Friday, May 3, 2019

'MAMBO YOTE YAENDESHWE KISHERIA' RAIS MAGUFULI




Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi, amesema, Serikali inatambua mchango wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika ( TLS) katika kuimarisha na kudumisha Utawala wa Sheria nchini.

Akasema wakati wote Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri kutoka TLS ilimradi kwamba, maoni au ushauri huo unajikita katika kujenga, kuimarisha, hauegemei upande wowote, wenye staha na usio na mashinikizo.

“ Kwanza niwashukuru sana kwa kuja kukutana na kufanya mazungumzo nami, niwapongeze wewe Rais kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa TLS pamoja na wote mliochaguliwa katika baraza la uongozi. Ni matumaini yangu kwamba, hamtawaangusha wanachama wenu waliowachagua, msiwaagushe tafadhali” Akasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuongeza

“Wakati wote Serikali imekuwa ikithamini sana mchango wenu na maoni yenu. Na kwa kweli mmekuwa mkitoa mchango na maoni mazuri sana, niwahakikishe kwamba Serikali wakati wote ipo tayari kushirikiana nanyi. Jambo la muhimu ni kuwa na majadiliano ( dialogue) pale ambapo mnaona kunajambo la kujadiliana kabla ya kulitolea matamko," amesema.

Ameendelea kwa kusema, "Niwahakikishe kwamba, Serikali kwa ujumla na hasa Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika uongozi wake anapenda sana Sheria na anataka mambo yafanyike kisheria na kwa kuzingatia sheria ” akasisitiza Profesa Kilangi

Mazungumzo kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ujumbe wa Balaza la Uongozi yaliyochukua zaidi ya masaa matatu, yalifanyika siku ya Alhamisi katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mitumba- Ihumwa Jijini Dodoma.


from UHONDO KITANDANI http://bit.ly/2VdtoZ6

No comments:

Post a Comment