Friday, May 3, 2019

SOKO LA MADINI LAZINDULIWA CHUNYA




Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amezindua Soko la Madini Chunya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais John Pombe Magufuli ya kutaka Wilaya ya Chunya kuhakikisha imekamilisha na kuzindua soko la madini ndani ya kipindi cha siku saba.

Uzinduzi huo ulishirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mary-Prisca Mahundi, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Anthony Tarimo na Kamishna Msaidizi- Uendelezaji wa Migodi kutoka Wizara ya Madini, Ali Ali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Profesa Msanjila alisema kuwa, tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha Sekta ya Madini inakua, inanufaisha watanzania pamoja na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa.

Akielezea mafanikio ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa rasilimali za madini, Profesa Msanjila alisema kuwa, ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wananufahika na rasilimali za madini, Serikali ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili Namba 5 ya Mwaka 2017; Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi Namba 6 ya mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123.

Aliendelea kueleza kuwa Serikali pia imefuta baadhi ya tozo ambazo zilikuwa kero kwa wafanyabiashara wa madini hususan wachimbaji wadogo na kufafanua kuwa tozo hizo kuwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18 na kodi ya zuio ya asilimia tano kwa wachimbaji wadogo.


from UHONDO KITANDANI http://bit.ly/2VaKYgc

No comments:

Post a Comment