Sunday, March 22, 2020

UTANIKUMBUKA TU SEHEMU YA TATU-03



"Jina langu naitwa Edga, sijui mwenzangu wewe unaitwa nani", aliongea jamaa huyo aliyekuwa akiombwa msaada na Kayumba. Kayumba alijitambulisha kisha akaambatana na Edga mpaka maskani anapoishi. Kijana Edga hakuwa na nyumba, alilali nje pembezoni mwa frem za maduka.. Hakuwa peke yake bali walionekana vijana wengine. Hiyo hali ilimshtua sana Kayumba, na hapo ndipo alipokumbuka maneno yale aliyoambiwa na Edga, lakini wakati akiwa katika hali ya kustaajabu, Edga alimgeukia kisha akasema "Kayumba, awali unaniomba msaada nilikwambia kwamba yataka moyo. Mjini hapa mimi sina nyumba wala chumba,kwahiyo nilishindwa kukukatalia kwa sababu siwezi jua roho niliyonayo mimi kama na wenzangu wanayo. Haya sasa ndio maisha ninayo ishi, hawa wote unao waona ndio washkaji zangu shaka ondoa "
" Edga, mimi ni mwanaume. Nakabiriana na kila hali, kwahiyo kuhusu suala hili wewe ondoa hofu kabisa ", alijibu Kayumba huku akiachia tabasamu bashasha usoni mwake, wakati huo huo baadhi ya vijana kadhaa waliokuwa wamelala waliamka. Mmoja wao alisema."Muda wote mmsimama kulikoni?.."
"Ni mimi Edga, jamani tumepata mgeni. Anaitwa Kayumba. Huyu jamaa nimekutana naye njiani alikuwa hana dira, hajui anzie wapi wala aishie wapi..."
"Kwahiyo?..", Edga kabla hajamaliza kuongea alichotaka kusema, aliulizwa.
"Nimeamua kumsaidia ili awe moja ya familia yetu, wasaka tonge", alijibu Edga. Punde si punde mtu mwingine aliamka, kwa sauti kali akasema "Huu utaratibu wa wapi? Unawezaje kumsaidia mtu kihorera? Hapa mjini mbona Edga unakuwa kama wakuja? Unajifanya unaroho nzuri sana sindio! Usitufanye sisi wajinga, akili ya kuambiwa changanya na yako, hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kutoka kwao akaja mjini pasipo dira ", alifoka mtu huyo, aliitwa Boko. Kijana ambaye ni pande la mtu.
" Afadhali kiongozi utusaidie suala hili ", mtu mwingine aliunga mkono kile alichokiongea Boko. Roho Ilimuuma sana Kayumba, alijua fika yeye ndio chanzo chote cha mzozo huo,lakini hali ya ugeni wa jiji la Dar es salaam ilimlazimu kukaa kimya huku akimuomba Mungu Edga asije akapindua mawazo yake.  Baada ya zogo la hapa na pale, hatimaye Boko, kiongozi wa vijana hao wasaka tonge alitoa amri, kwa sauti kali akasema "Kayumba, huyo mtu wako mstiri kwa leo tu ila kesho ajue pakwenda aidha ikiwezekana uondoke naye"
"Sawa kaka hakuna shida", alijibu Edga kwa sauti ya chini kabisa kisha akamshika mkono akasonga naye mahali anapolaza mbavu zake. Alipofika alimkabidhi Kayumba box la kulalia, kisha yeye akaegemea ukuta akiwa amekaa tayari kwa safari ya kuutafuta usingizi.
   Ni suala ambalo upande wa Kayumba lilikuwa ngumu sana kuweza kupata lepe la usingizi, mawazo yake yote yalikuwa yakimfikiria Catherine. Alikumbuka maisha ya nyuma kabisa aliyokuwa akiishi naye, mpaka kufikia hatua ya kuthubu kumkana huku akidiriki kumtukana. Hakika roho ilimuuma sana, hasa akifikiria namna alivyokuwa akijitoa kwake kwa hali na mali kuhakikisha binti huyo anafikisha walau asilimia kadhaa ya ndoto zake. Baada kuwaza kwa muda mrefu, mwishowe alipitiwa na usingizi. Alilalia ila hata alipokuwa usingizini bado aliota ndoto kadhaa zilizomuhusu Catherine, moja ya ndoto aliyoota ni  kumuona Catherine akichukuwa uamuzi wa kujiuwa baada kuteswa na mapenzi.
  "Catherine.. Catherine", Kayumba akiwa kwenye dimbwi la njozi alilitaja jina la Catherine, na punde si punde alizinduka kutoka kwenye dimbwi hilo, akajikuta kuwa ilikuwa ndoto. Hakika alisikitika roho ilimuuma sana, machozi nayo hayakuwa mbali, yalimtiririka huku akililia moyoni. Lakini pindi alipokuwa katika hali hiyo, ghafla macho yake yalitazama kulia kwake,hatua kadhaa mbele alipata kuona kundi la vijana wakihesabu baadhi ya mali walizopora usiku wa siku hiyo. Alistuka Kayumba,na hapo ndipo alipojua kuwa amelala na watu ambao sio watu wema. Moyo wa woga ulimuingia, ikapelekea kumsahau Catherine kwa dakika kadhaa huku kijasho chembamba kikimtririka.
  "Hapa ni pasu kwa pasu wala hakuna zuruma", Kayumba alisikia sauti ya Boko ikitoa amri ilihari zoezi hilo la kugawana mali likiendelea, mali hizo ilikuwa ni simu na fedha kadhaa. Mara baada zoezi hilo kukamilika, Boko aliongeza kusema "Sasa ndugu zangu kuna jambo ambalo nataka kuwaeleza. Dhahiri shahili, tayari ndungu yetu ameshaanza kuleta uhuru wa manyani kwenye kikundi chetu. Kwa maana hiyo basi tunacho takiwa ni kumchukulia uamuzi mgumu kabla mipango yote haijakwenda kombo"
"Uamuzi gani huo!?..", aliuliza moja ya watu waliokuwa wakimsikiliza Boko kile anacho kisema.
"Mimi nafikiria tumfukuze mahali hapa", alijibu Boko wakati huo macho yake yakitazama kulia na kushoto, moyo wake ukiwa na wasi wasi kwani tukio walilotoka kufanya  muda mchache uliopita katu lisingeliweza kuuruhusu moyo wake kuwa na amani.  Kimya kidogo kilitawala mara baada Boko kuongea maneno hayo, lakini punde si punde kimya hicho kilitoweka mtu mwingine naye akatoa wazo lake, alisema "Kumfukuza huyu mtu sio suruhisho, kwa sababu ni kama tutakuwa tumempa nafasi ya kutuchafua huko alipo hata ikiwezekana kutochongea kwa jeshi la polisi. Kwahiyo cha kufanya ni kumuuwa tu", Kayumba alistuka kusikia maneno hayo ambayo Boko na watu wake walikuwa wakiyaongea. Ilikuwa ni njama ambayo walikuwa wakiipanga wakiamini kuwa hakuna anayewasikia.
"Safi sana", Boko aliunga mkono wazo hilo la kumuuwa Edga.
"Au mnaonaje?..", aliuliza Boko.
"Hakuna tabu"
"Hakuna shaka"
"Ndivyo kabisa", walisikika kwa sauti tofauti tofauti vijana hao wakiunga mkono suala la kumuua Edga.

   Kesho yake alfajiri, Edga alimuamsha Kayumba kwa dhumuni la kumuga akitaka kuelekea kwenye mihangaiko yake ya kila siku.
"Kayumba Kayumba", aliita Edga. Kayumba alikurupuka kutoka usingizini.
"Abwanaee! Kumekucha sasa. Mimi naingia mtaani kusaka tonge", alisema Edga wakati huo akiwa amesimama. Kayumba alinyanyuka akajinyooshea kisha akajibu "Sawa braza. Lakini bado nahitaji msaada wako kaka!.."
"Msaada gani sasa? Inamaana hujaona kama tayari umeniponza?Kayumba umeshavuruga kambi ninacho kuomba fuata ustarabu wako", alifoka Edga.
"Tazama kila mmoja ameshaondoka kuelekea katika mihangaiko yake, mimi tu ndio nimebaki. Kosa langu kukutaarufu kuwa natoka? Na jana situlikubaliana kuwa leo utajua ustarabu wako? Haya nini tena unataka kutoka kwangu!..", aliongeza kusema Edga. Maneno hayo aliyaongea huku akimtazama Kayumba kwa macho ya hasira kiasi kwamba ilimpelekea Kayumba kuwa mnyonge maradufu. Na alipokwisha kumwambia maneno hayo, alizipiga hatua kuondoka zake huku Kayumba akiishia kumtazama  tu,moyo wake nao ukimshawishi amwambie Edga juu ya kile alichokisikia usiku wa jana. Ndipo kwa sauti ya upole Kayumba alipasa sauti kumuita Edga, kijana Edga hakugeuka mpaka pale alipoitwa zaidi ya mara mbili "Unasemaje?..", aliuliza Edga mara baada kumgeukia Kayumba.  Kwa masikitiko, Kayumba akasema "Ahsante sana kwa msaada wako kijana mwenzangu, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo kama nitashindwa kukueleza kile kinachoendelea nyuma ya pazia",alisema Kayumba, maneno ambayo yalimstua sana Edga hima alimsogelea Kayumba kisha akamuuliza "Unamaana gani kusema maneno hayo?.."
"Edga, kifo kipo mkononi mwako. Jamaa zako wamepanga wakuuwe,mipango yao waliipanga usiku walipotoka kazini wakati huo ulikuwa umelala. Tafadhali usipuuze", alijibu Kayumba, kisha akayafuta machozi yake. Roho ilimuuma sana, aliamini kuwa huwenda Edga akawa msaada wake katika jiji hilo la Dar es salaam,jji ambalo limejaza kila aina ya maisha. Lakini pia mbali na suala hilo, maumivu ya kile alichokumbana nacho kutoka kwa Catherine bado yaliutesa sana moyo wake hali iliyopelekea kutokwa na machozi. Na wakati Kayumba akiwa katika hali hiyo ya majonzi, upande wa Edga alionekana kuduwazwa na maneno ya Kayumba. Alishusha pumzi ndefu, akainua uso wake kutazama juu. Akakumbuka.
           **********

"Edga, kuna dili lipo mbele yetu. Unatakiwa ukachukue nyaraka kwenye nyumba ya Mr Omon. Hili ni dili kubwa sana, na sisi tumekuteua wewe ili ulikamilishe..", alisikika akisema Boko kiongozi wa kundi,maneno hayo alikuwa akimwambia Edga.
"Hii nyumba ngumu sana, kuingia na kutoka pia. Hivyo basi umakini unahitajika ili dili hili liweze kulikamilisha. Kila sehemu kuna ilinzi, tena ulizi madhubuti", aliongeza kusema. 
"Lakini nitawezaje wakati mimi bado mgeni katika mambo haya? Ni heri tungeshirikiana hata wawili braza", alijibu Edga kwa sauti ya woga. Boko alikasirika kusikia maneno hayo, alimtazama  kwa hasira kisha akasema "Usinipangie kazi, unataka kusema miezi hii mitatu uliyojiunga nasi bado hujazoea? Hiki ni kipimo cha maisha, na kuishi ni kuchagua siku zote ukitaka kuruka sharti uagane na nyonga".
"Hapana bro, kwa hilo sipo tayari", alikacha Edga, akikataa agizo la kiongozi wake, kitendo ambacho kilimkera sana Boko. Na tangu siku hiyo maelewano baina yake na yao yakawa ya kususua huku kwa mara kadhaa wakimtenga kwenye ufanyaji wao wa kazi.
   Alishusha pumzi Edga baada kuyakumbuka hayo, alitikisa kichwa ishara ya kukubali jambo fulani wakati huo huo akaikumbuka na ile ndoto ambayo aliota akizikwa mzima mzima huku muhusika mkuu katika ndoto hiyo akiwa Boko ambaye alishirikiana na watu ambao hakuwafahamu. Mapigo ya moyo wake yalimuenda mbio, kijasho chembamba kilimtoka. Na hapo ndipo alipoamini kuwa kweli kifo u mkononi mwake wakati wowote, na hivyo hana budi kumfukuza Kayumba. Aliona ni heri aungane naye wakajenge maskani nyingine wakiwa pamoja, alihisi Kayumba ni zaidi ya ndugu na hivyo alimkimbilia ili amuombe msamaha huwenda akawa mkosefu juu yake.
"Braza..braza..braza", Edga alipasa sauti kumuita Kayumba huku akimkibilia, lakini Kayumba hakugeuka na wala sauti hiyo hakuweza kuisikia,mawazo yake yote alikuwa akimuwaza Catherine mwanamke wa ndoto yake aliyempenda kwa dhati ambapo alidiriki kumsomesha akiamini kuwa hiyo ndio zawadi pekee anayostahiri. Ila wakati Kayumba akiwa kwenye dimbwi hilo la mawazo, punde alizinduka baada kuguswa bega. Alisimama kisha akageuka nyuma ghafla ilimuona Edga.
  "Samahani sana Braza Kayumba,naomba usiondoke ", Aliongea Edga huku akitaharuki kumuona Kayumba uso wake ukiwa umechoshwa na machozi, aliamini kuwa huwenda kitendo cha kumtaka aondoke maskani kwao ndicho kimempelekea amwage machozi na hata asijue kuwa Kayumba anasiri nzito ndani ya moyo wake. Hivyo pumzi alishusha Kayumba mara baada kuyasikia maneno hayo ya Edga,kisha akasema "Edga..Edga..moyo wangu unaumia macho yangu yanavuja machozi juu ya yale maumivu ninayo yahisi. Kayumba najiuliza nimemkosea nini Mungu. Lakini Kuna wakati najiona mimi ni fungua la kukosa, sina budi kukubaliana na kila hali. Ahsante sana kwa msaada wako braza sasa acha nikafie mbele ya safari",alisema kwa uchungu  Kayumba huku machozi yakimbubujika mikono nyuma uso akiwa ameinamisha chini aliondoka zake!

      ITAENDELEA..





from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/39eWGbQ

No comments:

Post a Comment