Monday, February 24, 2020

STORY: KISA MAPENZI TU SEHEMU YA: 16




*******************
ILIPOISHIA
Gari hili la watekaji lilipotoka nje kabisa ya eneo la Hotelini liliweza kuingia mpaka kwenye barabara kubwa ya Lami na kuanza kutokomea kwa kasi kubwa sana huku na mimi nikiwemo 'Mateka' ndani yake! 👉👉ENDELEA NAYO SASA👇👇

Ndani ya gari hii jumla tulikuwa watu watano watekaji hawa walikuwà wanne pamoja na mimi hapa, kule upande wa mbele walikaa wawili na huku upande wa nyuma tulikuwa watatu huku mimi ndio nikiwa nimedhibitiwa katikati hapa kwenye hii siti ya nyuma. Yaani upande wa kulia alikaa baunsa na kushoto kwangu pia alikaa baunsa! "Jamani sasa mnanipeleka wapi nyie watu, na nimewakosea nini kwani?" nilijaribu kuwauliza. "Funga huo mdomo wako mpumbavuu wewe, tulia utaenda kupaona unapopelekwa" alinijibu jamaa mmoja wa huku nyuma tulipokaa. "Oyaa Stopa inakuaje bado amjamziba macho huyo kenge?" alisema jamaa wa kule mbele ambaye ndio alikuwa ni dereva wa gari hii. Bila kuchelewa huyu jamaa aliyeitwa kwa jina la Stopa akachukua kitambaa cha rangi nyekundu na kuanza kunifunga nacho machoni mwangu hakujali machozi yangu ambayo kwa muda huu  yalikuwa yameshaanza kunitoka. "Tayari nimeshamfunga macho" alisema huyo jamaa Stopa. Safari ya kuelekea sehemu isiyojulikana ikaendelea huku mimi ndio hivyo tena nikinyimwa hata nafasi ya kuona huko ninapopelekwa kwa kuzibwa macho yangu na kile kitambaa nilichofungwa.
Moyoni mwangu sasa nilianza kujilaumu na kujiuliza hivi ni kwanini nilijiingiza kwenye haya Mahusiano ya kimapenzi na Prisca, nikaanza kuyakumbuka maisha yangu ya dhiki Yale niliyokuwa naishi kule Kipawa Karakata 'Uswahilini' na kuyaona yana afadhali kubwa sana kuliko hata haya maisha mazuri na ya raha ambayo Prisca alitaka niishi naye kule nyumbani kwake, sasa hivi ndio yananigharimu maisha yangu. "Yaani ndio naenda kufa kweli eti Kisa mapenzi tu?" nilijikuta najiuliza hilo swali ndani ya moyo wangu huku bado machozi yakiendelea kunitiririka na kukilowanisha hiki kitambaa nilichofungwa nacho machoni mwangu. Pia niliweza kumsikia yule jamaa baunsa aliyekuwa amekaa kule mbele na dereva akimpigia simu huyo mtu aliyewatuma kuja kuniteka mimi na kumjulisha kuwa tayari wamefanikiwa kuniteka na sasa ndio wapo njiani kunipeleka huko mafichoni. Kwa upande wangu nilijua kabisa huyo mtu aliyewatuma hii kazi watekaji hawa atakuwa ni Benny pamoja na Eddy ambao ndio mara ya mwisho walinitishia maisha kule nyumbani kwa Prisca Jana asubuhi walipokuja na kunikuta pale. "Daah sijui kama nitapona mimi huko mbele ya wale watu?" niliendelea kujiuliza maswali huku bado machozi yakinibubujika. Baada ya yule jamaa kumaliza kuongea na simu nikaweza kumsikia akiwaambia wenzake: "Aisee mkuu amefurahi sana kusikia tumemkamata huyu Pimbi, amesema tumpeleke kule Kinyerezi tukamfungie mpaka yeye atakapokuja hapo baadae" alisema jamaa huyo akiwaambia wale  wenzake, mimi nilibakia tu najililia mwenyewe na nafsi kwani sikuwa najua nini kinaenda kunikuta huko ninapopelekwa na pia sikuwa najua nini kiliendelea kule kwenye eneo la Hoteli kwa upande wa Prisca mara baada ya mimi kutekwa na hawa majamaa!.
***************
Baada ya mwendo wa muda mrefu kutoka kule SINZA HOTEL ambapo ndio nilipotekwa hatimaye nilihisi gari hii ya hawa watekaji ikipunguza mwendo na kusimama kabisa halafu nikamsikia dereva akipiga honi ya gari, hii ni ishara ya kuwa tayari tumeshafika kwenye hiyo sehemu waliyokuwa wamekusudia kunileta. Mapigo yangu ya moyo yakaanza kunienda mbio na kuona sasa muda wangu wa kuishi duniani umeisha! Mara nikasikia sauti ya Geti kubwa likifunguliwa na gari ikaweza kuingia ndani halafu huku nyuma Geti likafungwa tena, gari ilienda na kusimama halafu ikazimwa kabisa na milango ya gari ikaanza kufunguliwa na mimi nikaanza kushushwa kwa nguvu. "Oyaa wee kunguni tayari umeshafika kwenye kiama chako" aliniambia Jamaa mmoja huku akinifungua kile kitambaa nilichofungwa nacho machoni. Baada ya kufunguliwa kitambaa nikaweza kuona mazingira ya humu ndani tulipoingia, japo macho yalikuwa ni yenye kuona maruweruwe yaliyosababishwa na kile kitambaa nilichofungwa machoni kwa muda mrefu. Lakini niliweza kuona haya mazingira ya hapa ambapo lilikuwa ni jumba la kifahari sana huku kwa uwañi kulikuwa na uwanja Mkubwa sana uliozugushiwa Uzio wenye mitambo ya kuzuia wezi kwa juu ya ukuta (Fen's) magari mawili ya kifahari nayo pia niliweza kuyaona hapa sehemu ya uwani pamoja na vijana kama sita hivi waliojazia miili yao (Mabaunsa) ambao walionekana kama ni walinzi wa hapa huku wakiwa wamebeba silaha nzito pamoja na Mbwa wanne walioshiba. Wakaanza kuniongoza kwa kuniswaga kama vile Ng'ombe kuniingiza ndani ya hilo jumba la kifahari huku wakiwa wamenidhibiti kwa kunizunguka yaani nilikuwa nimewekwa katikati tukitembea, japo ilikuwa bado ni majira ya asubuhi lakini sikuwa najua ni saa ngapi. Baada ya kuwa tumeingia ndani ya hili Jumba tuliweza kutokezea kwenye sebule moja kubwa sana nadhifu na yenye kuvutia huku ikiwa imepambwa kwa Fenicha za gharama kubwa! Hapo sebuleni atukukaa tukapitiliza moja kwa moja kwenye korido ndefu ambayo pembeni yake ilikuwa na msururu wa vyumba kama vinane (8) hivi na vyumba vyote vikiwa vimefungwa milango yake, safari yetu ikaenda kuishia kwenye chumba cha mwisho kabisa ambacho mlango wake ulikuwa umepakwa rangi nyekundu tofauti na ile milango ya vyumba vungine sijui kwanini mlango huu upo tofauti. Baada ya kufunguliwa mlango nikaingizwa mpaka ndani ya chumba hicho huku bado nikiwa nipo chini ya ulinzi Mkali wa hawa mabaunsa ambao wameniteka! "Sasa bwana mdogo hapa ndio umeshafika, subiri kidogo mwenyeji wako atakuja kuamua juu ya hatima ya maisha yako" aliniambia Baunsa mmoja aliyeonekana kuwa ni kiongozi wa hapa ambaye tulimkuta humuhumu ndani ya hili jumba. Baada ya hapo akaamuru nivuliwe fulana pamoja na suruali halafu nifungwe na minyororo kwenye kiti cha nyuma ambacho ndio pekee kilikuwepo humu ndani ya hiki chumba, "Lakini jamani kwani mimi nimewakosea nini mpaka mnanifanyia hivi?" niliwauliza. TUUUUUU! Huo ni mlio wa ngumi nzito iliyotua 'Mubashara' kwenye paji la USO wangu na kupelekea nione maruweruwe kama sio mapichapicha mbele yangu! "Hatutaki maswali ya kipuuzi hapa, majibu ya hayo maswali yako msubiri mwenyeji wako atakuja kukujibu" aliunguruma baunsa huyo aliyenitwanga hiyo ngumi. Basi ikabidi niwe mpole na kunyamaza kimya, punde damu ikaanza kunitoka puani na mdomoni kutokana na ile ngumi niliyopigwa! Wakanivua nguo zote na kunibakisha na boksa tu ya ndani niliyoivaa halafu wakanikalisha kwenye kiti na kuanza kunifunga hiyo minyororo kama vile mbuzi ninayesubiri kuchinjwa. "Sasa kijana utakaa hapo mpaka mwenyeji wako atapofika" aliniambia baunsa Huyo huku akiachia tabasamu baya la kifedhuri usoni kwake na kuzidi kuchukiza. Halafu baada ya hapo watu wote wakatoka humu chumbani na kufungia mlango kwa nje huku wakiniacha ndani peke yangu! "Ooho mungu wangu angalia nimeletwa hapa kuja kuteketea, naomba unionyeshe miujiza nipate kuokoka" nilisema huku nikilia machozi. Nilijilaumu na kuona bora hata ningetoroka Jana usiku uleule kabla ya Prisca ajarudi tena pale Hotelini kama ningejua yatanikuta haya Majanga, nikajikuta ghafla nimeanza kumchukia Prisca na kumuona yeye ndio chanzo cha haya Majanga yote ya mimi kutekwa, "Bora ningebakia na maisha yangu yaleyale ya kushindia kunywa uji wa chumvi na kuvaa yeboyebo, angalia sasa mapenzi yananiua" nilijisemea kwa huzuni huku nikilia na kusindwa kabisa kufurukuta hapa kwenye kiti nilipofungwa. Nilichokuwa nakisubiri kwa sasa ni kifo tu ambacho ndio nilikiona mbele yangu kinaninyemelea hapa kwenye hii sehemu, nilisikitika sana kujiona nakufa bila hata ya kumuaga bibi yangu huko kijijini alipokuwa na ikiwa siku hii ya leo ndio tulipanga kwenda kumuona bibi kabla ya kutokea kwa hili tukio langu la kutekwa. Sikuwa na matumaini ya kutoka nikiwa mzima kwenye eneo hili pindi huyo mwenyeji wangu atakapofika kama vile walivyosema wale walioniteka na mwenyeji mwenyewe nilimuhisi atakuwa ni yule Benny mpenzi wake wa zamani Prisca pamoja na Eddy kaka yake Prisca. Nikiwa bado naendeleà kutafakari hapa kwenye hiki kiti nilipofungwa na minyororo Mara ghafla mlango wa humu chumbani ukafunguliwa na mabaunsa wapatao watatu wakaingia kwa fujo huku kwa nyuma yao wakifuatia Benny pamoja na Eddy na mwanaume mmoja mwenye asili ya Kichina aliyevaa mavazi ya kidaktari sikuweza kujua ni kwanini walikuja na huyu daktari wa kichina hapa. Kitendo tu cha kumuona Benny na Eddy nikajua hapa tayari kumeshakuchaa!.

ITAENDELEA ...





from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2PmdKWt

No comments:

Post a Comment