Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amerudia kauli yake aliyoitoa Februari 11 mwaka huu alipoongea na wajumbe wa Kamati Tendaji ya chama cha madini Mkoa wa Morogoro– MOREMA ya kutaka Maeneo ya uchimbaji wa madini ambayo hayaendelezwi, leseni husika zifutwe na maeneo hayo kupatiwa wachimbaji wadogo.
Kauli hiyo ameirudia mwanzoni mwa wiki hii wakati akiufungua Mkutano wa Wadau wa Madini Mkoa wa Morogoro uliofanyika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Kigurunyembe katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambao unalenga kuboresha Sekta ya madini Mkoani humo ili kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Dkt. Kebwe amesema hakuna maana ya wachimbaji hao kuwa na maeneo makubwa lakini hawayafanyii kazi huku akiongeza kuwa fedha wanazolipa wachimbaji kwa mwaka katika maeneo yao ni kidogo ukilinganisha na fedha ambazo wangelipa wachimbaji wadogo endepo wangepewa maeneo hayo.
“Mimi Mkuu wa Mkoa napendekeza wanyang’anwe kwa sababu kwa upande wa utaratibu wa kisheria kwanza hawajaendeleza kwa hiyo utakuwa hujakosea, wanyang’anywe wapewe wachimbaji wadogo” alisema Dkt. Kebwe
Sambamba na hilo amemuagiza Afisa Madini Mkoa wa Morogoro kushirikiana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Clifford Tandari kuratibu zoezi la kufungua masoko ya madini kabla au ifikapo Mei 30 mwaka huu ili wachimbaji wasipate changamoto ya mahali pa kuuzia madini yao lakini pia Serikali kufaidika na madini hayo na kudhibiti utoroshwaji.
Aidha, Dkt. Kebwe ametumia fursa hiyo kuagiza chama cha Madini Mkoa wa Morogoro, Morogoro Region Mining Association – MOREMA kusajili wachimbaji wote wa madini waliopo Mkoani humo ili wafahamike huku akitaka MOREMA kusimamia sheria hususan utoroshwaji wa madini na kutofanya kazi hiyo kwa kificho na wale watakaokwenda kinyume na sheria wachukuliwe hatua za kisheria.
Naye Rais wa Shirikisho la vyama vya Wachimbaji madini Tanzania (FEMATA) Bw. John Bina, pamoja na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufuta utitiri wa kodi ambazo zilikuwa kero kwa wachimbaji madini amewataka wachimba hao kulipa kodi kwa Serikali kama walivyomwahidi Rais kwenye kikao chao cha mwezi Januari mwaka huu.
Sambamba na maagizo hayo, Bw. Bina ametumia fursa hiyo kulaani vitendo vilivyotokea katika Mikoa ya Mbeya na Shinyanga ambapo baadhi ya wachimbaji wametorosha madini hivyo kwenda kinyume na ahadi waliyoitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “kwa niaba ya wachimbaji wote napenda kulaani wale ambao jana katika Mkoa wa Mbeya na Kahama waliohusika kwenye wizi wa dhahabu … wale tunasema sisi sio wenzetu” alisisitiza John Bina.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa FEMATA, Kamishna Haroun Kinega amesema Serikali imesikia kilio cha wachimbaji wadogo wa madini cha uwepo wa maeneo makubwa kuhodhiwa kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi, tayari Tume ya madini inaendelea kufuta leseni za maeneo hayo na kutoa kwa wachimbaji wadogo.
from UHONDO KITANDANI http://bit.ly/2GSvPWT
No comments:
Post a Comment