Sunday, March 22, 2020
RIWAYA:UTANIKUMBUKA TU SEHEMU YA NANE-08
Ghafla Edga akaingiwa na wazo, aliona hana cha kupoteza zaidi ya kuchukuwa fedha hizo ili apate nauli ya kuelekea Dar es salaam kumtafuta dada yake. Akiwa na wingi wa hofu, alizichukuwa fedha hizo na wala hakutaka hata kuzihesabu hima alirejea sebuleni moja kwa moja akatoka ndani ambapo nje alikutana na mlinzi.
"We vipi, kwema huko?..", aliuliza mlinzi akimtilia shaka Edga ambaye kwa wakati huo alionekana kuwa na hofu.
"Hapana..hakuna hakuna tatizo babu", alijibu Edga kwa sauti ya woga wakati huo akifungua geti, alifunga kisha akatimua mbio kuelekea stendi ya mabasi. Alilala hapo hapo stendi, kesho yake alfajiri alipanda basi liendalo Dar es salaam. Alishusha pumzi Edga, hakuamini kama ameponyoka salama kwenye msala huo mzito wa kuiba fedha. Safari sio kifo, salama wa salimini Edga aliwasiri jijini saa ya jioni. Hakujua aeleke wapi, mpaka jua linazama Edga alikuwa bado hajajua muelekeo wake na hivyo ilimlazimu alale kwenye jumba la abiria. Lakini kesho yake asubuhi alistuka kujikuta mfukoni amebakia na shilingi elfu mbili tu kati ya fedha zote alizoiba, Edga alihaha kuzitafuta mfukoni pasipo kufanikiwa kuziona.
"Laah! Tayari wajanja wameondoka nazo", alijisemea baada kuzikosa, na hapo ndipo alipoanza kuwaza namna gani ataishi mjini pasipo kuwa na dira. Akiwa katika hali hiyo ya sintofahamu, ghafla alisikia sauti ikisema "Wale wa Kariakoo panda juu ukazibe, Kariakoo siti zipo za kumwaga. Mjini kariakoo twendeni", ilikuwa sauti ya kondakta akipiga debe. Edga alichomoa mfukoni shilingi elfu mbili aliyoasalia nayo kisha akazipiga hatua kuisogelea ile daladala.
"Konda, nauli bei gani?..", aliuliza Edga mara baada kumkaribia kondakta.
"Mia mia tatu, panda tuondoke", alijibu konda. Haraka sana Edga aliingia ndani ya dala hiyo punde safari ikaanza. Aliposhuka, alishangaa sana kuona majengo marefu huku wingi wa watu nao ukimuacha mdomo wazi. Jioni ilipoingia, alijikuta akitaharuki kuona watu wakilala nje ndipo naye hakuwa na budi kuungana na hao watu walalao nje. Hayo ndiyo yakawa maisha ya Edga ndani ya jiji, yalikuwa maisha magumu sana ambayo yalimpelekea kushindwa kufanya kile kilicho mleta jijini badala yake akajikuta akisaka sarafu ili apate mkate wa kila siku.
Maisha hayo yalikuwa endelevu mpaka anafikisha miaka kumi na tisa, alitegemea kuishi kwa kamali. Mchezo ambao ulimpa umaarufu mkubwa kwa wahuni wenzake, aliitwa Master. Jina ambalo alibatizwa baada kuonekana bingwa wa kuwala wenzake kwenye mchezo huo uliofahamika kwa jina karata tatu. Siku moja Edga akiwa na vijana wenzake wakicheza kamali kwenye moja ya uchochoro, ghafla waliona gari ndogo aina ya Rav4 limesimama. Punde si punde ndani ya gari hilo walishuka wanaume wawili wakiwa wamevalia makoti maeusi na miwani meusi pia. Edga na kundi lake walistuka, amri ikatoka kwa watu wale wawili "Hapo hapo malipo mikono juu", walisema wakati huo tayari wakiwa wamechomoa bastora.
"Chuchumaa chini", waliongeza kusema kwa amri baada kuwafikia. Hofu iliwatanda vijana hao wakiamini kuwa wamevamiwa na jeshi la polisi, lakini wakati wapo kwenye hofu hiyo mtu mmoja kati ya wale wawili aliangua kicheko kisha akasema "Acheni woga nyie watoto wa mama, yani koti kubwa na miwani mnatishika?.."
"Aaah sio poa mkuu, au wewe huoni kama mishe zetu hizi tunaishi kama kunguru?.." alisema Edga.
"Kweli kabisa wasi wasi mwingi", aliunga mkono mtu wa pili.
"Wasi wasi ndio akili ma-braza, acheni kukaa kiboya. Hebu tuachane na hayo kwanza,kuna habari njema nimewaletea. Lakini nataka kujua mko tayari?.."
"Habari gani hiyo?..", Edga alihoji.
"Hapa sio sio sehemu sahihi ya kuzungumza, aliyetayari twende".aliongeza kusema mtu huyo aliyevalia koti jeusi. Edga na wenzake walikaa kimya huku kila mmoja ndani ya ubongo wake akijishauri,jambo ambalo liliweza kuzua ukimya. Lakini baadaye ukimya huo ulitoweka, Edga akasema "Mimi nipo tayari".
"Vizuri sana, tunaweza kwenda?.."
"Ndio",Edga alibali.
"Naitwa Ndama,na huyu mwenzangu anaitwa Dominic", alijitambulisha mtu huyo na pia akamtambulisha na mwenzake.
"Mimi naitwa Edga".
"Ahahahaha safi, Edga amini kwamba utajiri upo mkono mwako endapo kama utakubali dili hili", aliongea Ndama kisha wakaambatana na Edga kuelekea kwenye gari. Sasa safari ikaanza, Kinondoni Studio walifika. Waliingia kwenye moja ya jumba bovu ambalo ndani palikuwa na vijana wakivuta bangi wengine wengine wakinywa pombe.
"Safi sana Ndama kwa kuongeza jopo,sasa kundi limetimia lakini sio rahisi kihivyi kumkubali huyu dogo mpaka tumpe mtihani kidogo" aliongea mtu mmoja ambaye alionekana kuwa ndio kiongozi wa kundi, aliitwa Boko.
"Sawa, hilo sasa lipo juu yenu", Ndama alijibu kisha akarejea ndani ya gari akaondoka zake. Sasa Edga anajikuta anaingia mkononi mwa Boko muhuni wa jiji, Boko na watu wake ni wezi. Kazi hiyo wanaifanya nyakati za usiku. Hivyo Edga baada kuungana na kundi hilo, alipewa mtihani wa kuvamia moja ya duka kubwa la nguo Kinondoni. Alifanikiwa, walimpongeza sana. Boko aliamini kuwa amepata mtu sahihi lakini baadaye Edga akapoteza sifa zake baada kumgomea Boko amri aliyotoa ambayo upande wake aliona ni vigumu kuweza kutekeleza. Ilikuwa jioni sana pindi wawili hao walipokuwa wakipanga mkakati kabambe wa kupora.
"Oya! Naombeni mnisikilize kwa umakini", Boko aliongea. Ukimya ukatawala kwa vijana wake akiwemo na Edga.
"Edga, kuna dili lipo mbele yetu, dili ambalo lipo kando na kile tunacho kifanya ila nina uhakika endapo kama hili dili litakwenda vema basi sisi wote hapa ni matajiri. Unatakiwa ukachukue nyaraka kwenye nyumba ya Mr Omon. Hili ni dili kubwa sana, na sisi tumekuteua wewe ili ulikamilishe..", alisikika akisema Boko kiongozi wa kundi,maneno hayo alikuwa akimwambia Edga.
"Hii nyumba ngumu sana, kuingia na kutoka pia. Hivyo basi umakini unahitajika ili dili hili liweze kulikamilisha. Kila sehemu kuna ilinzi, tena ulizi madhubuti", aliongeza kusema.
"Lakini nitawezaje wakati mimi bado mgeni katika mambo haya? Ni heri tungeshirikiana hata wawili braza", alijibu Edga kwa sauti ya woga. Boko alikasirika kusikia maneno hayo, alimtazama kwa hasira kisha akasema "Usinipangie kazi, unataka kusema miezi hii mitatu uliyojiunga nasi bado hujazoea? Hiki ni kipimo cha maisha, na kuishi ni kuchagua siku zote ukitaka kuruka sharti uagane na nyonga".
"Hapana bro, kwa hilo sipo tayari", alikacha Edga, akikataa agizo la kiongozi wake, kitendo ambacho kilimkera sana Boko. Na tangu siku hiyo maelewano baina yake na yao yakawa ya kususua huku kwa mara kadhaa wakimtenga kwenye ufanyaji wao wa kazi.. Edga alishusha pumzi ndefu baada kukumbuka hayo, alimgeukia Kayumba kwa sauti ya upole iliyojaa huzuni ndani yake akasema "Hivyo ndivyo ilivyokuwa Kayumba, maisha ni kuchangua. Mimi niliona yale ndio maisha,ingawaje mazingira ndio yaliyonishawishi baada dhumuni langu la kumtafuta dada yangu kuzimika ghafla kama mshumaa. Kayumba hapa nilipo sijui na wala sielewi kama dada yangu bado mzima au amepoteza maisha ", chozi lilimtoka Edga alipokwisha kusema maneno hayo. Kayumba alimsogelea akamgusa bega kisha akasema." Braza Edga pole sana kwa mitihani lakini hupaswi kukata tamaa, wewe ni shujaa. Ukijikwaa nyanyuka endekea na safari. Lakini pia siku zote kaa ukijua, milima haikitani lakini binadamu hukutana. Wasaka.."
"Tongee.." aliitikia Edga japo kwa sauti ya chini sana. Muda huo tayari ilikuwa yapata saa sita usiku, Edga na Kayumba walilala kwa dhumuni la kesho kuwahi kazini.
Siku iliyofuata ilikuwa siku njema sana, anga lote la jiji lilionekana kung'aa. Hali hiyo ilionyesha fika kuwa kuna dalili chache ya mvua kuonyesha. Edga aliachia tabasamu kisha akasema "Siku njema huonekana asubuhi"
"Naam! Abadani hujakosea", alijibu Kayumba kisha kila mmoja akaelekea kwenye kiwanja chake cha riziki. Edga alienda kubeba mizigo (Kuli) ilihali Kayumba naye alikwenda kuuza madafu.
Ilipotimu mnamo saa sita jua kali, anaonekana Kayumba akivuta kwama lake liliosheheni madafu, jasho la chumvi lilimvuja kichwa chini mikono nyuma. Punde si punde mlio wa honi ya gari ulisika wakati huo huo gari ndogo aina ya Noah yenye rangi nyeusi ilisimama mbele yake. Kayumba alikereka sana, akapayuka kwa hasira "Hii ni dharau", alisema huku akiliacha kwama lake nyuma na kisha kumfuata dereva ili ampe ya moyoni. Lakini alipo ukaribia mlango, kioo kilishushwa. Kayumba akamuona ni yule mrembo aliyemsaidia siku ya jana alipoporwa mkoba wake.
"Aah kumbe ni wewe mrembo", aliongea Kayumba kwa tabasamu bashasha..
"Ndio habari yako.. Ammh madafu unauza bei gani?.."
"Madafu mia nane tu", Kayumba alitaja bei. Mrembo huyo alihitaji dafu moja akatoa noti ya shilingi elfu kumi na wala hakuta kurudishiwa chenji. Kayumba alistaajabu sana, hakuamini macho yake aliamini kuwa wadada wazuri kama hao huwa na kasumba hasa kwa masikini kama yeye. Hivyo aliona kuna haja ya kufahamu jina lake, kwa tabasamu bashasha Kayumba akasema "Ni mara mbili sasa tunakutana, sio mbaya kama tukifahamiana hata kwa majina. Jina langu naitwa Kayumba", mrembo huyo binti wa kiarabu aliyevalia hijabu nyeusi aliachia tabasamu na akasema "Naitwa Najrat, kaa ukijua nametokea kukupenda", kwisha kusema hivyo akawasha gari akaondoka huku nyuma Kayumba akibaki mdomo wazi, maneno ya mrembo Najrat yakijirudia mara mbili mbili kichwani mwake ilihali tabasamu pana likitawala uso wake..
"Au ni jini? Kama hilitokuwa zali? .", alijuliza Kayumba..
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/3ao6Ybj
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment