Sunday, March 22, 2020

UTANIKUMBUKA TU SEHEMU YA SITA-06




Aliachia tabasamu pana Kayumba, dhahiri shahili maneno ya Edga yalimfariji vilivyo. Na wakati akiwa kwenye hali hiyo ya tabasamu, Edga aliongeza kusema. "Kazi ndio kila kitu, wewe ni zaidi ya ndugu sasa Kayumba kwahiyo sipo tayari kuona moyo wako unasononeka. Vile vile kama ulikuwa hujui, mwenzio nafikiria kukutafutia kazi nyingine. Kazi ya kubeba mizigo naona ni adhabu kwako".
"Ahahahah, ni kweli kabisa ila usipate tabu bwana. Hakuna kazi rahisi hapa chini ya jua", alijibu Kayumba akitanguliza kicheko.
"Hivi kuendesha mkokoteni unaweza?..", aliuliza Edga.
"Ndio naweza", Kayumba alijibu kishujaa.
"Basi naomba kesho twende sehemu, kuna mchongo nataka nikuunganishe nao. Natumai utafurahi sana", aliongeza kusema Edga.
"Naam! Kweli wewe mtoto wa mjini, maana unamipango zaidi ya raisi wa Marekani bwana Barack Obama", alisifia Kayumba wakati huo macho yake yakiitazma mahali pakulaza mbavu zake. Muda huo ilikuwa yapata saa saba usiku, hivyo basi hawakuwa na lazida walilala kwa dhumuni la kesho panapo MAJALIWA yake Mungu kukuche waende kusaka tonge. Usiku huo ulikuwa mzuri sana kwa kijana Kayumba, aliyatuliza vilivyo mawazo yake kwa kuwaza mstakabali wa kuisaka shilingi, zoezi hilo halikuchukuwa muda mrefu sana mwishowe usingizi ulimpitia. Kesho yake alfajiri na mapema alikurupuka kutoka usingizini baada Edga kumuamsha. "Ahahahah hahahahah", Edga aliangua kicheko. Alipokatisha kicheko chake akasema "Yani huwezi amini Kayumba, ukiamshwa kutoka usingizini unaonekana mbaya. Uso mkavu kama gurudumu la trekta", alitani. Kayumba aliachia tabasamu huku akiyafikinya macho yake, alipohakikusha kuwa sasa yanaona vizuri alimuuliza muda Edga. "Hivi itakuwa saa ngapi muda huu?.."
"Sina saa ila nafikiri saa kumi na moja na dakika zake, kumekucha. Sasa twende huko nilikokwambia". Edga na Kayumba walianza safari. Walifika sehemu hiyo husika, ilionekana mikokoteni mingi sana. Wawili hao bado walivuta hatua zao, kuuacha mkokoteni moja baada ya mwingine huku macho yao yakiiangalia. "Karibuni..", alisikika mtu mmoja akiongea. Mtu huyo alikuwa amesimama kando huku mkononi akiwa ameshika daftari ndogo. Mtu huyo alikuwa akikodisha mikokoteni na kuuza pia.
"Tunaangalia upi unatufaa", alijibu Edga.
"Mnanunua au mnakodi?..", aliuliza bwana huyo.
"Hapana tunakodi..", Kayumba alijibu, punde si punde macho yake yaligota kwenye mkokoteni ambao alivutiwa nao.
"Huu unatufaa sana", alisema Kayumba. Ndipo muhusika alimsogelea na kisha kukamilisha taratibu stahiki.
"Hiki ni kitendo kikubwa mno cha mkokoteni hapa mjini, kwa maana hiyo basi uaminifu ndio nguzo pekee ya kufikia malengo yako. Na ndio maana jambo la kwanza tunalo zingatia ni kufahamu kituo chako maalumu unachofanyia kazi, na mengine kadha wa kadha tuliyoorodhesha hapa kwenye daftari letu tu. Kazi njema ".
" Shaka ondoa ndugu yangu ", alisema Edga wakati huo akihesabu fedha na kisha akamkabidhi mtu huyo.   Zoezi hilo lilipokamalika, waliondoka mbali na eneo hilo. Walienda nje kidogo ya jiji, huko palikuwa na minazi mingi mno. Vijana mbali mbali walioonekana kuwa na mikokoteni wengine baiskeli walikuwa shap kulangua madafu,fujo za hapa na pale zilisikika huku Lugha mbali mbali za maudhui nazo zikitamba achilia mbali utani kadha wa kadha kuhusu soka na siasa.
"Penye wengi kuna mengi bwana", alisikika mzee moja akisema maneno huku macho yake yakitazama namna vijana waliyokuwa wakichakarika,wakati huo huo Edga aliingiza mkono mfukoni akachomoa kiasi kadhaa cha fedha akamgeukia Kayumba kisha akasema "Kayumba, kama nilivyokwisha kukueleza hapo awali rafiki yangu. Sisi ni wasaka tonge, kwa maana hiyo basi lazima tupange mipango madhuti jinsi ya kusaka pesa. Asikwambie mtu braza heshima pesa, shkamoo kelele. Nina imani kabisa tutafanikiwa.. Hii fedha tuliyoweka, nimeona bora tununue madafu ukayauze mtaani wakati huo mimi naendelea na kazi yangu ya kubeba mizigo ".
" Wazo nzuri sana rafiki yangu, ila nisingependa uendelee kuifanya ile kazi. Kaka utavunjika mgongo angalia kijana ujue!?.. ", alisema Kayumba akimuasa Edga.
" Ahahahaha hahahaha ", Edga aliangua kicheko. Alipokihitimisha akasema." Mwanzo mgumu, acha nipambane najua Mungu u karibu nami. Na sasa tusogee  ili tuchukue mzigo ukaanze kazi. Ammmh! Siku ya leo nitatembea na wewe  ukariri maeneo ili kesho na hata siku nyingine usipate shida".
  "Sawa". Edga akiwa sambamba na Kayumba walijongea kununua mzigo wa madafu. Zoezi hilo halikuchukuwa muda mrefu, na sasa wakaanza safari ya kurejea jijini huku wakikokota mikokoteni wenye madafu. Siku hiyo walizulula karibu Wiliya yote ya Ilala na viunga vyake, mnao saa kumi na mbili mzigo wote ulikuwa umekwisha. Hakika walifurahi sana, maswahiba hao walishangilia kwa kuruka ruka huku wakitembea miondoko ya kunyata ikiwa ishara ya masihara. Watembea kwa miguu waliwashangaa sana, achilia mbali abiria waliokuwemo ndani ya daladala na wale waliokuwemo ndani ya magari yao binafsi. Wote macho yao yalisonga kwa vijana hao wasaka tonge, Kayumba na mwenzake Edga ambao wote kwa pamoja walishindwa kuzizuia hisia zao za furaha mara tu walipomaliza mzigo.
  "Hii kazi inakufaa sana rafiki yangu Kayumba, hesabu zetu zimegonga pale pale. Nilikwambia mzigo huu ukiisha tutakuwa na faida kubwa, tazama sasa mtu wangu. Ahahahah hahahahah",alisema Edga huku akiwa na furaha isiyo kifani. Fedha walizopata siku hiyo si haba kwa maisha yao ya kulala nje, walirizika nayo jambo ambalo liliwapelekea kuanza kupanga mikakati ya kununua mkokoteni wa kwao ili kuepukana na adha ya kukodi.
   "Hilo wazo nzuri sana", Edga alimuunga mkono Kayumba ambaye alitoka wazo la kununua mkokoteni wao.
"Kwa sababu endapo kama tutafanya hivyo itatuwea rahisi kupanga chumba chetu na maisha yakaendelea..", aliongeza wazo Kayumba. Hakika ni mawazo chanya ambayo yalimfanya Edga kuachia tabasamu na kisha akasema "Unasikia Kayumba? Kauli yetu nikisema wasaka, wewe unaitikia tongeeee, tunarudia mara mbili baada ya hapo sasa tunatishiana kwa kurushiana ngumi. Yani nikipiga juu wewe unainama, ngumi inapita halafu unajibu mashambulizi  vile vile na mimi naikwepa"
"Ahahahah.. Hahahahah", Kayumba alicheka. Na hayo yote Edga aliyafanya kwa jitihada ili Kayumba apate kumsahau Catherine, binti aliyemuachia kovu la mapenzi kwa kumtakataa kuwa hana elimu alidiriki kusahau kuwa elimu hiyo anayojivunia alisomeshwa na nguvu Kayumba. Mpango huo kwa asilimia kadhaa ulikwenda vema, Kayumba wakati wote alionyesha kufurahia maisha.
    Siku  iliyofuata alikwenda peke yake. Alinunua mzigo na kisha kwenda kuuza, ajabu siku hiyo alimaliza mapema. Saa tisa alasiri alirejea maskani hali ya kuwa jioni saa kumi na mbili Edga naye alirudi. Alishangaa sana kumkuta Kayumba, kwa sauti ya juu akacheka sana kisha akasema "Wasaka.."
"Tongee..", aliitikia Kayumba, maneno ambayo wawili hao waliyarudia mara mbili mbili na punde si punde wakaanza kurushiana ngumi na kuzikwepa. Baada ya hapo waligongeana tano kisha wakaketi na kuanza kupeana pole ya mihangaiko ya kutwa nzima.
"Kazi inakwenda vizuri sana braza.. Lakini pia habari njema ni kamba kichwa changu kwa sasa hakimfikirii tena Catherine.."
"Kayumba? Unasema kweli?..", Edga alitaharuki baada kuyasikia maneno hayo aliyoyasema Kayumba. Alimtazama kwa mshangao, wala asiyaamini masikio yake.
"Hahahah, hebu rudia tena unasema Catherine?..", alihoji Edga kwa tabasamu bashasha.  Kayumba aliongeza kusema "Ukweli ni kwamba kichwa changu kwa sasa hakimfikirii tena Catherine"
"Oyoooooh! Vizuri sana", alishangilia Edga, kisha akasema "Amini kwamba  na wewe una moyo na sio jiwe,kwahiyo ipo siku atajua thamani yako kwake. Na ndio utajua kuwa wewe ni mstahili juu yake. Kayumba kutesa  kwa zamu, nakuhakikishia ipo siku atakumbuka kuwa wewe uikuwa mtu sahihi kwake,wakati huo wewe huna tena hisia juu yake. Sababu yule aliyebadilisha mikate mitano ikashibisha maelfu ya watu,na ndio yule aliebadilisha maji kuwa divai. Basi huyo huyo anaweza kuubadilisha moyo wake kukuhitaji wewe. Na hapo ndipo Catherine atakapojua utofauti kati ya mimba na ujauzito.", alisema Edga, maneno ambayo  yalimfanya Kayumba kuachia tabasamu.

       - - - - - USIKOSE SEHEMU IJAYO------







from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/39azJXw

No comments:

Post a Comment