Sunday, March 22, 2020

RIWAYA:UTANIKUMBUKA TU SEHEMU YA TISA-09





Kayumba alibaki na taharuki, alihisi huwenda amsekia vibaya kile alichokiongea Najrat. Lakini yote kwa alishusha pumzi akarejea kwenye kwama lake, akaendelea na mihangaiko ya kusaka shilingi. Mnamo sana kumi na mbili jioni, mzigo ulikuwa umekwisha. Kayumba alirejea maskani, punde si punde Edga naye alifika na baada ya kusalimiana Kayumba akasema "Leo mambo yamekwenda kama yalivyo pangwa"
"Ahahahah hahahaha", Edga aliangua kicheko kisha akahoji "Kwanini umesema hivyo, sijakuelewa ujue?.."
"Najua huwezi kunielewa lakini maana yangu ndogo sana, Edga mzigo umekwisha", alijibu Kayumba kwa furaha. Wawili hao walicheka sana, baada ya vicheko hivyo Edaga akasema "Kweli waliosema siku njema huonekana asubuhi wala hawajakosea,braza leo magari ya mzigo yamekuwa mengi mno  kiasi kwamba tulibagua bosi yupi mwenye mtonyo wa kutosha. Kwahiyo hapa nilipo pochi imetuna"
"Ahahahah", Kayumba aliangua kicheko kwa mara nyingine tena kisha akaongeza kusema "Tukiachana na hayo, nina habari njema nyingine..."
"Ipi hiyo?..", alihoji Edga wakati huo akiwa makini kumsikiliza Kayumba. Kayumba akajibu "Nadhani unakumbuka niliwahi kukwambia kwamba kuna binti nilimsaidia baada kuporwa mkoba wake"
"Ndio nakumbuka"
"Enhee.. Basi leo wakati napamabana na mkokoteni wangu, nipo hoi jasho mpaka kwenye kisigino jua kali, mara ghafla nikasikia bleki ya gari mbele yangu, nikainua uso nikaiona Noah nyeusi. Unajua mimi nikiwa kazini huwa sipendi dharau, kwa hasira nikamfuata dereva wa ile gari ili nimpe makavu, lakini braza mwili wangu ulijikuta ukinyong'onyea baada dereva kushusha kioo uso kwa uso nikamuona yule mrembo huku akiachia sabasamu. Tuliongea mengi sana ila alicho nishangaza ni baada kununua dafu akatoa noti ya shilingi elfu kumi halafu akakata chenji, na mwishowe wakati anaondoka akaniambia kwamba ametokea kunipenda ", aliongea Kayumba.
" Kweli!?.. ", kwa taharuki ya aina yake Edga alimuuliza Kayumba.
" Basi ndugu yangu hupaswi kulemba mwandiko kwa mrembo huyo wa kiarabu, na ndio maana nilikwambia kwamba wewe unanyota ya utajiri. Kwa maana hiyo basi usijipendekeze kwake, vuta subira kama amekupenda atakutafuta kwa udi na uvumba..."
"Lakini Edga mimi kwa sasa nayaogopa sana mapenzi, sitaki tena kulia kisa mapenzi"
"Kayumba rafiki yangu, naomba unielewe, anayekupenda kwa dhati katu hatapenda kukuona unalia.
" Sawa, hebu tuachane na hayo. Leo pesa ipo mshkaji wangu kwahiyo twende tukale chakula cha nguvu.."
"Hilo tu ndilo lililobakia.." aliongea kwa furaha Edga. Hayo ndio yakawa maisha ya vijana hao, Kayumba na Edga. Maisha ya furaha sana ingawaje waliishi kwa nguvu na kula kwa utepe ila kwa furaha haikuweza kukauka. Walifanya kila jitihada kuhakikisha furaha haipotei kwenye nyuso zao, kwenye magumu walitiana moyo na kwenye furaha walifurahi zaidi. Naam! Hao ndio wasaka tonge.
  Siku zilisonga, Kayumba hakubahatika tena kukutana na mrembo Najrat. Hakuliwazia sana suala hilo sababu alimchukulia Najrat kama mpita njia na sio vinginevyo, hivyo Kayumba alifanya kazi kwa juhudi zake zote. Hatimaye alisahau kama aliwahi kukutana na Najrat, lakini siku moja alipokea karatasi kutoka kwa kijana mmoja ambaye alifahamu kutokana na kazi anayoifanya. Kijana huyo alikuwa muuza duka, ambapo wakati Kayumba akakikokota kwama lake alisikia sauti ikimuita, haraka sana alitii wito.
"Habari yako bwana mkubwa".
"Salama tu vipi kwema?..", alijibu Kayumba.
"Kwema, naona unapambana". Aliongeza kusema kijana huyo muuza duka.
"Naam! Nautafuta utajiri." Kayumba alijibu huku akijifuta jasho usoni kwa flana yake.
"Vizuri, kuna ujumbe wako hapa nimeachiwa. Na kibaya zaidi aliyeniachia hakutaka nikutajie jina", alisema kijana huyo huku akimkabidhi Kayumba kipande kidogo cha karatasi. Kayumba alipokea karatasi hiyo, akiwa na shauku ya kutaka kujua kilichoandikwa aliifungua.
"Mambo Kayumba, naomba kesho saa nne asubauhi tukutane Seline Hotel nina maongezi zaidi ya kuzungumza na wewe, nakutakia kazi njema mpenzi", Kayumba alisoma kile kilichoandikwa kwenye karatasi hiyo. Ghafla akajikuta akiachia tabasamu wakati huo akiitazama mara mbili mbili hiyo karatasi.
"Sawa ahsante bwana", alimshukuru  huyo kijana aliyempatia karatasi, na sasa alizipiga hatua kurudi kwenye mkokoteni wake. Lakini kabla hajapiga hatua mbili, alisikia sauti ya kijana huyo ikisema "Chukuwa hii fedha", Kayumba aliposikia maneno hayo aligeuka akakutana na mkono wa huyo kijana ukiwa umeshika fedha,na kabla hajazipokea alihoji "Za nini hizo?.."
"Aliyeacha huo ujumbe ameniambia nikukabidhi", alijibu kijana huyo. Kayumba alipigwa na butwa. Alistaajabu sana kila akitazama kiasi hicho cha fedha, zilikuwa fedha nyingi mno. Alizipokea kisha akarudi kwenye mkokoteni wake akaendelea na kazi huku akiahidi kufika Seline Hotel pasipo kuchelewa. Jioni aliporejea maskani, alikuwa ni mtu mwenye wingi wa furaha. Hata pia alipomueleza Edga, naye pia alifurahi zaidi.
"Nilikwambia mimi, amini ndugu yangu siku zote Mungu hamtupi mja wake...", alisema Edga kwa furaha.
  "Hakika nimeamini, na kuanzia sasa naweza kusema maisha ya kulala nje baaasi. Hii laki tatu aliyonipa huyu mrembo, inatosha kupanga chumba na chenji inarudi. Naomba unipe ramani mahali ilipo hiyo Hotel ili wakati mimi naelekea huko, wewe ubaki unatafuta chumba ", alisisitiza Kayumba.
" Hahaha ah.. Wasaka.. "
" Tongeeeee ", walitaniana kama ilivyo ada. Na pindi furaha ikiwa imatamaraki kwa wasaka tonge hao, upande wa pili Catherine alionekana kukosa furaha. Usiku huo hakupata usingizi, aliona Dunia inamtenga hasa hasa kila alipoitazama picha kubwa iliyokuwa ukutani. Picha ya kijana msomi mwenzie atwae Johnson. Catherine kitanda alikiona kidogo, kila mara alikuwa akijipundua huku na kule huku nafsi yake ikiwa imefura giza la maumivu ya kusalitiwa na Johnson mwanaume aliyempenda kwa dhati na kuthubutu kumkana Kayumba.
"Johnson wa kunifanyia mimi hivi? Johnson kweli amedhutu kunidhihaki kiasi hiki? Mbona hakuniambia kama anampenzi mwingine! Nakuchukia sana Johnson sikupendi tena", alijisemea Catherine na punde akaangua kilio. Tangu awali hakujua ya kuwa Johnson ni mwanaume asiye dumu na mwanamke mmoja,kijana huyo alipendelea sana kuwachezea mabinti na kuwaacha kwenye mataa. Catherine akajikuta akiingia kwenye mkumbo huo wa wale mabinti wanaotumia na kuachwa, sasa anaachiwa maumivu makali ya usaliti. Jambo hilo linamfanya anamkumbuka Kayumba, aliona ni heri arudishe hisia zake kwa Kayumba akiamini kuwa huwenda akapata faraja ya moyo wake pasipo kujua kuwa Kayumba ameshamsahau.
"No! Lazima nimfuate Kayumba wangu kijijini, nitamuomba radhi kwa kile nilichomtendea",alijisemea Catherine huku akipandisha kwikwi baada kulia kwa muda mrefu. Lakini wakati Catherine akiwaza suala hilo la kumfuata Kayumba, upande wa pili hivyo hivyo Najrat alionekana kukosa usingizi. Mawazo yake yote alimuwaza Kayumba huku akitamani pawahi kukukucha ili aweze kuonana naye kama alivyomuasa.
Siku iliyofuata ilikuwa siku nzuri sana, hali ya hewa ilionekana kuwa shwari kabisa. Kayumba na Edga waliamka, mabox yao wakayahifadhi pema tayari kwa safari ya kuelekea kufanya kile walichokipanga usiku wa jana.
 "Kama nilivyo kwambia, sio mbali saana ila nina imani utafika tu", alisema Edga huku akijinyoosha.
"Hilo ondoa shaka, jitahidi upate chumba kizuri", alijibu Kayumba.
"Ahahhah hahahahah", Edga aliangua kicheko, alipokatisha kicheko chake akatania kwa kusema  "Usijali mume wa Najrat",
"Hahahahah..", Kayumba alifurahia utani huo wa Edga. Ndio maisha waliyokuwa wakiishi, na hivyo sasa alianza safari kuelekea Soline Hotel akitii wito la mrembo Najrat huku asijue mrembo huyo anakipi hasa anataka kumueleza. Hatimaye alikaribia kufika,kwa mbali aliliona gholofa la Hotel hiyo ambapo ingemlazimu kuvuka barabara ili aelekee upande wa pili mahali ilipo hiyo Hotel. Lakini wakati  anavuka barabara kuelekea upende wa pili, ghafla aligongwa na gari.

            Itaendelea...







from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2WB9BlW

No comments:

Post a Comment