Monday, March 2, 2020
Hasira; Chanzo kikubwa cha kuvunjika uhusiano!
LAITI kama kwenye dunia hii kila mmoja angejitambua, akafuata misingi sahihi ya uhusiano, basi kusingekuwa na ugomvi. Watu wangekuwa wanapishana tu kwenye mambo madogomadogo na kuwekana sawa kisha maisha yanaendelea, lakini kutokana na ugumu wa mioyo yetu, tunaifanya dunia kuwa uwanja wa mapambano. Watu wanagombana kila kukicha, wanapigana na hata kuuana, kisa mapenzi.
Ukifuatilia, chanzo kikuu cha matatizo haya huwa ni usaliti. Tamaa zinawatesa watu, wanashindwa kuishi njia kuu na kujikuta wakisababisha machafuko pindi watu wao wanaposhtukia mchezo huo.
Wengine hata siyo tamaa ya kitu au vitu, bali ni tabia tu. Hata ufanyeje ndivyo mtu alivyo tu. Yeye hawezi kutulia. Anataka huku, anataka kule; yaani ili mradi tu aufurahishe moyo wake kwa njia hiyo. Ukiachana na hayo, kipo chanzo kingine kikubwa cha machafuko ambacho ndicho nataka kukizungumzia leo. Chanzo hicho ni hasira. Hakuna asiyejua kwamba hasira ni hasara. Ukiziendekeza hasira siku zote huwezi kufanikiwa.
Kweli kwenye uhusiano kuna vitu vingi ambavyo ni maudhi. Unakutana na mtu, yeye maisha yake ni maudhi tu. Anakera, mbishi na mambo mengine kama hayo. Unapokuwa na mtu kama huyo ni changamoto mno kwenye mapenzi.
Ndiyo maana mara nyingi kwenye makala zangu nimekuwa nikisisitiza, epuka kuanzisha uhusiano na mtu pasua kichwa. Mtu ambaye yeye ugomvi ni kama ibada, hafai. Mtu ambaye mkiwa naye mnafurahi asilimia 3, 7 ni maudhi. Huyo muepuke mapema.
Lakini yote kwa yote, lazima tutambue hakuna binadamu aliyekamilika. Kila mtu ana upungufu wake, hivyo unaweza kujiona upo sahihi kumbe wewe ndiye tatizo. Ni vizuri kuruhusu akili yako ijifunze kutoka kwa wanaokuzunguka.
Hivyo basi, hata uwe na utashi wa namna gani wa kuwaepuka watu ambao ni kero kwenye maisha yako, lazima utambue bado huwezi kupata yule ambaye atakuwa amekamilika kwa asilimia mia. Lazima kuna mengine mtabadilishana mkiwa kwenye mapenzi.
Kikubwa unachotakiwa kukijua, mara baada ya kuanzisha safari yako ya uhusiano na mtu ambaye unaamini anafaa, basi jiepushe na kitu kinachoitwa hasira. Hasira ndugu zangu ndizo zinasababisha matatizo mengi kwenye jamii yetu.
Unapokutana na makwazo fulani kwenye uhusiano wako, kikubwa wewe ‘jipe muda’. Usikurupuke kufanya uamuzi. Kuwa na desturi ya kupuuza. Puuzia kwa muda, fanya jambo lingine ambalo litakutoa kwenye mawazo hayo.
Hata kama amekukwaza namna gani, unatamani kumfikishia ujumbe mhusika wala usiwe na haraka. Jipe muda wa kufanya mambo mengine, lile liweke kiporo. Utakapolizungumza baadaye ni tofauti na utakavyolizungumza papo hapo. Unapokurupuka kusema jambo wakati huo, ni hatari. Unaweza kutamka jambo ambalo ni baya mno. Kujipa muda kunalipa.
Kunalifanya pendo lizidi kuwa na uhai. Wanaokurupuka kufungua kinywa wakati wana hasira siku zote huwa wanajikuta pabaya. Unatamka neno ambalo litakuwa baya kwa mwenzako, naye anakujibu vibaya, kinachofuata hapo ni ugomvi ambao unaweza kusababisha hata vifo vyenu. Kama siyo vifo, basi mmoja anaweza kuishia gerezani na mwingine kaburini.
Hakuna cha maana mnachokuwa mmekipata zaidi ya kuishia kwenye matatizo makubwa. Ukitafakari kwa kina baada ya tatizo kutokea, unaona kumbe ungejizuia wala msingefikia hatua mliyofikia. Unalitafakari jambo lililosababisha maafa, unaliona ni dogo kabisa.
Jambo lenyewe halina kichwa wala miguu, lakini ndilo hilohilo limesababisha maafa. Ndugu zangu, tujichunge sana na hasira. Maudhi hayaepukiki, lakini tuchague amani. Tujipe muda wa kufikiria kidogo kabla ya kufanya jambo.
Kaa mbali na mpenzi wako unapokuwa na hasira. Ondoka, nenda mahali pengine ambako utakutana na mazingira na watu tofauti. Utachangamka, ukirudi kwa mtu wako huwezi kuwa yule wa kwanza. Mbaya zaidi kujitenga huku ndiko kunakofanya uhusiano uwe na umri mrefu. Wapendanao mnatakiwa kuvumiliana, kuchukuliana udhaifu na kuwa na upendo wa dhati.
from UHONDO KITANDANI https://ift.tt/32J5oO5
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment