Sunday, March 1, 2020

Hivi Ndivyo Tabia Zako za Asili Zinavyoweza Kuharibu Penzi Lako Jipya.



Kama mwenza wako ana tabia ya asili yoyote ile unayoihisi au kuifahamu, inakupasa kuwa makini naye kwani tabia hiyo au hizo zinaweza kukuathiri kisaikolojia au kimazingira.

Inaweza kukuathiri kisaikolojia kwa maana ni tabia ambayo ni ngumu kuiondoa katika damu ya mtu ambaye amezaliwa na tabia hiyo, hivyo itakulazimu kutumia muda mwingi katika kutafuta njia mbadala ya tabia asili ya mwenza wako.

Yawezekana ikawa ni vigumu kufahamu ni kwa namna gani unaweza kulizoea tatizo lake na kuishi naye katika uhusiano wa kimapenzi. Ila kama ulimpenda kwa dhati na hukulazimishwa kuwa naye, basi jifunze kumzoea na kuepuke baadhi ya tabia hizo.

Kwa upande wa kimazingira, tabia ya asili inawezekana kuwa ni mwenza wako kuwa mkorofi, mmbeya, malaya na kadhalika, jambo ambalo laweza kukugombanisha na wazazi, ndugu, majirani na hata marafiki zako, kwani kila kukicha kesi za ugomvi mtaani zitamhusu mkeo au mmeo, mara kapigana na fulani, katukanwa na fulani au unahisi katembea na Kulwa au Zulfa wa nyumba ya pili.

Kiukweli tabia za asili ni ngumu kuzizoea au kuziishi ila kwa kuwa umeshaamua kuwa mwili mmoja, huna budi kukubaliana na tabia hizo ili maisha yasonge.

Kwa ushauri wangu, ni vyema vijana wa sasa wakawa wazi katika maisha ya uchumba na kuishi maisha halisi na kwa muda, tena mkiwa karibu. Hii itasaidia kuzifahamu baadhi ya tabia za asili za umpendaye.

Kwa kuzifahamu, itakusaidia kufahamu ni kwa namna gani utaishi naye na kama ikitokea akakukwaza, basi utajua ni kwa namna gani utamvumilia au kumtuliza na maisha yakaendelea.

Uhalisia wa maisha ni eneo muhimu mno katika uhusiano. Kama kweli ni muungwana, jiachie, acha kujifanya ni mstaarabu ilihali wewe siyo mstaarabu, acha kujifanya unawapenda ndugu wa mwenza wako wakati moyoni unawachukia. Huo ni unafiki na ni maisha ya kuigiza ambayo ipo siku yatakushinda.






from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/2weh3It

No comments:

Post a Comment