-
"Ahahahaaaaa! Nacheka kwa madaha kwani furaha niliyo nayo moyoni siwezi kuelezea. Baada ya kiza cha muda mrefu, hatimaye napata kuona mwanga. Ama kweli Mungu mkubwa. Kayumba sasa nipo huru huku macho yangu yakitamani kumuona mpenzi wangu Catherine mwanamke nimpendae kwa dhati kutoka kati kati ya kiini cha moyo wangu. Kwa hakika jinsi nimpendavyo nipo tayari hata kufa kwa ajili yake, na ndio maana nilikubali kufungwa jela ili nifanikishe hitaji la moyo wake.. Catherine sasa mwanaume wa ndoto yako nipo huru, najua miaka saba ni mingi sana ukiwa hujanitia machoni, lakini leo hii narejea uraiani na bila shaka niliyokusisitiza uyafanye utakuwa umeyatekeleza ingawa waswahili husema kwamba mchumba hasomeshwi. A hahahahaaaa! Hapana sitaki kuamini maneno yao,bila shaka Kayumba nitakuwa mwanaume wa kwanza aliyethubutu kufanya jambo hilo. Naamini nitakuwa mfano wa kuigwa. Ahahahah hahahah". Maneno hayo Kayumba alikuwa akijisemea ndani ya nafsi yake wakati huo uso wake ukionyesha wingi wa tabasamu. Furaha isiyo kifani ilitamaraki kwa kijana Kayumba hasa baada kumaliza kifungo chake cha miaka saba aliyohukumiwa baada kukutwa na hatia ya kuiba mali ya mwananchi. Kayumba aliona dunia imebadirika sana, vitu vingi vimeongezeka na vingine vimeboreshwa. Lakini vyote hivyo havikumfanya kustaajabu sana bali akili yake sasa aliielekezea kwa Catherine mpenzi wake. Alijawa na shauku ya kutaka kumuona. Hatimaye alifika kijijini kwao. Sherehe na ndelemo vililindima, ndugu jamaa pamoja na marafiki walifurahia ujio wa ndugu yao. Mzee Masasa akaamuru mwanawe achinjiwe Jogoo mkubwa kuliko wote ndani ya wale aliowafuga,yote hayo ikiwa furaha isiyo kifani juu ya kijana wake aliyerejea uraiani. Jioni ya siku hiyo waliifanya kuwa sikukuu. Na siku iliyofuata, Kayumba alizunguka kijijini huku na kule. Alishangaa sana kuona kijiji chao kikiwa na mabadiriko, maendeleo mbali mbali yalimfanya Kayumba kuzidi kupigwa na bumbuwazi jambo ambalo lilimpelekea kujawa na tabasamu wakati wote. Moja kwa moja alifika nyumbani kwa rafiki yake wa karibu sana, rafiki ambaye walikuwa wakisaidiana kila jambo kabla hajafungwa jela. Aliitwa Fikiri. Fikiri hakuyaamini macho yake baada kumuona Kayumba. Kwa taharuki ya aina yake alisema "Kayumba? Niwewe ama ndoto?"
" Fikiri, hapana wala sio ndoto. Kayumba nipo huru ". Alijibu Kayumba huku uso wake ukionyesha tabasamu bashasha.
" Ebwanaeeh! Mungu mkubwa kaka "Aliongeza kusema Fikiri wakati huo akimlaki kiume na kisha akamsogezea kigoda. Kayumba aliketi kisha akaanza kumuuliza juu ya maisha yalivyokuwa wakati yeye yupo jela. Fikiri aliongea yote, maneno ambayo yalimfurahisha Kayumba lakini marafiki hao hawakuishia hapo, zaidi Kayumba aliuliza maendeleo ya Catherine.
"Catherine?.." Fikiri alishtuka.
"Ndio Mbona kama umeshtuka? Kuna nini rafiki yangu?.." Aliuliza kwa taharuki ya hali ya juu. Fikiri kabla hajasema jambo lililompekea kustuka, alishusha pumzi ndefu kwanza kisha akasema "Ndugu yangu Kayumba, ni kweli Catherine ulimpenda sana na yeye alikupenda vilivyo. Ila sasa baada wewe kuhukumiwa jela, Catherine alibadirika sana. Cathe aliyekuwa akikuaga kwa kilio na machozi siku ile ya hukumu, sio Cathe huyu wa sasa". Alijibu Fikiri.
"Bado Fikiri sikuelewi. Hivi unamaana gani kusema maneno hayo?.." Kayumba aliongeza kuhoji kwa mshangao huku macho yake yakimtazama Fikiri. Na kabla Fikiri hajaongeza neno lolote, Kayumba akaongeza kusema "Na je, unaweza kunisindikiza nyumbani kwao? Nikamuone.."
"Nyumbani? Catherine kwa sasa yupo Dar es salaam, baada ya masomo yake alipata ajira huko huko, kwahiyo kwa sasa hapa kijijini akija anakuja kusalimia tu.." Alijibu Fikiri. Kayumba alistushwa na jibu hilo, mara mapigo yake ya moyo yakamuenda mbio, huku hamu ya kumuona Catherine ikizidi kutamaraki katika fikra zake hali ambayo ilimfanya kupoa kidogo. Hali hiyo ilimuogopesha sana Fikiri na hapo ndipo aliposema "Kayumba, hupaswi kuumiza kichwa juu ya jambo hili. Kwanza mshukuru Mungu kwa sasa upo huru, na jambo la pili endapo kama unataka kumuona Catherine wako basi nipo tayari kukupatia maelekezo mahali pakumpata Jijini Dar es salaam. Mtaka cha uvunguni sharti ainame"
" Fikiri, nipo tayari kuinama ilimladi nikipate cha uvunguni. Sioni tabu kutoka hapa kuelekea Dar es salaam kumfuata Catherine.. Naomba unipe muongozo namna ya kumfikia, sipo tayari kumpoteza Catherine wangu ". Alisema Kayumba kwa hisia kali juu ya Catherine. Fikiri akainuka kwenye kigoda akaingia ndani, muda mchache baadae akatoka na karatasi iliyokuwa na maelezo ambayo yalielekeza wapi anapopatikana Catherine, akamkabidhi karatasi hiyo kisha akamwambia." Hii hapa ramani kaka, bila shaka huwezi kupotea hata iweje. Ramani hii alinipa siku moja alipokuja kutusabahi hapa kijijini, na leo hii ramani hii nakukabidhi wewe mshakaji wangu sababu nafahamu umuhimu wako kwa Catherine japo Catherine wa zamaani sio wa sasa "
"Nakushukuru sana Fikiri, wewe siku zote umekuwa bora sana. Na ndio maana hata nilipo kuwa jela nilikuwa nasali na kuomba ili siku moja niwe pamoja nawe uraiani. Fikiri kuna watu wanakwambia kwenda jela ni ujanja, bila shaka hao watu hawajawahi kuingia huko. Ujanja wakati kila kitu unapagiwa?.. "
" Ahahahah Hahaha "Fikiri aliangua kicheko mara baada kuyasikia maneno hayo ya Kayumba. Alipokwisha kukatisha kicheko chake akahoji" Mungu mkubwa ndugu yangu. Enhee nambie safari lini?..".
" Wiki ijayo, siku za hapa katikati nitakuwa katika harakati za kutafuta nauli na pia fedha ya kumnunulia Catherine japo vizawadi". Alijibu Kayumba kwa tabasamu bashasha.
"Sawa nakuombea ili ufanikiwe" Alikata kauli Fikiri, maongezi yao yakawa yamekomea hapo ambapo Kayumba alinyanyuka kutoka kwenye kigoda chake akaonda nyumbani hapo kwa rafiki yake aitwae Fikiri.
Ni dhahili shahili Kayumba alipania kumfuata Catherine jijini Dar es salaam,alitamani sana kukutana naye huku fikra zake zikiamini kuwa Catherine hatakama inasemekana kabadirika kamwe hawezi kumbadilikia na yeye. Fikra hizo zilimfanya Kayumba kucheka ndani ya moyo wake na kisha kujisemea " Itakuwa msimamo anaoonyesha Catherine wangu, ndio unao muhukumu kuwa kabadirika. Vijana wengi hupenda mwanamke anayrjirahisisha pindi aelezeapo hisia juu yao. Wakidiliki kabisa kusahau kuwa siku zote mwanamke imara huwa hajilengeshi. Bila shaka hii kitu ndio inayomfanya Catherine wangu kuhukumiwa kwa makosa hayo, nadhani hukumu yangu imemfanya aikumbuke ahadi yake aliyoniahidi siku ile ya hukumu yangu. Nami nasema Catherine baki na msimamo huo huo kwani tayari mwanaume wa ndoto zako nipo uraiani. Ahahahah hahaha " Alihitimisha kwa kicheko Kayumba mara alipokwisha kujesmea maneno hayo. Kamwe hakutaka kuamini kama Catherine kabadirika,na hivyo alingojea kwa shauku sana siku ya ile aliyopanga kumfuata Catherine iweze kutumia. Hatimaye siku ilikaribia. Aliwaeleza wazazi mzee Masasa na Bi Mitomingi juu ya safari ya kuelekea Dar es salaam kutafuta maisha na wala hakutaka kuwaambia ukweli kuwa anaenda Dar kumtafuta Catherine.
"Ni jambo jema sana mwanangu, ingawa mapema sana tangu utoke jela. Wazee wako tulihitaji uendelee kukaa nasi maana miaka saba si haba kijana wangu" Alisikika akisema hivyo mzee Masasa baba yake Kayumba. Muda huo ilikuwa yapata saa mbili usiku, usiku wa mbalamwezi wakiwa wameketi kando ya moto kwani msimu huo ulikuwa wa baridi kali,mahindi nayo waliyegeuza kwenye mafiga, zogo nalo likiufanya moto kukolezwa vilivyo.
"Lakini kwa kuwa umeamua kwenda kutafuta maisha, basi Mungu akutangulie kwa kila jambo mwanangu" Alidakia Bi Mitomingi mama Kayumba ambaye yeye muda huo alijitenga kando kidogo ya moto ingawa alionekana kujikunyata ndani ya blanketi. Kayumba alifurahishwa na namna wazazi wake walivyolipokea suala hilo,usiku huo huo alienda kumuaga Fikiri kisha kesho yake alfajiri safari ikaanza. Safari ya kuelekea Dar es salaam kumfuata Catherine mwanamke mpenzi wake ambaye alijitolea kumsomesha kwa udi na uvumba akihakikisha kuwa ndoto yake isiyeyuke.
Dar es salaam alifika mapema sana, hivyo kupita ramani aliyopewa iliweza kumuongoza mpaka mahali ilipo nyumba anayoishi Catherine. Ni nyumba nzuri sana, nyumba iliyopo Mikocheni B. Nyumba ambayo ilipendeza sana kwa kuitazama. Kayumba baada kugundua tayari kafika, alijitazama kwanza akaachia tabasamu wakati huo akiushika vema mfuko uliokuwa na zawadi aliyomeletea Catherine. Akazipiga hatua za pole pole kulisogelea geti, punde alibisha hodi geti likafunguliwa.
"Habari yako kaka" Kayumba alimsabahi mlinzi aliyefungua geti.
"Salama sema shida yako" Alijibu mlinzi huyo kwa sauti ya jazba. Kayumba akatabasam kidogo kisha akasema "Samahini naitwa Kayumba, bila shaka hapa ni nyumbani kwa Catherine.." Aliongeza kusema Kayumba.
"Catherine?.. Ndio nani huyo?.." Mlinzi alishtuka kulisikia jina hilo.
"Ndio, inamaana humfahamu?.."
"Ndio simfahamu, umepotea nyumba. Huyo Caselini wako mimi simjui unanipotezea muda bwana" Alijibu mlinzi na punde akataka kufunga geti lakini Kayumba alizuia huku akisisitiza kuwa nyumba hiyo ndio anayoishi Catherine,kitendo ambacho kilizua tafarani hapo getini. Lakini wakati tafarani hiyo ikiendelea mara Ilisikika sauti ikisema kwa jazba "We mzee Masumbuko! Vipi mbona sielewi kunanini hapo getini?.." Sauti hiyo ilisababisha tafarani hiyo kutulia wakati huo mlinzi akageuka kumuitika bosi wake. Hapo Kayumba anapata kumuona Catherine, tabasamu bashasha liloonekana usoni mwake na wala asiyaamini macho yake ilihali muda huo mzee Masumbuko akasema "Kuna mshamba hapa ananisumbua"
"Hebu mruhusu". Catherine aliamuru, amri ambayo mzee Masumbuko aliweza kuitii akamruhusu Kayumba aingie. Hakika Kayumba alifurahia sana, furaha aliyokuwa nayo moyoni mwake haikuwa na kipimo. Alizipiga hatua kumsogelea Catherine hali ya kuwa Catherine akionekana kusimama na wala asistushwe na ujio wake.
"Oooh! Malikia wa moyo wangu, Catherine mpenzi kipenzi changu nimerudi, Kayumba nipo huru sasa" Alisema Kayumba alipomkaribia Catherine.
"Mbona kama hufuraishwi na ujio wangu? Maana sioni ukionyesha hata tabasamu? Unataka kuniambia miaka saba yote hujanikumbuka?.." Aliongeza kusema Kayumba huku akimtazama Catherine uso kwa tabasamu bashasha ilihali Catherine akionyesha uso wa hasira. Mwisho akakohoa kidogo kisha akasema." Kayumba, naomba useme shida iliyokutoa kijijini ikakuleta nyumbani kwangu. Nina kazi nyingi za kufanya ndani sitaki unipotezee muda wangu". Kayumba alistushwa na maneno hayo ya Catherine. Akashusha pumzi kisha akasema "Hebu acha utani Catherine, basi twende ndani nikakusaidie kazi"
"Umsaidie nani? Nafasi pekee ambayo anaweza kunisaidia ni mpenzi wangu na sio wewe" Alijibu Catherine kwa sauti ya juu.
"Inamaana kwamba mimi sio mpenzi wako? Catherine umenisaliti?.." KWA sauti ya chini iliyojaa huzuni ndani yake aliuliza Kayumba. Hapo Catherine akacheka kwa dharau kisha akajibu "Ndivyo ilivyo Kayumba, asante kwa kunisomesha lakini kwa sasa nafasi yako imezibwa na mtu mwingine. Ulitegemea miaka yote saba niishi bila mwanaume? Ungelikuwa wewe ungeweza?"
"Sio rahisi hivyo Catherine", alisema Kayumba kwa msisitizo.
"Hupaswi kupingana na ukweli, kwa maana hiyo basi nakuomba utoke nyumbani kwangu haraka sana iwezekanavvyo...." alifoka Catherine huku mdomo ukimtetemeka kwa hasira ilihali maneno hayo yalimchanganya Kayumba, hakuamini kile alichokisikia akajihisi kukosa nguvu wakati huo huo machozi yakimtiririka machoni mwake. Kwa huzuni akasema" Kwanini Catherine umeamua kunifanyia unyama huu? Yote niliyokifanyia kama pendo langu kwako leo hii malipo yake ni haya? Umesahau kuwa wewe ndio sababu ya mimi kufungwa jela?.. Kwanini Catherine kwanini lakini? Kumbuka Catherine uliniahidi nini siku ile nahukumiwa jela, kumbuka Catherine kumbuka ", alisema Kayumba kwa uchungu huku machozi yakizidi kutiririka.
USIKOSE SEHEMU IJAYO. UTANIKUMBUKA TU!
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2J9OKyc
No comments:
Post a Comment