboga hizo au imekuwaje, ila moja kwa moja alihisi ni Ibra tu kwani hakuna mwingine ambaye angenunua zile mboga kama sio Ibra.
Akatoa samaki ambao walikuwa wamekaushwa vizuri ili awaunge na kumuandalia Ibra mezani, ila alipokuwa anageuka na wale samaki akashangaa kumuona Neema akiwa ameweka vizuri ugali kwenye sahani na kufanya amuulize kwa mshangao,
“Khee Neema umeingia saa ngapi humu jikoni?”
“Nimeingia wakati wewe unatafuta mboga kwenye friji ndio nikaamua nikusaidie kusonga huu ugali maana maji yalikuwa yanachemka.”
“Umejuaje kama yale maji yalikuwa ya ugali?”
“Kheee dada, ukizoea kupika basi itakuwa rahisi sana kujua kila aina ya pishi na ndiomana nimejua kwa haraka sana kuwa yale maji yalikuwa ya ugali na ugali huo tayari. Lete hao samaki nikupikie haraka wakati unaenda kuandaa huu ugali mezani”
Sophia hakuongeza neno bali alimpa Neema wale samaki kisha akabeba ule ugali na kuupeleka mezani huku akiwaza kuwa neema amewezaje kusonga ugali kwa muda mfupi kiasi kile! Akajiuliza,
“Ingawa ugali ni chakula cha haraka kupika ila mmh ndio kwa muda mfupi vile?”
Hakupata jibu na kurudi jikoni ambapo alimkuta Neema ameshamaliza kuunga wale samaki na alishawaandaa kwenye bakuli, Sophia alishtuka ila alishindwa kuuliza chochote ambapo alichukua ile mboga na kwenda kuweka mezani kisha akaenda kumuita mume wake.
“Chakula tayari Ibra”
“Mmh umepikia kompyuta au?”
“Kwanini?”
“Mbona kimekuwa haraka sana!”
“Nakujali mume wangu na ndiomana nimeharakisha”
“Sio swala la kunijali Sophia ila umetumia muda mfupi sana”
Kisha Ibra akainuka na kwenda mezani kula ambapo alikula huku akimsifia mkewe kuwa amepika chakula kitamu sana, Sophia alikuwa akitabasamu tu ingawa alielewa wazi kuwa zile sifa alipaswa apewe Neema maana ndiye aliyepika chakula kile, ila hakumwambia mumewe kwavile alikataa kula chakula kilichopikwa na Neema.
Ibra alipomaliza kula alimuuliza Sophia,
“Mbona huyu Neema muda wote namuona akiangalia Tv tu, hivi hachoki?”
“Kasema anapenda kuangalia Tv kuliko kitu chochote kile na ndiomana mimi huwa namuachaga tu aangalie, tena mara nyingine utakuta anaangalia na wala hata hajitingishi yani sijui kukaa vile hachoki”
“Labda hachoki, ila kwa mimi siwezi kwakweli kuangalia Tv muda wote siwezi. Sasa huko kupika na kazi nyengine za hapa atakuwa anazifanyaje?”
“Kazi anafanya vizuri ila ndio akishafanya anarudi tena kwenye Tv”
“Mmh basi sawa”
Ibra akainuka na kurudi tena chumbani kwao kwani hakutaka hata kukaa sebleni. Ila Sophia alikwenda kukaa na Neema ambaye muda wote alikuwa makini kuangalia Tv tena kuna kipindi alionekana kutokupepesa hata macho na kumfanya Sophia ajiulize zaidi kuwa huyu Neema hachoki.
Walikaa pale hadi giza lilipoingia na kuwasha taa za ndani, kisha Sophia akainuka na kuelekea chumbani alipo mumewe.
Alimkuta akiwa amejiinamia tu kama ambavyo alijiinamia mwanzo,
“Kheee hayo mawazo Ibra sasa yamezidi jamani. Tushirikishane hutaki sasa hata sijui ndio nini wakati mimi ndio mkeo”
Ibra muda huu alimuuliza swali Sophia,
“Hivi Sophy una uhakika kuwa Jane ni mchawi?”
“Jane ni mchawi ndio tena ni mchawi aliyekubuhu”
“Mmh sio kwamba anasingiziwa?”
“Hivi mume wangu huyo Jane ana lipi labda la kusingiziwa? Hata kama kusingiziwa ndio watu wote hawa wanamsingizia? Tuseme mimi namsingizia, da’ Siwema je anamsingizia? Yule mganga je? Na Neema je anamsingizia? Yule Jane hata hasingiziwi mume wangu ni mchawi kweli, na bora tumepata kiboko yake humu ndani maana hatokanyaga tena nyumba hii na mauchawi yake”
“Dah! Nashindwa kuamini kwakweli maana mi ninavyomuona Jane ni wa kawaida tu”
“Kwani unafikiri mchawi ukimuona unamjua kwa haraka hivyo? Huwezi kumjua sababu anakuwa ni mtu wa kawaida tu halafu wanajifanya wana roho nzuri balaa kumbe roho zao ni za kichawi. Kwakweli mume wangu tunatakiwa kushukuru sana uwepo wa huyu Neema humu ndani”
Kisha Sophy akamuomba mumewe waende sebleni wakapate chakula cha usiku,
“Ila najisikia kushiba sijui kama nitaweza kula”
“Sasa ungependa chakula gani kwa usiku huu?”
“Labda ningepata mkate tu na chai au maandazi tu na chai maana nimeshiba mke wangu”
“Basi twende tukanunue mkate, tuchemshe chai tunywe mume wangu”
Wakakubaliana kufanya hivyo, kisha kwa pamoja wakatoka mle chumbani.

Walipofika sebleni walimkuta Neema akiwa pale pale kwenye Tv ila alipowaona tu akawakaribisha waende mezani, Sophia akamuuliza alichoandaa
“Itakuwa vyema kama mkisogea pale wenyewe muone nilichowaandalia”
Sophia akamshika mumewe mkono na kwenda nae mezani ambapo walikuta Neema amewaandalia maandazi na chai, Sophia akatabasamu na kumwambia mumewe
“Hakuna haja tena ya kwenda dukani mume wangu kwani chakula ulichohitaji kipo tayari”
“Amejuaje kama tunahitaji chakula hicha muda huu?”
“Labda kwavile kaona tumekula jioni”
Kisha Sophia akamsihi mumewe akae pale mezani na waweze kula kile chakula ambapo Ibra alifanya hivyo na kukaa pale mezani halafu wakaanza kula ila Ibra alimuuliza Sophia kuwa huyo Neema amekula muda gani,
“Ngoja nimuite umuulize mwenyewe”
Sophia akamuita Neema ambaye aliwafata pale mezani na kuwasikiliza walichomuitia, Ibra akamuuliza Neema
“Mbona huji kula na sisi?”
“Mimi nimekula jikoni kwahiyo sina njaa tena”
“Usije sema tunakutenga, tafadhari siku nyingine tuwe tunakula pamoja umesikia Neema”
“Sawa msijali nimewaelewa tutakuwa tukila pamoja ila tatizo ni kuwa hamtashiba”
“Hatutashiba kivipi?”
Neema akacheka na kujibu kamavile mtu anayetania,
“sababu nakula sana”
Sophia akacheka pia na kumwambia,
“Ungekuwa unakula sana si vyakula vingekuwa vimeisha humu ndani jamani, Neema bhana tuwe tunakula pamoja ndio vizuri”
“Sawa dada nimekuelewa nitakuwa nafanya hivyo”
Kisha akarudi tena kwenye kuangalia Tv na kuwaacha Sophia na Ibra wakiendelea kula.
Walipomaliza kula, Ibra akamwambia mkewe kuwa anaona vyema yeye akalale tu kwani amejawa na uchovu sana,
“Sawa mume wangu,na mimi nitakuja kulala muda sio mrefu”
Ibra akaenda chumbani kisha Sophia akenda sebleni kukaa na Neema huku akijaribu kumuuliza kuwa ameionaje siku,
“Neema siku ya leo umeionaje na maisha ya humu ndani umeyaonaje kwa ujumla?”
“Nimeipenda na kuifurahia sana siku ya leo kwani inaonyesha wazi kuwa maisha yangu humu ndani yatakuwa ni yenye furaha”
“Na vipi ule ujio wa Yule Jane?”
“Yule hawezi kuja tena hapa, popote ninapokuwa hakuna mtu mbaya anayeweza kusogea ndiomana Yule alikimbia mwenyewe maana asingeweza kukaa na mimi karibu”
“Nafurahi kusikia hivyo maana alikuwa ananikera sana Yule binti, ngoja nikutakie usiku mwema ingawa sijui utaenda kulala saa ngapi”
“Muda sio mrefu na mimi nitaenda kulala hata usijali dada”
Sophia akaelekea chumbani ambapo alimkuta mumewe akiwa amelala hoi kabisa kisha nae akajiunga kwenye kulala pembeni ya Ibra.

Usiku wa manane Ibra alishtuka kutoka usingizini ambapo alihisi kamavile tumbo lake limevurugika hivyo akaamka na kukaa kitandani ila aliona ni vyema anywe maji hivyo akainuka na kuelekea jikoni ili akachukue maji. Ila alipofika sebleni alishangaa kumuona Neema akiangalia Tv ila kwavile mkewe alimwambia kuwa Neema anapenda sana Tv hakushangaa zaidi ila aliona ni vyema amuulize kuwa hana usingizi au imekuwaje.
Ibra akamsogelea Neema na kumuuliza,
“Vipi mpaka saizi, huna usingizi?”
Neema aliinua sura yake na kumuangalia Ibra, kwakweli Ibra hakuweza kumtazama Neema mara mbili kwani macho ya Neema yalikuwa yakiwaka moto na kumfanya Ibra apige kelele za woga kwa mara ya kwanza katika maisha yake.

Itaendelea...............……!!!
.





from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/38aeWTu

No comments:

Post a Comment