Friday, May 3, 2019

Serikali kuendelea kumkomboa Mwanachi mnyonge




Serikali itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake ili kumkomboa mwananchi mnyonge ili kila mtu apate haki na kuwa sawa na mwingine na ashiriki kujenga uchumi wa viwanda. 

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga amesema hayo alipokuwa akizungumza na wasajili wasaidizi wa watoa huduma ya msaada wa kisheria nchini katika kongamano la watoa huduma ya msaada wa kisheria linalofanyika jijini Arusha. 

“Tumetunga Sheria ya Msaada wa Kisheria na tunaitekeleza kwa dhati, niwahakikishie kuwa tunafanya kila lililo ndani ya uwezo wa Serikali kumkomboa mwanchi mnyonge ili kila mmoja ajione ana haki sawa na mwenzake na aweze kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa viwanda ambayo ndio dira ya Serikali,” alisema Dkt. Mahiga. 

Amesema Serikali inatamani kuona upatikanaji haki na msaada wa kisheria unaongezeka na kuwafikia wananchi kule waliko na kuongeza kuwa wasajili wasaidizi wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha watoa huduma ya msaada wa kisheria katika maeneo yao wanawafikia wananchi wengi zaidi huku wakitoa huduma bora. 

Waziri Mahiga amewataka wasajili wasaidizi hao kutoka katika Halmashauri za Wilaya zote nchini, miji na majiji kuweka mikakati ya namna bora ya kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yao ili kufikia lengo la kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wengi na kwa kiwango kilicho bora. 

Amesema Serikali kupitia Sheria ya Msaada wa Kisheria No.1 ya Mwaka 2017 itaendelea kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa haki kwa wakati huku misingi ya utawala bora unaozingatia wajibu, sheria na demokrasia. 

Awali akizungumza katika Kongamano hilo Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome aliwakumbusha wasajili wasaidizi hao kuwa wasimamizi wazuri wa watoa huduma kwakuwa wao ni kiungo kati ya Serikali na watoa huduma hao. 

Aliwataka kuzingatia kuwa huduma ya msaada wa kisheria ni kazi ya kujitolea yenye kuhitaji uadilifu wa hali ya juu huku akiongeza kuwa kazi hiyo ni sawa na utoaji wa huduma za kiroho ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa dini mbalimbali nchini.



from UHONDO KITANDANI http://bit.ly/2LlG7EC

No comments:

Post a Comment