Monday, March 2, 2020
Kuna mapenzi ya dhati dunia ya sasa?
MUNGU ni mwema! Jumamosi nyingine tunakutana kwenye darasa letu. Kama mada inavyojieleza hapo juu, kuna mapenzi ya dhati kwenye dunia ya sasa? Najua jibu la swali hilo kila mtu analo kutokana na mapito yake. Wengi wamejikuta kwenye maumivu makali ya mapenzi kutokana na jinsi watu wanavyoishi na kuyachukulia mapenzi. Tupo kwenye dunia ambayo usaliti ni kama vile fasheni.
Mwanaume ukiwa na mwanamke mmoja watu wanakushangaa. Mwanamke ukiwa unatembea kifua mbele na kusema unaye mwanaume wako mmoja, mnapendana mpaka pale kifo kitakapowatenganisha, basi wenzako wanakuona mshamba.
Ndugu zangu, swali hili lijibu unavyolijua lakini kimsingi kwa sasa kweli hali ni mbaya. Hakuna utulivu sana kwenye ulimwengu wa wapendanao. Wanaingia kwenye uhusiano, hawadumu sana wanaachana kutokana na vyanzo mbalimbali.
Je, tutafanyaje? Tusishiriki kabisa masuala ya mapenzi? Wanaoishi vizuri miaka mingi kwenye dunia hii wanawezaje?
Sikia rafiki, unachotakiwa kufanya kwenye dunia hii ni kujua kwamba unataka uishi vipi ili kuepukana na matatizo ya mara kwa mara. Kikubwa ni kuwa mtu wa kujitambua na umuelekeze mwenzako juu ya umuhimu wa kujitambua.
Aelewe kwamba nia na madhumuni yenu ni kutaka kuwa na mafanikio ya kimahusiano na hata kimaisha.
Baada ya kuelewa somo hilo sasa, mjue njia za kupita ili muweze kufika mbali. Kuna mambo inabidi muyaepuke ili kuweza kulinda penzi lenu. Msiwe watu wa kuchunguzana sana. Kuna mambo madogo-madogo mnapaswa kuyapotezea ili kufanya mambo yaende.
Ukimfuatilia sana mwenza wako unaweza kujikuta kila siku mnagombana bila sababu za msingi. Sisemi kwamba usimfuatilie mwenza wako lakini inatakiwa isizidi kupita kiasi. Jipe nafasi kidogo na kumpunguzia ile hali ya kuona unamfuatilia sana.
Jenga imani kwa mpenzi wako. Amini anakupenda, amini kwamba hatakusaliti. Endapo atathubutu kufanya huo usaliti, jua kwamba hilo ni kosa lake na acha hukumu yake itamfuata.
Kila mtu amuamini mwenzake. Lakini kama mwenzako anakuamini, jichunge na ujue kwamba unayo thamani kubwa kwake ndio maana amekuamini. Ibebe hiyo kama dira ya maisha yenu. Kila mmoja ajitambue kwamba ukimfanyia mwenzako ubaya jua unaweza kukurudia.
Usimfanyie mwenzako kitu kibaya kwani anaweza kukufanyia halafu na wewe hutakubali. Ili kuepuka hilo, acha kufanya masihala katika suala linalohusu mahusiano. Mpende mwenzako kwa moyo na akili zako zote.
Kuna maradhi, hivyo kila mmoja ajue kwamba ana wajibu wa kumlinda mwenzake. Ukifanya masihala kwenye suala la afya ujue kabisa unakikaribisha kifo mapema. Usikubali kumhatarishia mwenzako maisha yake.
Kuwa wa kwanza kumlinda ili naye akulinde. Hili liwe wazi kwenu na ikiwezekana muwe mnakumbushana mara kwa mara juu ya umuhimu wake. Kila mmoja alitambue hili, litawasaidia sana!
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/38eolcF
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment