Mpenzi msomaji wangu, leo nataka kuzungumzia namna unavyoweza kusherehekea Sikukuu ya Idd wakati mpenzi wako akiwa mbali na wewe. Je, uko mbali na mpenzi wako na hutakuwa naye sikukuu hii? Mbinu hizi hapa chini zitakusaidia sana…
MAWASILIANO
Hakikisha siku hiyo simu yako ina muda wa maongezi wa kutosha na chaji iko ‘full’. Hii ni kwa sababu mawasiliano ya mara kwa mara lazima yafanyike. Kwa siku hii haiwezi kuwa kero, mpigie simu kila unapojisikia na yeye kwa kuonesha kukujali anatakiwa kupokea.
Pia sms nzuri ndiyo wakati wake. Muandikie nyingi kadiri unavyoweza na yeye pia ili kukufanya ujisikie mwenye amani, atatakiwa kukujibu haraka iwezekanavyo. Hii ni mbinu ya kujiweka karibu naye na endapo utaitumia simu yako ipasavyo, hutajisikia mpweke na siku yako itapita huku ‘ukiwa na mpenzi wako’.
ZAWADI
Hiki ndiyo kipindi chake. Siku hiyo muandalie zawadi ambayo itamfanya ajione umemthamini. Zipo zawadi zinazoshauriwa kwa kipindi hiki cha sikukuu. Kwa mfano, unaweza kumnunulia nguo, viatu, vipodozi na vitu vingine ambavyo atavitumia siku hiyo. Kwa zawadi hizo ni lazima popote atakapokuwa atajisikia yuko nawe.
ATATOKA NA NANI?
Ni vizuri sana kujua huko aliko atatoka na nani kwenda wapi. Katika mazingira haya siyo mbaya kufanya ushushushu kujua kama atakavyokuambia ni sahihi. Ni vizuri pia huyo anayetoka naye ukawa na mawasiliano naye na awe ni mtu unayemuamini. Mfuatilie kwa karibu na wala usimuache akajichunga mwenyewe. Najua unaweza ukawa unamuamini lakini kujiaminisha zaidi siyo mbaya. Nasema hivi kwa kuwa sote tunajua siku za sikukuu zinavyokuwa.
Ni siku ambazo hata wale ambao hawakuwa na mawazo ya kusaliti wanajikuta wakifanya hivyo. Wapo ambao walitoka wakiwa wazima lakini wakashawishika kunywa pombe na wakafanya ambayo hawakudhamiria. Zungumza naye mara kwa mara na mkumbushe umuhimu wa yeye kujichunga na kutokusaliti kwa kuwa uko mbali naye.
MUWEKEE MIPAKA
Si vibaya pia ukamuwekea masharti na mipaka kwa siku hiyo. Kwa mfano unaweza kumkataza pia asitoke ikishafika saa moja. Awe nyumbani na wewe uwe nyumbani, muutumie muda huo kuzungumza mambomengi ambayo yatawaliwaza. Pia suala la pombe unaweza kumtaka asinywe hata akiwa yuko nyumbani.
Hivi utajisikiaje pale ambapo utampigia simu mpenzi wako na yeye akakuambia yuko nyumbani, amekunywa pombe na amelewa sana? Hata kama amelewa akiwa nyumbani lakini haileti picha nzuri. Sote tunajua madhara ya pombe kwa hiyo ni vizuri tukashauriana kutotumia kilevi hicho.
MSAPRAIZI
Zaidi ya yote, kuna kitu kinaitwa ‘sapraiz’. Kwa lugha ya kawaida neno hili linamaanisha kumfanyia mtu kitu ambacho hakukitarajia. Katika siku za sikukuu wengi wamekuwa wakiwafanyia wapenzi wao ‘sapraiz’ lakini kwa yule ambaye yuko mbali na mpenzi wake ‘sapraiz’ kubwa anayoweza kumfanyia ni kumtembelea. Hebu jiulize, wewe uko Mwanza na mchumba au mpenzi wako yako Dar.
Mmekuwa mkiwasiliana na akakueleza kuwa, kutokanana kubanwa na mambo hataweza kufika huku na wewe pia ukiwa huwezi kumfuata. Kutokana na mazingira hayo, mnaendelea kuwasiliana lakini siku moja kabla ya sikukuu, ukijua kabisa yeye atakuwa nyumbani, unapanda gari na kwenda Dar kisha ukifika unampigia simu na kumwambia aje akupokee stendi. Kwanza hataamini kile unachomwambia lakini akishakuona hiyo furaha yake haiwezi kuelezeka.
Wapo waliofanikiwa kufanya ‘sapraiz’ hizo na wameona jinsi walivyowafurahisha wapenzi wao. Lakini pia wapo waliofanya hivyo, wakaambulia maumivu kwani waligundua kuwa wenzi wao siyo waaminifu. Siyo mbaya sana kugundua hilo, kwani inakuwa rahisi kwako kuchukua uamuzi. Kuna sababu gani ya kuendelea na mpenzi ambaye siyo mwaminifu? Niishie hapo kwa leo, niwatakie maandalizi mema ya Sikukuu ya Idd.
from UHONDO KITANDANI http://bit.ly/2wEJsnT
No comments:
Post a Comment