Tuesday, February 4, 2020
KITUMBUA CHA KIHINDI SEHEMU YA PILI (2)
“Ahaa! Ni kweli. Sasa unatakiwa kusaini kwanza hapa. Gharama yake buku mbili” alisema afande yule huku akimfunulia daftari.
Magosho akakumbuka kuwa mfukoni mwake kulikuwa kumesalia shilingi elfu mbili tu. Inamaana kama angetoa buku mbili ile basi angerudi kwa miguu kwasababu angekosa hata nauli.
“Yaani broo hapa unaponiona nina buku tu mfukoni” Alisema Magosho kwa sauti ya kubembeleza.
“Sasa unadhani tutafanyaje?”
“Naomba nisaidie ndugu yangu”
“Siwezi, kama huna pesa we ondoka tu” alisema afande huku akifunga daftari lake.
ENDELEA…2
Magosho akapata wazo la kuondoka halafu arejee baadaye akiwa na uamuzi sahihi. Alihofia kukurupukia maamuzi halafu baadae kuambulia majuto.
“Aroo we Mujamaa” Afande alimuita Magosho wakati alipokuwa akiondoka.
Magosho akageuka nyuma kumuangalia. Askari yule alimuoneshea ishara ya kumuita kwa kutumia kirungu chake. Magosho akarejea kwa mwendo wa kujivuta akiamini askari yule alikuwa akimsumbua bure.
“Lete hilo buku lako” alisema mgambo yule huku akifungua daftari amabalo mwanzo alilifunga baada ya kutajiwa shilingi elfu moja. Magosho alipotoa ile pesa alimkabidhi lakini mgambo yule alikataa kuipokea na kumwambia aiweke juu ya daftari.
Kitendo kile kilimfanya Magosho kubaini kuwa kumbe mchango aliokuwa akiutaka askari yule ulikuwa ni kinyume na sheria. Ilimbidi atoe tu, sasa angefanya nini wakati yeye ndiye mwenye shida. Baada ya kutoa pesa alisaini kwenye daftari lile na kuelekea mapokezi.
Alipofika aliwakuta vijana wengine wamekaa kwenye foleni wakisubiri kufanyiwa usaili, na yeye akajiunga nao. Ulifika muda ambao aliitwa ndani kwenda kuonana na wahusika, yaani waajiri wenyewe. Alipoingia aliwakuta watu watatu wanaume wawili na mwanamke mmoja. Baada ya kuwasalimia walimuelekeza mahali pa kuketi.
“Karibu kijana” alisema mmoja wa wahusika wale.
“Asante sana” Magosho alijibu kwa unyenyekevu.
“Unatokea wapi?”
“Mbagala”
“Elimu yako?” mwanamke yule alihoji swali ambalo lilikuwa ni adui kwa Magosho. Hakupenda kulisikia katika masikio yake na ndilo lililomfanya kukosa ajira kwenye ofisi nyingi sana. Lakini hata kama alikuwa halipendi swali lile lakini ndio alikuwa amekwisha ulizwa hivyo hakuwa na namna zaidi ya kulijibu. Sasa shughuli ikaja ajibu nini? na kama angesema ameishia elimu ya msingi kungekuwepo na uwezekano wa kupoteza nafasi ingawa walikuwa wanaajiriwa hata wale wasio na elimu kubwa.
“Nimesoma hadi kidato cha nne” alijikuta akitamka.
“Umekuja na uthibitisho?” alihoji yule mama.
Siku ya kufa nyani miti yote hutereza, akashangaa sababu ya watu wale kumuuliza masuala ya elimu wakati kwenye matangazo yao wamesema wanawaajiri hata wale wasio na elimu. “Mnh hii sasa kali” akajisemea kimoyomoyo.
“Sikuja na uthibitisho wowote” akajikuta akiwajibu pasipo kujielewa.
“Ok usijali, hilo sio tatizo. Kama unahitaji ajira basi tutakuajiri” alidakia jamaa mmoja aliyekuwa pamoja na yule mama mle ndani.
“Labda tuambie kama kweli unahitaji kazi” alisema mtu mmoja.
“Nahitaji na ndiyomaana nipo hapa” Magosho akajibu kwa kujiamini.
“Sasa sisi tutajuaje kama kweli unahitaji ajira?” yule mwanamke akatupa swali.
“Kuja kwangu hapa inatosha ninyi muamini”
“Hilo halitoshi. Hebu thibitisha kauli yako”
“Amini nawaambia nahitaji kazi”
“Sikiliza kijana. Kwaufupi ni kwamba mkono mtupu haurambwi” alisema yule mama huku akijifanya yuko bize na kuandika andika vitu alivyokuwa anavifahamu yeye.
“Bado sijaelewa” Magosho alizungumza kwa mshangao.
“Kazi zipo kijana lakini kalamu ya kuandikia jina lako imekwisha wino” alisema mama yule huku akiendelea kuandika andika.
Magosho akatafakari kauli ile kwa umakini. Mtu anasema kalamu imekwisha wino inakuwaje anaendelea kuandika?.. Jibu alilolipata pale ni kwamba alikuwa anatakiwa kutoa chochote kitu. Wakati akiendelea kutafakari kauli ile sauti ya mwanaume ikamgutusha.
“Hata kama ukipata hamsini inaweza kutosha”
“Hamsini nini?” alihoji Magosho kwa mshangao.
“Alloo ajira hakuna naona unatuzunguusha” alisema jamaa kwa hasira.
“Ngoja kwanza Ngosha, Kijana nenda ukajipange halafu ukiwa tayari siku yoyote uje” yule jamaa mwingine alizungumza kwa sauti ya upole.
Kwakuwa Magosho alikwisha tambua ni kitu gani kilichokuwa kikitakiwa pale na hakuwa na uwezo wa kukipata alijiinua kwenye kiti na kutoka nje. Alikuwa amechoka kuliko maelezo. Hakuwa na namna zaidi ya kurejea nyumbani.
*****
Magosho alipofika nyumbani alikwenda moja kwa moja chumbani kwake pasipo kupitia kwa ndugu yake kumjulia hali. Akajitupa kitandani kwa nguvu kutokana na uchovu, kitanda nacho kikaitikia “Rabeka”. Kilikuwa kimevunjika kutokana na kushindwa kuhimili kile kishindo cha Magosho.
Ashura alishituka baada ya kusikia sauti ya kitu kikianguka chumbani kwa kaka yake. Alichokuwa akikifahamu yeye ni kwamba kaka yake huyo hakuwepo. Alifungua mlango na kuchungulia ndani. Alimkuta kaka yake amelala huku kitanda kikiwa kimevunjika.
“He kumbe umerudi?” alihoji Ashura kwa mshangao.
“Ndio nimeingia sasa hivi” alijibu Magosho huku akijizoa zoa kutoka pale chini.
“Kwahiyo ndio ukaamua kuvunja kitanda?”
“Ah! Nimechoka bwana”
“Sasa ukichoka ndio unavunja kitanda?”
“Bahati mbaya” Magosho alijibu kwa upole.
“Mavi yenyewe uharo halafu unayatia maji. Sasa utalala wapi?”
“Nitakitengeneza bwana!” Magosho alijibu kwa hasira kidogo, inaonekana hakupendezwa na maswali ya ndugu yake.
“Au ndio ulikuwa unapigana na yule nzi?” Ashura alihoji huku akicheka.
“Hebu ondoka Ashura, usinichanganye”
“Kweli nini! Mbona umekasirika?” Ashura alizidi kumtania kaka yake ambaye alikuwa ametawaliwa na uchovu pamoja pamoja na mawazo yaliyo changanyikana na hasira. Alichukua tena mti wa ufagio na kumkimbiza mdogo wake huku akimtishia kumtandika. Ashura akiwa mbele na yeye nyuma hadi kwa mama yao ambaye alikuwa amejipumzisha kwenye mkeka barazani.
“Mamaaa…mamaaa….mamaaa” Ashura alikuwa akikimbia huku akipiga kelele.
Mama Ashura alishituka kutoka usingizini. Masikini kumbe alikuwa hajisikii vizuri kiafya.
“ Mama mwanao nitampiga huyu” alisema Magosho huku akisogea hadi pale alipokuwa amelala mama yake.
“Vipi mama mbona umelala saa hizi unaumwa?” alihoji Magosho kwa sauti iliyojaa upendo na wasiwasi.
“Afadhali umerudi mwanangu” alisema mama Ashura kwa sauti ya chini.
“Una nini mama?”
“Vipi kwanza huko mjini, umefanikiwa?”
“Hakuna kitu mama, tatizo pesa. Kila mahali wanataka rushwa, yaani rushwa, rushwa inanuka” alisema Magosho kwa sauti kavu iliyokata tama
“Usikate tamaa mwanangu, mtafutaji hachoki” mama Ashura alizungumza kwa sauti ya chini isiyo ya kawaida.
“Vipi lakini mama unaonekana haupo sawa” alihoji Magosho.
“Nahisi kuumwa viungo vyote, Ila mgongo na kiuno ndio vinaniuma zaidi” alisema mama Ashura huku akijipepea kwa upande wa kitenge kutokana na joto la jijini Dar Es Salaam.
“Sasa umekunywa dawa?”
“Nimekunywa panadol, nenda kwa mama Mbingu akakupe mzizi wa muarobaini nije kuchemsha” alisema mama Ashura.
Wakati Magosho alipokwenda kuchukua dawa hiyo ya muarobaini huku nyuma hali ya mama Ashura ilibadilika na kuwa mbaya zaidi.
Ashura alimfuata kaka yake na kumfahamisha hali halisi. Magosho pamoja na mama Mbingu wakaongozana hadi kwa mama Ashura. Kwa kweli hali waliyoikuta pale haikuwa ya kuridhisha hata kidogo.
“Nyie watoto mnahatari!... mama yenu anaumwa hivi mmemuweka tu ndani” alisema mama Mbingu kwa mshangao baada ya kuona hali ya mama mwenzie.
“Hali yake haikuwa hivi, amezidiwa sasahivi nilivyokuja kwako” aliizungumza Magosho.
“Haya tumpelekeni kwa Mzee Kutuzo haraka sana” alisema mama Mbingu na pasipo kuchelewa walimchukua na kumpeleka kwa mzee Kutuzo ambaye alikuwa ni mganga wa kienyeji.
*****
Baada ya kufika kwa mganga kwanza kabisa alitoa dawa kama huduma ya kwanza. Kwa kiasi fulani dawa ile aliyompa ilionekana kufanya kazi kwani mama Ashura alianza kupata ahuweni. Jambo ambalo lilileta matumaini kwa watoto wake pamoja na mama Mbingu.
Baada ya kutoa huduma ile mganga alianza mbwembwe zake za jadi na kupandisha maruhani. Lengo kubwa lilikuwa ni kutaka kuufanyia uchunguzi mwili wa mama Ashura ili apate matibabu yaliyo sahihi.
Jini alipanda na kuanza kuzungumza lugha ngeni kwenye masikio ya wateja wake. Aliendelea kutabana huku akiwa ameshikilia kipande cha kioo kilichokuwa kimefungwa fungwa vitambaa vilivyokuwa na rangi tatu, yaani nyeupe nyeusi na nyekundu. Mganga alikuwa akipiga mbweo mithili ya mtu aliyekuwa ameshiba sana. Watu wote walikuwa kimya wakimsikiliza mganga.
“Mgonjwa anaitwa nani” alihoji mganga Kutuzo.
“Mama Ashura” alijibu mama Mbingu.
“Jina lake la utotoni?”
“Mainaya” alijibu Magosho.
Mganga aliendelea kuzungumza maneno yake ya kiganga huku akitaja jina la Mainaya mara kwa mara. Baada ya sekunde kadhaa alitupa kile kioo na yeye akadondoka chini na kuanza kuunguruma kama mbwa.
Hali ile iliwashangaza sana wakina Magosho na wenzake. Hawakufahamu wafanye nini lakini mama mbingu ambaye alionekana kuwa mzoefu wa mambo yale akawaambia watulie.
Mganga alilala pale chini kwa dakika kadhaa halafu akainuka. Alichukua upembe mkumbwa wa mnyama uliokuwa umefungwa kitambaa cheusi na kuanza kumzunguushia nao mama Ashura. Alifanya zoezi lile mara kadhaa halafu akaokota kibuyu kilichokuwa na shanga kwenye shingo yake na kutoa dawa ambayo alimpaka mama Ashura usoni kisha akarudi kukaa kwenye kiti chake. Akaokota kile kioo chake na kukipiga piga kwa usinga wake mara kadhaa huku akikichungulia chungulia.
“Niseme nisiseme” alizungumza mganga yule kwa sauti nzito
“Sema mganga” alijibu mama Mbingu.
“Mainaya ametupiwa Jini ” alisema mganga huku akichungulia kioo chake.
“Mungu wangu!” alihamaki mama Mbingu.
“Jini?” Magosho akahoji kwa mshangao.
“Ndio tena Jini maiti” mganga alizidi kufafanua.
Magosho, Ashura pamoja na mama Mbingu wakawa wanatazamana wasijue cha kuzungumza. Mganga akavunja ukimya ule.
“Zaidi ya hayo Kuna vitu amelishwa ambavyo sio vizuri” mganga alizidi kuleta changamoto hasa kwa watoto wa mgonjwa.
ITAENDELEA
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2v3Lros
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment