Sunday, March 22, 2020

UTANIKUMBUKA TU SEHEMU YA PILI-02





"Kayumba, kwa sasa sihitaji ngojera zako. Nimeshakwambia kuwa tayari nina mtu wangu. Na hivi karibuni tunaraji kufunga ndoa. Hebu jitazame, hivyo ulivyo unaweza kunimiliki mimi? Mimi ni msomi lakini pia mimi ni mwanamke mzuri nahitaji matunzo ya ghalama, wewe huwezi kunihudumia ", aliongea Catherine huku akimzunguka Kayumba ambaye kwa muda huo alikuwa amesimama, uso wake ukionyesha huzuni. Machozi mithiri ya jasho yalimtiririka. Hakuamini maneno ayasemayo Catherine.  Kwa sauti ya huzuni na kilio, Kayumba aliongeza kusema.
" Catherine, inamaana umesahau msaada wangu juu yako? Kumbuka nilidiriki kujinyima ili wewe upate kile anacho kitaka Catherine. Kijijini waliniita kila aina jina la kuchukiza, na yote sababu ya kukuhudumia wewe ingali familia yangu siijali. Umesahau kuwa pasipo mimi kukulipia ada na kukusaidia mambo mengine zaidi leo usingekuwa na maisha haya? Elimu yako ndio kitu pekee unachojivunia mpaka kufikia hatua ya kuvunja ahadi yetu si ndio?", alipiga magoti, akayafuta machozi yake kisha akaendelea kusema." Nipo chini ya miguu yako, tafadhali rudisha moyo wako nyuma Catherine. Usidanganywe na hawa mabishoo wa mjini. Nakupenda sana Catherine wangu ".
"Nimeshakwambia sipo tayari kwa hilo, tena naomba uondoke ndani ya nyumba yangu haraka sana iwezekanavvyo" alisema Catherine kwa hasira. Maneno ambayo yalimfanya Kayumba kuzidi kutiririsha machozi. Moyo ulimuuma. Na wakati Kayumba yupo kwenye hali hiyo punde alikuja mpenzi wake. Ni mwanaume aliyeonekana shupavu kulingana na muonekano wa mwili wake ulivyo. Kwenye sikio lake la kushoto alivaa hereni. Kayumba alistuka alipomuona mwanaume huyo, alinyanyuka kutoka chini huku akimtazama kwa jicho la hasira. Akataharuki wakati huo huo mwanaume huyo alimkumbatia Catherine kwa mahaba mbele ya macho yake. Roho ilimuuma sana Kayumba, ni kama mwanaume huyo alizidi kumtonesha kidonda. Baada ya kitendo hicho,  sauti ilisikika ikisema "Huyu ndio umemuona anafaa kukusaidia kazi?.."
"Hapana mpenzi wangu, huyu kaka alikuwa mpenzi wangu zamani sana enzi za utotoni kijijini" Alijibu Catherine, akimjibu mpenzi wake juu ya kile alichouliza. Aliitwa Johnson.
  "Oooh! Eeh kwahiyo?" aliuliza Johnson.
"Amenifuata ili turudiane, ni jambo ambalo haliwezekani katika maisha yangu. Johnson hivi unionavyo mimi wa kuishi na huyo huyo mwanaume? Asiye na mbele wala nyuma?."
  "Hapana kamwe haiwezekani, labda kama atapenda tumpe kazi ya kusafisha mazingira hapa nyumbani ili ajikimu na maisha. Ahahahah huwenda kaupenda mji"
  "Hana maisha marefu hapa uraiani tangu atoke jela, kumpa kazi huyu mtu ni kukaribisha hasara humu ndani. Huyu mtu ni mwizi Johnson hafai kabisa",alidakia Catherine, maneno hayo aliyaongea kwa  nyodo, Kayumba alishangazwa sana na maneno hayo,alibaki kuduwaa huku mikono akiwa ameiweka kichwani. Alishusha pumzi ndefu kisha akasema "Braza. Najua humpendi kwa dhati Catherine ila upo kwa niaba ya kumchezea tu. Hujui ni wapi mimi yeye tumetoka  lakini hakuna shida, nimekubali kushindwa. Catherine naondoka ila nina imani ipo siku ipo siku utanikumbuka tu". Alipokwisha  kusema hayo Kayumba alizipiga hatua kuelekea getini tayari kwa safari ya kuondoka ndani ya nyumba ya Catherine. Aliumia sana ndani ya moyo wake, katu hakuamini kama Catherine angeliweza kuthubutu kuvunja nadhiri yao.
   "Hahaha hahahahah!.." kicheko cha mlinzi kilisikika, na punde akasema "Pole sana kijana, karibu Dar es salaam sasa. Nafikiri ulishindwa kusoma alama za nyakati kaka. Tangu lini mchumba akasomeshwa? Ni heri pesa zako ungelima mpunga, kuliko kumsomesha mchumba. Kwa kiswali chepesi tunasema, umejilipua.."
  "Sitaki kusikia upuuzi wako mjinga mkubwa wewe", alidakia Kayumba akimjibu mlinzi.
  "Kwenda zako huko, ukweli nimeshakwambia", mlinzi alifoka. Kayumba aliondoka mahali hapo akiwa ameinamisha uso wake chini mikono nyuma ilihali muda huo Catherine na Johnson  walicheza kwa kukimbizana, mahaba moto moto yalionekana huku kila mmoja akiwa na hamu na mwenzie. Na kabla wawili hao hawajaingia ndani, Catherine alizipiga hatua kumfuata mlinzi. Alipomfikia alisema "Mzee Masumbuko, siku nyingine usimruhusu huyu mbwa kuingia ndani ya nyumba hii. Mimi na yeye mkataba ulishamalizika sawa sawa?.."
  "Sawa bosi!",  aliitikia. Baada ya hayo Catherine alirudi kumkumbatia Johnson kisha wakaingia ndani.
    Jua tayari lilikuwa limezama, kwenye giza totoro anaonekana Kayumba akitembea huku hana hili wala lile. Mfukoni hakuwa na hata senti, sababu pesa aliyokuwa amebaki nayo kama akiba alimnunulia Catherine zawadi ya nguo ambayo nayo haikupokelewa. Kayumba alijikuta akijutia, neno laiti ningelijua halikuwa  chachu mdomoni mwake, kila mara alilitamka. Kitendo alichomfanyia Catherine aliona ni cha kinyama sana ambavyo hakutarajia kama Catherine angeliweza kumfanyia. Pumzi ndefu alishusha Kayumba, mikono aliweka kiunoni, macho yake nayo yalitazama kila pande la jiji. Aliona magari yakipishana, watembea kwa miguu nao wakirejea kurudi majumbani baada ya mihangaiko ya kutwa nzima. Alitikisa kichwa, akisikitika kisha akajisemea.
   "Naam! Dunia sasa imekuwa kigeugeu upande wangu. Catherine ameniachia kovu la milele moyoni mwangu. Laah! Amenifanya niwachukie wanawake ingawa najua pasipo hawa viumbe kamwe Dunia haitakuwa imekamirika. Lakini, mimi katika hili nitajitahidi kujizuia kupenda, nitaishia kutamani na sio kumuamini mwanamke kwa asilimia zote. Hatimaye usiku umeingia, Kayumba sielewi ni wapi nitaegesha ubavu wangu, ghafla nimekuwa kama kichaa. Eeh Mungu wangu nisaidie mimi ",alijisemea maneno hayo Kayumba huku akiwa amesimama kando ya barabara. Alikuwa mfano wa tiara, hakuwa na muelekeo. Ghafla mbele yake akaonekana kijana wa makamo akivuka barabara, Kayumba akavaa moyo wa ujasiri akamvagaa kijana huyo.
" Bro.. Bro.. Braza", aliita Kayumba. Kijana huyo aliyekuwa akivuka barabara aligeuka kutazama kule inapotokea sauti wakati huo huo Kayumba tayari alikuwa amemkaribia, alimsalimu. "Habari yako kaka"
"Njema tu za kwako", kijana huyo alimjibu Kayumba huku akimtazama kwa wasi wasi.
  "Kwangu pia njema. Ammmh! Kaka jina langu naitwa Kayumba. Naomba msaada wako tafadhali sina pakulala usiku huu, vile vile mimi mgeni hapa mjini, ndio leo nimefika. Sijui wapi pakuanzia wala pakuishia, nisaidie kaka nakuomba nipo chini ya miguu yako"
"Nikusaidieje? Na unawezaje kufunga safari ya kuja mjini pasipo kuwa na muelekeo? Halafu wewe hunijui wala mimi sikujui, haya itakuaje kama nikikupokea halafu ukanifia mikononi mwangu? Nitaanzia wapi kujieleza? Na je, unaniaminije mpaka ukathubutu kuvaa moyo wa ujasiri ukahitaji msaada wangu! Braza hapa mjini, mji huu unamambo mengi sana baadhi mchana watu ila usiku sio watu..", aliong'aka kijana huyo. Lakini mbali na kuongea maneno hayo kwa sauti ya ukali ila Kayumba aliendelea kumng'ang'ania amsaidie, wala hakujali,punde machozi yalimtoka wakati huo akishuka chini kumpiga magoti huku akiendelea kuomba msaada kwa mtu huyo asiyemfahamu, ni jambo ambalo limpelekea mtu huyo kuingiwa na huruma juu ya kile alichokionyesha Kayumba, hivyo alimshika mabega akamuinua kisha akasema.
 "Sawa nitakusaudia  kwa usiku huu, lakini kwanza yakupasa ukaze moyo na vile vile uwe jasiri na mtu mwenye siri "

   
    KWANINI KAYUMBA AMEAMBIWA HIVYO? TUKUTANE SEHEMU IJAYO ILI KUJUA KILICHO ENDELEA!





from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/39dn2Lx

No comments:

Post a Comment