Friday, May 31, 2019

NI HATARI KUMPELEKA MTOTO CHINI YA MIAKA KUMI SHULE ZA.BWENII



Zipo sababu lukuki kwanini tunawapeleka watoto wetu shule za bweni ikiwa ni pamoja na kufiwa na wazazi wao, majukumu ya kusaka riziki kwa wazazi, elimu bora na zingine kadha wa kadha. Leo tutajadili athari za shule za bweni kwa watoto wenye umri mdogo. Umri wa chini ya miaka kumi na vipi elimu ya bweni inaweza kuwa ama chachu ya maendeleo ya mtoto au kumdidimiza kabisa kimaendeleo. Tuanze kwa kuangalia nini mtoto anaweza kufanya kulingana na umri wake na tutahitimisha na maoni yetu kuhusu umri wa shule ya bweni. Kuanzia umri wa miaka miwili hadi minne, mtoto huwa hajawa na ufahamu wa kutosha kujua mabaya na mema. Anachokipenda yeye ndicho kizuri na asichokipenda sio kizuri. Ni muhimu mzazi kuelewa hili ili kutoa muongozo na uangalizi kwa mtoto kwa upendo pasipo kumuhukumu kuwa ana tabia mbaya kwani bado uwezo wa kupambanua baya na jema ni mdogo mno.
Ingawa bado hajawa na uwezo binafsi wa kung’amua mwenyewe mambo mema na mabaya, mtoto mwenye umri wa miaka mitano hadi sita anaweza kufuata maelekezo ya mzazi vyema zaidi. Mtoto wa umri huu anaamini kila anachosema mzazi. Bado hana uwezo wa kujua kwa utashi wake mwenyewe lakini anao uwezo mkubwa wa kufuata maelekezo ya mzazi/mlezi. Wataalamu wa makuzi wanashauri wazazi wawe makini katika kutoa maelekezo katika umri huu kwani unachomweleza huwa ni kama mbegu unayoipanda maishani mwake. Misimamo yako katika yale unayoyaamini kama ibada, aina za vakula, nk. kwake hupokelewa kama kilivyo.
Umri wa miaka saba mpaka minane, mfumo binafsi wa kung’amua jema na baya wa mtoto unaimarika. Anaanza kujua mifumo ya maisha ya jamii husika na anao uwezo wa kuelewa madhara ya kutenda mabaya. Mara nyingi katika umri huu, wataalamu wa makuzi wanaeleza kuwa kutotenda makosa hujengwa katika uoga wa adhabu zinazotolewa na si kwa sababu nyinginezo. Kwa mfano, mtoto anajua kuwa sababu kubwa ya watu kutokuiba ni kukamatwa na polisi na si kwa sababu maadili mema yanaelekeza hivyo. Mara nyingi unaweza kusikia watoto wa umri huu wakitishiana kuwa wakifanya hivyo watakamatwa na polisi au mzazi atawaadhibu. Kama mzazi, ni vyema kumuelewesha mtoto kuwa watu hawaibi kwa sababu wanaogopa polisi tu bali wizi ni tabia mbaya na si maadili mema.
Jambo jema katika umri wa kuanzia miaka tisa na kuendelea, ni mtoto anaanza kuelewa maumivu ya kutenda kosa na faraja ya kutenda mema. Kadiri alivyolelewa, mtoto huumia anapotenda jambo analohisi si jema. Uelewa wa dhana ya kuwa ‘watendee wengine vile ambavyo ungependa utendewe wewe’ huingia, kwahiyo ni vyema mzazi/mlezi kuwa mfano mwema kwa mtoto. Usimtendee vitendo vya kionevu mtoto ukidhani kuwa haelewi, anaelewa. Jitahidi kutenda haki kwani utamuandaa kupenda kutenda haki kwa wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watoto wanajifunza kwako zaidi kuliko mtu mwingine. Muongoze mtoto awe na uelewa wa kung’amua jema na baya pasi kushurutishwa.
Kutokana na mifano hiyo ya kitaalamu kuhusu uwezo wa mtoto sanjari na umri wake, inakuwa rahisi kwetu kushauri kwamba iwapo sababu za kumpeleka mtoto shule ya bweni kabla ya umri wa walau miaka zaidi ya 10 zinaweza kuepukika, muache asome shule ya kutwa. Hii ni fursa adhimu kwako kupanda mbegu ya matarajio yako katika maisha ya mwanao kwani unapata kujenga ukaribu siku hata siku. Ikishindikana kuwa naye katika shule ya kutwa, basi hakikisha unajenga ukaribu na waangalizi/waalimu wake huko anakoishi ili angalau ujue namna bora ya kuhakikisha makuzi kwake.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 , ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na


from UHONDO KITANDANI http://bit.ly/2WxA3gB

No comments:

Post a Comment